Lady Jaydee, malkia Bongofleva ‘mwenye dunia’ yake kimuziki
Muktasari:
- Tayari ametoa albamu na nyimbo nyingi zilizopata mafanikio makubwa, huku akisalia kuwa chachu ya mafanikio kwa wasanii wa kike wanaochipukia. Fahamu zaidi.
KWA miaka mingi mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee ameachia nyimbo zilizogusa hisia za wengi kwa sauti yake ya kipekee na ujumbe mzito, na sasa ni mmoja wa wasanii wakubwa na wenye heshima katika muziki wa Tanzania.
Tayari ametoa albamu na nyimbo nyingi zilizopata mafanikio makubwa, huku akisalia kuwa chachu ya mafanikio kwa wasanii wa kike wanaochipukia. Fahamu zaidi.
1. Kuna wasanii wengi ambao Lady Jaydee aliwatazama kwa jicho la kujifunza (role models), baadhi yao ni Angelique Kidjo (Benin), Whitney Houston (Marekani), Yvonne Chaka Chaka (Afrika Kusini) na Dr Dre (Marekani).
2. Albamu ya pili ya Lady Jaydee, Binti (2003) kwa asilimia kubwa imetayarishwa na Miikka ‘Mwamba’ Kari kutokea Finland, ambapo alishirikiana na baadhi ya wakongwe katika upigaji wa ala (live instruments).
3. Lady Jaydee ameshirikiana na wasanii wengi wa kike ambao hata wengine aliwahi kushindanishwa nao akiwemo Ray C. Hata hivyo, hajawahi kurekodi na Stara Thomas aliyevuma kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Mimi na Wewe (2000).
4. Wimbo uliomtoa Mwasiti kimuziki chini ya Tanzania House of Talent (THT), Niambie (2006) ulitayarishwa katika studio binafsi ya Lady Jaydee, huku video yake ikisimamiwa na Director Adam Juma kutokea Visual Lab.
5. Wasanii wa kimataifa ambao Lady Jaydee amewahi kutamani kushirikiana nao ni Dr Dre ambaye pia ni mtayarishaji na mwanzilishi wa Aftermath Entertainment, lebo ambayo imewatoa mastaa kama Eminem, 50 Cent na kadhalika. Mwingine ni Usher Raymond IV, mkali wa miondoko ya RnB na Pop kutokea Marekani ambaye wengi wanamkumbuka kupitia wimbo wake, Yeah! (2004) akishirikiana na Lil Jon na Ludacris.
6. Aliyekuwa msanii wa bendi ya Orchestra Makassy tangu mwaka 1983, na mtaalamu wa kupiga gitaa la bezi, Andy Swebe a.k.a Ambasador ambaye alifariki Desemba 2011, ndiye alipiga gitaa katika wimbo wa Lady Jaydee, Siri Yangu (2003).
7. Wimbo wa Lady Jaydee, Siwema (2003), awali uliimbwa na mwanamuziki wa dansi, Marijani Rajab aliyefariki Machi 1995, hivyo Jide yeye ameurudia tu ikiwa ni baada ya kupata ruhusa na ulijumuishwa katika albamu yake ya pili.
8. Lady Jaydee anawataja Sugu, Profesa Jay kama ndugu zake na si marafiki tena kutokana wamekuwa naye katika mambo mengi hasa ya kimuziki. Vilevile ameshirikiana na wote, Jide ameshiriki katika nyimbo za Sugu kama Mambo ya Fedha na Muda Mrefu, huku kwa Profesa Jay zikiwa ni Bongo Dar es Salaam, Ndio Mzee na Nimeamini.
9. Wimbo wa Kidum kutokea nchini Burundi, Nitafanya (2011) akimshirkisha Lady Jaydee, una matoleo (version) mawili ambayo wasanii hao waliyaachia kwa sababu maalumu, na hadi sasa ni moja ya kolabo kali za Afrika Mashariki.
10. Akiwa tayari ametoa albamu 10 huku ya 11 ikitarajiwa kuachiwa 2027, Lady Jaydee anaamini albamu zake zote zina ubora uliolingana kwa sababu aliweka jitihada akitegemea ziwe na matokeo makubwa zikiacha kumbukumbu kwa wasikilizaji.