Chuchu aficha mimba, akataa baby shower
Muktasari:
- Ujauzito huo umeibua gumzo kubwa baada ya Ray kuweka picha akiwa na Chuchu, huku mwigizaji huyo akionekana wazi kuwa katika hatua za mwisho za ujauzito. Jambo hilo limewafanya mashabiki wao kumiminika kwa pongezi.
MWIGIZAJI wa filamu nchini, Chuchu Hansy, amevunja ukimya kuhusu ujauzito wake unaoendelea kuvuma mitandaoni, akifichua kuwa yeye na mwenza wake wa muda mrefu, Vincent Kigosi ‘Ray’, wanatarajia kupata mtoto wao wa pili.
Ujauzito huo umeibua gumzo kubwa baada ya Ray kuweka picha akiwa na Chuchu, huku mwigizaji huyo akionekana wazi kuwa katika hatua za mwisho za ujauzito. Jambo hilo limewafanya mashabiki wao kumiminika kwa pongezi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ray alieleza furaha yake kwa ujio wa mtoto huyo, huku akimshukuru Chuchu kwa kumpa tena zawadi hiyo ya familia.
“Maneno hayatoshi kueleza furaha na shukrani nilizonazo moyoni. Unakaribia kunipa zawadi ya thamani kuliko zote, mtoto wetu wa pili,” aliandika Ray.
Ray aliendelea kumshukuru Mungu kwa baraka hiyo, huku akiahidi kuendelea kumpenda, kumthamini na kusimama na Chuchu katika kila hatua ya maisha yao.
Lakini wakati Ray akifungua pazia kuhusu ujauzito huo, Chuchu ameliambia Mwanaspoti kuwa yeye hakutaka kufanya ujauzito huo kuwa jambo la kila siku mitandaoni. Ndiyo maana aliamua kuuweka faragha na kuonyesha wakati ambao tayari umefika hatua kubwa.
Chuchu amesema amefurahi sana kupata ujauzito huo, lakini yeye si mtu wa kufanya mbwembwe kuhusu maisha yake binafsi.
“Nimefurahi sana, ila mimi huwa sina mbwembwe. Ndiyo maana nimeuficha ujauzito wangu, nimeamua kuonyesha ukiwa tayari umefika hatua hii,” amesema Chuchu.
Kauli hiyo inaendana na namna ambavyo amekuwa akiishi maisha yake ya kifamilia kwa utulivu, licha ya uhusiano wake na Ray kufuatiliwa kwa karibu na mashabiki kwa miaka mingi.
Baby shower hakuna
Na kama kuna jambo lingine ambalo Chuchu ameliweka wazi ni kwamba mashabiki wasitarajie kumuona akifanya sherehe kubwa ya baby shower kabla ya kujifungua, kama ilivyo kwa baadhi ya mastaa wengine.
Chuchu amesema kwa sasa hana mpango wa kufanya sherehe hiyo, akieleza kuwa mambo ni mengi na ataamua kuifanya baada ya mtoto kuzaliwa.
“Baby shower sina mpango nayo kwa sasa. Mambo ni mengi, nitafanya baada ya mtoto kuzaliwa,” amesema.
Hivyo, tofauti na baadhi ya mastaa ambao ujauzito wao huambatana na baby shower, picha za kila hatua na matukio mbalimbali ya kuhesabu siku za kujifungua, Chuchu amesema yeye ameamua kwenda kwa utaratibu wake.
RAY NAYE ALIFURAHI
Kwa upande wake, Ray hakuficha furaha yake baada ya ujauzito huo kuwekwa hadharani, akitumia ujumbe wake kumshukuru Chuchu na Mungu kwa zawadi hiyo.
Ujumbe wa Ray umewafanya mashabiki wao kurejea historia ya wawili hao, ambao kwa miaka mingi wamekuwa miongoni mwa mastaa waliovuta hisia kutokana na safari yao ya mapenzi.
Ray na Chuchu wamejaaliwa mtoto wao wa kwanza wa kiume, Jaden, mwaka 2017.
Ujio wa Jaden ulikuwa katika kipindi ambacho uhusiano wao ulikuwa ukifuatiliwa kwa karibu, huku Chuchu baadaye akiwahi kueleza changamoto mbalimbali alizokutana nazo katika uhusiano huo.
Mwaka 2017, Chuchu aliwahi kuzungumzia suala la ndoa yao na kueleza kwamba wakati huo hawakuwa wakiliwaza kwa haraka, huku wakijikita zaidi katika maisha yao na malezi ya mtoto wao.
Suala la ndoa limeendelea kuwa sehemu ya historia yao, huku kwa miaka tofauti Ray na Chuchu wakiulizwa mara kwa mara lini watafunga rasmi ndoa.
Mwaka 2014, Chuchu aliwahi kuzungumza na Mwanaspoti kuhusu suala hilo, akieleza kuwa walikuwa wachumba na ndoa ingefungwa kwa wakati ambao Mungu angewawezesha.
Miaka iliyofuata, suala hilo liliendelea kuwa gumzo huku Chuchu akieleza nyakati tofauti kuhusu uhusiano wao na changamoto zilizokuwapo, ikiwemo tofauti zao za kidini.
Mwaka 2025, Chuchu aliendelea kuzungumzia suala la kuolewa na Ray, huku ikiripotiwa kuwa tofauti ya dini ni miongoni mwa mambo yaliyowahi kufanya suala la ndoa yao lisionekane kuwa rahisi.
Kwa hiyo, licha ya kuwa wamekuwa pamoja kwa miaka mingi, wamepata mtoto na sasa wanatarajia mwingine, wawili hao hawajawahi kufunga ndoa rasmi.
Ujio wa mtoto huyu wa pili unaifanya familia yao kuingia ukurasa mwingine, miaka takribani tisa baada ya kumpokea Jaden.
Jambo hilo pia linaonekana kutimiza matamanio ambayo Ray aliwahi kuyaeleza hapo nyuma.
Mwaka 2019, Ray aliwahi kusema alikuwa na mpango wa kupata mtoto mwingine na Chuchu, akieleza kuwa hakukuwa na sababu ya kutafuta mwanamke mwingine kwa ajili ya kupata mtoto.
Mwaka 2024 pia, suala la mtoto wa pili liliibuka tena, huku Ray akiwataka watu kuwaacha yeye na familia yake kupanga muda wao wenyewe kuhusu suala hilo.
‘Ray amenilinda vizuri’
Mbali na suala la ujauzito na baby shower, Chuchu amezungumzia pia namna anavyojisikia katika kipindi hiki, hasa baada ya mijadala ya mitandaoni kuhusu mabadiliko ya mwili na uso kwa baadhi ya wanawake wajawazito.
Amesema yeye hajavimba uso wala pua, akihusisha hali hiyo na namna alivyokuwa akihudumiwa na Ray katika kipindi hiki.
“Mimi uso wala pua sijavimba, Ray amenilinda vizuri, nimetritiwa,” amesema Chuchu.
Kauli hiyo imeongeza ladha kwenye habari yao, huku ikionyesha upande mwingine wa Ray katika kipindi ambacho mwenza wake anabeba ujauzito wa mtoto wao wa pili.
Kwa sasa, Chuchu amesema hana haraka ya kufanya sherehe kubwa ya ujauzito, badala yake anasubiri mtoto azaliwe ndipo afanye sherehe yake.
Na wakati yeye akichagua ukimya na kutokuwa na mbwembwe, Ray tayari ameshaweka wazi furaha yake.