Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rany Kida; King of Dance mwenye simulizi moto ya dansi

KIDA Pict
KIDA Pict

Muktasari:

  • Miongoni mwao ni Rany Kida, dansa kijana ambaye amejijenga katika tasnia ya dance Tanzania na sasa anafanya kazi na wasanii mbalimbali, huku akisisitiza kuwa hakupitia mgongo wa msanii mkubwa kufikia alipo.

KATIKA dunia ya burudani, kuna watu wanaofika kwenye kilele cha mafanikio kupitia majina makubwa ya wasanii, lakini pia wapo wanaopambana wenyewe hadi kujenga utambulisho unaowafanya watambulike bila kutegemea jina la mtu mwingine.

Miongoni mwao ni Rany Kida, dansa kijana ambaye amejijenga katika tasnia ya dance Tanzania na sasa anafanya kazi na wasanii mbalimbali, huku akisisitiza kuwa hakupitia mgongo wa msanii mkubwa kufikia alipo.

Safari yake inaanzia Biharamulo mkoani Kagera, ambako alilelewa licha ya kuwa na asili ya Kinyakyusa. Jina lake halisi ni Imran Said, lakini jina la Ran Kida limebeba historia ya safari yake katika unenguaji.


KID 03

RANY KIDA IMETOKA WAPI?

Akieleza chimbuko la jina hilo, Rany Kida anasema ‘Ran’ amelitengeneza kutoka kwenye jina lake halisi la Imran, huku ‘Kida’ likiwa na maana ya King of Dance, jina alilopewa baada ya kushinda mashindano mwaka 2018.

“Ran nimetengeneza kutoka kwenye jina langu Imran, nimechukua sehemu ya mwisho ya jina hilo. Kida ni King of Dance, ambacho nilikipata baada ya kushinda mashindano mwaka 2018. Kwa hiyo Rany Kida ni kama Ran King of Dance,” anasema.

Ushindi huo ukawa sehemu muhimu katika safari yake na kumpa utambulisho ambao baadaye ungeendelea kukua katika ulimwengu wa dance.


HAKUBEBWA NA STAA

Tofauti na baadhi ya madansa ambao majina yao yamekua zaidi baada ya kufanya kazi na wasanii wakubwa, Rany Kida anasema yeye amepitia njia yake mwenyewe.

Njia hiyo haikuwa nyepesi, kwani alikutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kukataliwa na kudhulumiwa, lakini hakuruhusu hali hizo zimrudishe nyuma.

“Nilipitia changamoto nyingi kwenye safari yangu. Kuna wakati nilikataliwa na hata kudhulumiwa, lakini sikukata tamaa. Niliendelea kupambana mpaka nikajenga jina langu mwenyewe,” anasema.

Leo hii, Rany Kida anafanya kazi na wasanii mbalimbali kulingana na mahitaji ya kazi zao.

Anasema hana bei moja kwa kila msanii anayehitaji huduma yake, kwa sababu kiwango cha malipo hutegemea aina ya kazi pamoja na ukubwa wa msanii.

“Sina bei moja ambayo namtoza kila msanii. Kuna msanii anayeanza na kuna msanii mkubwa, hivyo naangalia kazi yenyewe na msanii anayehitaji huduma yangu,” anasema.

Miongoni mwa wasanii ambao amewahi kufanya nao kazi ni Jason Derulo, ambaye aliwahi kumlipa kwa ajili ya kushiriki katika video yake.


KID 02

KULEA VIPAJI

Rany Kida haishii kwenye majukwaa na video za muziki. Ameingia pia kwenye ufundishaji wa kunengua kupitia madarasa anayoyaendesha.

Kila Jumamosi huwa na darasa la jamii, ambapo mshiriki hulipia Sh5,000, huku Jumapili ikiwa maalumu kwa private classes zinazohitaji miadi.

“Jumamosi huwa nafanya darasa la jamii ambapo mtu anaingia kwa Sh5,000. Jumapili huwa kuna private classes kwa wale wanaohitaji mafunzo binafsi na wanaweka miadint,” anasema.

Kupitia madarasa hayo, anasema amekuwa akikutana na vipaji mbalimbali ambavyo anajaribu kuvipa nafasi ya kukua.

Anatoa mfano wa mwanafunzi wake aliyepata fursa ya kufanya dili la matangazo, baada ya yeye kusaidia kuunganisha familia ya mtoto huyo na mmiliki wa biashara hiyo. “Mimi furaha yangu ni kuona mtu ninayemfundisha anapata nafasi. Kuna mwanafunzi wangu nilimsaidia mpaka akapata dili la matangazo. Nilisaidia kuunganisha familia yake na mwenye biashara na mambo yakaenda.”


HESHIMA KWA MADANSA

Pamoja na hatua alizofikia, Rany Kida bado anaona kuna jambo kubwa linalohitaji kubadilika katika tasnia ya burudani: namna madansa wanavyothaminiwa. Kwa mtazamo wake, dansa ana mchango mkubwa katika kufanya muziki uonekane na hata kusambaa mitandaoni, lakini mara nyingi bado huonekana kama mtu wa pembeni katika uzalishaji wa kazi za muziki.

“Dansa ana mchango mkubwa sana kwenye muziki. Kuna nyimbo zinakuwa kwa sababu ya dance, lakini bado dancer anaonekana kama extra. Kuanzia kwenye malipo mpaka huduma tunazopata kwenye location, bado kuna changamoto,” anasema.

Anasema kwake, si kila wimbo anaweza kuucheza au kuufundisha kwa sababu tu umetoka kwa msanii fulani.

“Mimi lazima niupende kwanza wimbo. Siwezi kucheza au kufundisha wimbo kwa sababu tu nataka msanii anione au nipate comments. Lazima muziki wenyewe univutie.”


DANCE IMEMLISHA

Kwa Rany Kida, dance si hobby wala shughuli ya pembeni. Ni sehemu kubwa ya maisha yake na chanzo kikuu cha kipato.

Anasema takribani asilimia 70 ya kipato chake kinatokana na dansa huku asilimia 30 ikitokana na shughuli nyingine za kibiashara na fursa alizozipata kupitia mtandao alioujenga katika sanaa hiyo.

“Kwa sasa kama nikigawa kipato changu, kama asilimia 70 kinatokana na dance. Asilimia 30 nyingine ni biashara na fursa ambazo nimezipata kupitia mtandao wangu wa dansa”

Mafanikio hayo yamefanya pia aweze kumsaidia mama yake mzazi, ambaye kwa sasa anamhudumia kupitia kipato anachopata katika shughuli zake za sanaa.

“Dansa imenisaidia sana. Hata mama yangu namhudumia kupitia kile ninachokipata kwenye dance. Hilo ni jambo ambalo linanipa nguvu zaidi ya kuendelea.”


KID 01

TASWIRA YA MADANSA

Katika jamii, wakati mwingine madansa hupewa taswira ya kuwa watu wa starehe kupita kiasi au wanaohusishwa na matumizi ya vilevi.

Ran Kida anapinga mtazamo huo na kusema nidhamu ni sehemu muhimu ya mafanikio kwa mtu anayechagua kuwa mnenguaji kama taaluma.

“Watu wanaweza kuwa na picha tofauti kuhusu madansa, lakini si kila dancer ni hivyo. Mimi sijawahi kutumia kilevi cha aina yoyote. Ukiamua kufanya unenguaji kama kazi, unatakiwa kuwa na nidhamu,” anasema.

Kwa vijana wanaotaka kufanikiwa katika sanaa, anataja mambo manne anayoyaona kuwa muhimu.

“Kwanza uwe na nidhamu, pili mweke Mungu mbele, tatu zingatia muda na nne epuka kabisa matumizi ya vilevi. Hayo ni mambo muhimu sana kwa kijana anayataka mafanikio,” anasema.


NDOTO KUANZISHA CHUO

Pamoja na kunengua, Rany Kida ana vipaji vingine kama ubunifu wa mavazi na kuimba, lakini ndoto yake kubwa ni kuona dansi ikiingia katika mfumo rasmi zaidi wa elimu.

Anataka siku moja kuanzisha chuo cha unenguaji ambayo itakuwa sehemu ya vijana kujifunza kunengua kama taaluma na si shughuli ya kucheza mitaani pekee. “Nataka siku moja niwe na 'Dance Academy' yangu. Nataka vijana wapate sehemu rasmi ya kujifunza kunengua siyo kucheza tu mitaani, bali wajue kwamba hii ni taaluma,” anasema

Mbali na hilo, ana ndoto ya kuona dance ya Tanzania ikivuka mipaka na kupata nafasi katika soko la kimataifa ndani ya miaka mitano ijayo.

“Ndoto yangu ni kuona dance ya Tanzania inafika kimataifa. Ndani ya miaka mitano ijayo nataka kuona nimefanya kitu kikubwa ambacho kitaifanya dance yetu iheshimike hata nje ya Tanzania.”

Kutoka Biharamulo hadi kwenye majukwaa ya dance, Rany Kida anaamini safari yake bado haijafika mwisho. Kwake, kunengua siyo dansi tu.

Ni taaluma, ni kipato, ni fursa na, zaidi ya yote, ni njia anayoamini inaweza kubadili maisha ya vijana wengi.