Rungu la BASATA latua kwa Nandy, Harmonize na wengine
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na BASATA usiku wa kuamkia leo imemtaja Harmonize, jina halisi Rajab Abdul Kahali, akihusishwa na video ya wimbo wake uitwao Kudos, ambayo baraza hilo limesema haikuzingatia maadili ya Mtanzania na inavunja heshima ya msikilizaji au mtazamaji.
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limechukua hatua dhidi ya wasanii Harmonize na Nandy, likiwataka kulipa faini pamoja na kuchukua hatua nyingine kutokana na ukiukwaji wa maadili katika kazi zao za sanaa.
Taarifa iliyotolewa na BASATA usiku wa kuamkia leo imemtaja Harmonize, jina halisi Rajab Abdul Kahali, akihusishwa na video ya wimbo wake uitwao Kudos, ambayo baraza hilo limesema haikuzingatia maadili ya Mtanzania na inavunja heshima ya msikilizaji au mtazamaji.
Kwa mujibu wa BASATA, Harmonize hakuwasilisha utetezi wala maelezo mbadala hadi wakati uamuzi huo ulipotolewa. Kutokana na hilo, baraza limeamuru video hiyo kushushwa kwenye mitandao yake ya kijamii, alipe faini ya Sh5 milioni ndani ya siku 14 na asijihusishe na kazi za sanaa kwa namna yoyote hadi atakapotekeleza maamuzi hayo.
Katika hatua nyingine, BASATA imemchukulia hatua pia muongozaji wa video hiyo, Kennedy David Sanga, ambaye amesema alitenda kosa la kimaadili kwa kuongoza video hiyo iliyokiuka maadili ya Mtanzania.
Sanga naye ameamriwa kushusha video hiyo kwenye mitandao yake, kulipa faini ya Sh5 milioni ndani ya siku 14 na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.
Mbali na Harmonize na Sanga, BASATA imetangaza hatua dhidi ya Avil Contractors Company Ltd, waandaaji wa shindano la Miss Grand Tanzania, kwa kuendesha shindano hilo bila kuwa na kibali cha tukio kutoka BASATA.
Kampuni hiyo imepewa faini ya Sh3 milioni na imeamriwa kutokujishughulisha na kazi za sanaa hadi itakapotekeleza uamuzi huo.
NANDY NAYE
Kwa upande wake, msanii Faustina Charles Mfinanga, maarufu Nandy, amefungiwa kwa kosa la kuvaa nguo ambayo BASATA imeieleza kuwa haikuwa na staha na ilivunja heshima ya mtazamaji wakati akitumbuiza katika fainali ya Miss Universe Tanzania 2026 iliyofanyika Haddypro, Dar es Salaam.
Tofauti na Harmonize, BASATA imesema Nandy alikiri kosa, akashusha video iliyotajwa kutokuwa na maadili kwenye mitandao yake ya kijamii na kulipa faini ya Sh3 milioni.
Kutokana na kutekeleza masharti hayo, Nandy ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za sanaa, lakini akiwa chini ya uangalizi wa BASATA.
BASATA pia imeichukulia hatua Millen Privé & Co. Lifestyle Limited, mwandaaji wa Miss Universe Tanzania, kwa kuruhusu tukio hilo la kimaadili kutokea.
Kampuni hiyo imeamriwa kulipa faini ya Sh3 milioni ndani ya siku 14 na imepewa onyo kali, huku ikitakiwa kuwa makini zaidi katika utekelezaji wa shughuli zake za sanaa.
Katika taarifa hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Edward Buganga, amewataka wasanii na wadau wa sanaa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili ya Mtanzania wanapotekeleza shughuli zao.
Hatua hizo zinakuja wakati BASATA ikiendelea kusisitiza utekelezaji wa Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la Mei 22, 2026, ikiwataka wadau wa sanaa kuhakikisha kazi na matukio wanayohusika nayo yanafuata taratibu zilizowekwa.