Nyota Bigi yarudi kusaka vipaji
Muktasari:
- Serengeti Lite kwa kushirikiana na KUNTA Africa, imetangaza kurejea kwa Nyota Bigi msimu wa pili, safari hii ikitanua wigo wa kusaka vipaji katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
KAMA una kipaji cha kuimba, kucheza, kuigiza, kuchekesha au kubuni na umekuwa ukikificha kwa muda mrefu, sasa ni wakati wa kukitoa hadharani.
Serengeti Lite kwa kushirikiana na KUNTA Africa, imetangaza kurejea kwa Nyota Bigi msimu wa pili, safari hii ikitanua wigo wa kusaka vipaji katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Usaili wa kusaka nyota wapya utaanzia Dar es Salaam, Oktoba 3, 2026 kabla ya kuhamia Mwanza Oktoba 10, 2026, Arusha Oktoba 17, 2026 na Dodoma Oktoba 24, 2026.
Msimu huu unalenga kuibua vipaji mbalimbali vya Watanzania, ikiwamo uimbaji, kucheza, uigizaji, uchekeshaji, ubunifu, uanamitindo pamoja na vipaji vingine vya ubunifu ambavyo bado havijapata nafasi ya kuonekana.
Nyota Bigi ni sehemu ya kampeni ya Serengeti Lite inayokwenda kwa kaulimbiu ya “Lite Your Imagination”, inayolenga kuwahamasisha vijana kuamini katika uwezo wao, kuonyesha ubunifu wao na kutumia vipaji walivyonavyo kama sehemu ya safari yao ya mafanikio.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Kampuni ya Vinywaji ya Serengeti, Henry Esiaba, amesema Nyota Bigi inalenga kutoa jukwaa kwa vipaji vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Tanzania ina vipaji vingi, lakini changamoto kubwa kwa baadhi ya vijana ni kukosa nafasi ya kuvionesha mbele ya hadhira.
“Tuna vipaji vingi katika kila kona ya nchi hii. Ila kinachokosekana wakati mwingine ni nafasi ya kuonekana. Nyota Bigi ipo kwa ajili ya kuwapa vijana wa Tanzania jukwaa hilo,” amesema Esiaba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bia wa Kampuni hiyo, Rhona Namanya, amesema msimu wa pili umeongezwa ukubwa kwa kupeleka mchakato wa kusaka vipaji katika miji zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.
“Mwaka huu tunafurahi kuwajulisha Watanzania kuwa msimu wa pili utakwenda katika miji mbalimbali Tanzania, ukilinganisha na mwaka jana ambapo tulitafuta vipaji hapa Dar es Salaam tu,” amesema Rhona.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, usajili tayari umefunguliwa kupitia msimbo wa QR wa Nyota Bigi, tovuti ya Nyota Bigi, WhatsApp au simu.
Waombaji wanatakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 35, kitambulisho halali pamoja na video fupi inayoonyesha kipaji chao.
Usaili utafanyika kwa njia ya ana kwa ana na mtandaoni, hatua inayolenga kuwapa nafasi washiriki kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza.
Safari ya Nyota Bigi haiishii kwenye mashindano pekee. Wale watakaofanikiwa kuvuka hatua mbalimbali wanaweza kupata fursa za kuingia katika maeneo mapana ya tasnia ya ubunifu, ikiwamo mitandao ya kijamii, uanamitindo, burudani, usimamizi wa vipaji na studio za kurekodi.
Kwa Serengeti Lite, mpango huo unalenga kuifanya kaulimbiu ya “Lite Your Imagination” kuwa vitendo kwa kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha kile wanachoweza kufanya badala ya kubaki wakifikiria kuhusu vipaji vyao.