Mr Cheeks, Jay Moe hip hop itakavyoongea Chuga
Muktasari:
- Mr Cheeks anayefahamika kwa historia yake ndani ya kundi la Lost Boyz, amesema kazi hiyo na Jay Moe ipo kwenye hatua za mwisho, hivyo mashabiki wanaweza kutarajia kusikia matokeo ya muunganiko huo.
RAPA mkongwe kutoka Marekani, Terrance Cocheeks Kelly maarufu kama Mr Cheeks yupo nchini Tanzania akiwa na jambo zito mezani, kukutana na mkongwe wa hip hop, Juma Mchopanga maarufu Jay Moe kwa ajili ya kutengeneza kolabo inayotarajiwa kuunganisha sauti mbili kutoka pande tofauti za dunia.
Mr Cheeks anayefahamika kwa historia yake ndani ya kundi la Lost Boyz, amesema kazi hiyo na Jay Moe ipo kwenye hatua za mwisho, hivyo mashabiki wanaweza kutarajia kusikia matokeo ya muunganiko huo.
Kolabo hiyo inakuja wakati Tanzania ikisherehekea miaka 30 ya Bongo Flava, huku tamasha kubwa likitarajiwa kufanyika leo, Septemba 19, 2026, kwenye Viwanja vya General Tyre jijini Arusha unakoweza kupaita Chuga.
Kwa hiyo ujio wa Mr Cheeks hauishii kwenye kutumbuiza pekee, bali pia umefungua nafasi ya kuwakutanisha mastaa wa Hip Hop kutoka Marekani na Tanzania kwenye kazi moja.
MR. CHEEKS, MKONGWE WA HIP HOP
Mr. Cheeks si jina jipya kwenye Hip Hop ya Marekani. Amejenga jina lake kwa muda mrefu, hasa kupitia kundi la Lost Boyz lililokuwa likitokea Queens, New York.
Kundi hilo lilikuwa na Mr. Cheeks pamoja na Freaky Tah, Pretty Lou na DJ Spigg Nice. Katika miaka ya 1990, Lost Boyz walipata umaarufu kupitia nyimbo mbalimbali zilizowafanya wafahamike zaidi kwenye Hip Hop ya Marekani.
Miongoni mwa nyimbo zao zilizojulikana ni Lifestyles of the Rich & Shameless, Jeeps, Lex Coups, Bimaz & Benz na Renee.
Lost Boyz walitoa albamu yao ya kwanza, Legal Drug Money, mwaka 1996. Mwaka uliofuata walitoa Love, Peace & Happiness, kisha mwaka 1999 wakatoa LB IV Life.
Baada ya safari yake na Lost Boyz, Mr. Che eks aliendelea na muziki akiwa solo. Mwaka 2001 alitoa albamu yake John P. Kelly, iliyokuwa na wimbo Lights, Camera, Action, ambao ulifanya vizuri na kufika nafasi ya 14 kwenye chati ya Billboard Hot 100.
TANZANIA ANAIJUA
Ujio wa Mr. Cheeks Tanzania una historia yake. Kabla ya safari hii, Lost Boyz waliwahi kutumbuiza nchini Tanzania mwaka 1998. Hivyo, kurejea kwake Tanzania baada ya miaka mingi kunamrudisha kwenye nchi ambayo tayari ina sehemu katika historia yake ya muziki.
Safari hii anakuja katika kipindi ambacho Bongo Flava inatimiza miaka 30, jambo linalofanya uwepo wake kuwa sehemu ya sherehe zinazokumbusha safari ndefu ya muziki wa Tanzania. Na si hivyo tu, sasa anafungua ukurasa mwingine kupitia kolabo na Jay Moe.
JAY MOE AINGIA UWANJANI
Jay Moe ni mmoja wa wasanii waliokuwepo katika hatua mbalimbali za ukuaji wa Hip Hop Tanzania, akijenga jina lake kupitia kazi zake na kuendelea kuwa sehemu ya kizazi kilichosaidia muziki huo kupata nafasi kubwa nchini. Sasa anakutana na Mr. Cheeks, rapa mwenye historia kutoka Queens, New York.
Hapo ndipo kolabo hii inapopata ladha yake: upande mmoja kuna uzoefu wa Hip Hop ya Marekani, kuna historia ya Hip Hop Tanzania.
MASIKIO KWAO
Kinachosubiriwa sasa ni kazi yenyewe. Mashabiki wanataka kujua Jay Moe ataingiaje kwenye mtindo wa Mr. Cheeks na Mr. Cheeks naye atakavyokabiliana na ladha ya Hip Hop Tanzania.