Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nondo za makungwi wanne kwa Nandy

Muktasari:

Kila walipokuwa wakipiga hatua katika uhusiano wao ikiwamo walivyovishana pete kwa mara ya kwanza, wengi walisema ni kiki.

Kila walipokuwa wakipiga hatua katika uhusiano wao ikiwamo walivyovishana pete kwa mara ya kwanza, wengi walisema ni kiki.

Hata waliporudia tukio hilo na kutoleana mahari ilisemekana kiki pia. Lakini leo nyota huyo wa Bongofleva Christina Mfinanga, maarufu Nandy atafanyiwa singo maalumu kwa ajili ya kuandaliwa kuingia kwenye ndoa na mchumba wake Billnass hapo Julai 16.

Julai 16 wawili hao watatimiza maamuzi yao yatakayosuuza mioyo ya mashabiki wao waliokuwa wakihusudu mahusiano yao tangu walivyoamua kuyaweka hadharani.

Kikubwa kinachofanya watu kuwafuatilia ni kutokana na safari yao ya mahusiano ilivyokuwa, ikumbukwe kuwa Nandy alianza kuwa mahusiano na Billnass kabla ya marehemu Ruge Mutahaba aliyekuwa mzalishaji wa vipindi wa kampuni ya Clouds Media.

Hata hivyo mahusiano hayo yalikuwa siri ilikuja kubainika pale msiba ulipotokea kwa namna Nandy alivyopewa nafasi na familia ya kina Ruge.

Hata hivyo siku chache baada ya kufariki Ruge, Nandy akaoneka kwenye mahusiano na Bilnass ambapo pia miaka miwili iliyopita waliipua kibao chao kilichokwenda kwa jina la ‘Bugana’.

Kuanzia hapo mapenzi ya wawili hawa yaliendelea kubamba siku hadi siku na haikuwa siri tena, kwa kuwa wote ni wanamuziki wameendelea kufyatua vibao pamoja vikiwamo ‘Party’ na ‘Do Me’.

Hata hivyo wakati ndoa hiyo ikitarajiwa kufungwa Julai 16,wiki nzima mfululizo Nandy amekuwa akituma picha akionekana yupo na walimu maalumu (makungwi) ambao wanamfundisha mambo mbalimbali yatakayomsaidia anapokwenda kuanza maisha mapya, akiwamo muwigizaji wa siku nyingi, Bi Star, mtangazaji Mariam Migomba,mtangazaji Lilian Mwasha na mwimbaji wa siku nyingi wa nyimbo za taarabu Patricia Hillary.

Mwandishi wa makala hii amefanya mahojiano na kila mmoja kuhusu kazi hiyo aliyopewa ya kumuelimisha staa huyo aliyeibuka kwa mara ya kwanza na kibao cha ‘Nagusagusa’ na kufuatiwa na vingine kama ‘Wasikudanganye’,’One Day’, ‘Kivuruge’,’Ninogeshe’ na cha mwisho kukiachia siku za karibuni kilikuwa ni ‘Siwezi’.


Bi Star

Mama huyu ambaye ni matata katika uigizaji mbali ya kupata jina miaka ya nyuma kwa kuigiza kama mke wa Muhogo Mchungu kwenye maigizo ya kundi la Kaole na sasa ana miaka 34 katika fani hiyo. Lakini kwa sasa anatikisa vilivyo katika tamthilia ya Kombolela, akiigiza kama binti mtata wa familia ya mzee Kikala.

Bi Star ana miaka 52, akiwaandaa maharusi watarajiwa wa kike na wa kiume kwenda kuwa wanandoa bora kwa miaka 20 sasa.

Bi Star ambaye jina lake halisi ni Shamila Ndwangila, anasema kikubwa anachoona Nandy kumchagua yeye kuwa miongoni mwa makungwi au somo wake ni uzowefu katika kazi hiyo.

“Mimi mbali ya kuwa mwendesha shughuli (MC) ni mfundaji na pia namshukuru Nandy kwa kunichagua mimi,kwani ana bibi,shangazi zake ambao angeamua kuwatumia huenda mimi leo nisingeshiriki jambo hilo,”anasema Bi Star.

Bi star anadokeza kidogo mazungumzo yake na staa huyo kuwa ni pamoja na kumuhimiza kuwa mvumilivu katika ndoa,kwa kuwa ina raha na karaha zake.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwataka watu kuwaombea wanandoa hao kwani katika maisha mnaweza mkapendana lakini kukawa na husda za watu mkajikuta mnaachana bila kujua.

“Kwa faida ya wengine nawausia wanaotaka kuingia kwenye mahusiano ya ndoa kuhakikisha wanasomana tabia vilivyo, na wazazi wasiache kutimiza wajibu wa kuongea na watoto wao”anasema.


Mariam Migomba

Mtangazaji wa siku nyingi na mwigizaji,Mariam Migomba, anasema kuchaguliwa kwake na Nandy kunatokana na staa huyo kuhitaji mafunzo na si maneno.

Migomba mama wa watoto wawili, yumo ndani ya ndoa kwa miaka 31 sasa. Pia ni mzowefu wa kuzungumza masuala ya kijamii ikiwamo ya familia kupitia kipindi alichokuwa akitangaza cha ‘Mizani ya Ushambenga’.

Anasema kutokana na uzowefu wake katika ndoa na kufunda kwanza alimwambia msanii huyo anazungumza naye kama Faustina

na sio kama Nandy. Anasema alianza na tahadhari hiyo akijua kabisa katika ndoa hiyo wanakwenda kuishi mafahari wawili, kwa maana mastaa wanaofuatiliwa na wengi.

“Hivyo nimemwambia Nandy anapokuwa ndani na mumewe ahakikishe anaishi kama Faustina na kumuomba anifikishie ujumbe wangu kwa Billnass kuwa naye aishi kama Willium ili ndoa yao idumu badala ya kuleteana ustaa hadi ndani ya nyumba jambo ambalo linaweza kuwa sumu,”anasema Mariam.

“Pia nimemtaka Nandy kuwa msikivu kwa mumewe, jambo jema wanajuana kutokana na mahusiano yao kuanzia kwenye urafiki,kisha ndoa hivyo kunapotokea tofauti wakae chini wayazungumze na sio kukimbilia kila wakati kwa wazazi na mimi nipo tayari muda wowote wakinihitaji “anasema Mariam.

Pia mbali ya mengi niliyozungumza naye kama mwali wangu aliyeniamini ni pamoja na

“Katika hili wanaume wengi hawapendi kuonekana labda wameingia kituo cha kujaza mafuta katika gari,halafu mwanamke ndio anatoa hela,isipokuwa unapaswa kumpa mkononi aione ile hela ni yake na aitoe mwenyewe ndivyo walivyoumbwa hawa viumbe.

“Hapa nilijaribu kumuelewesha kama anahitaji kumsaidia mumewe kwa namna yoyote ile, iwe baina yao wawili, haijalishi ana uwezo kuliko mumewe”anasema Migomba.

Anasema hajapoteza kumfunda staa huyo, kwani imekuwa Baraka ya kupata kazi nyingi. “Tukubali,tukatae Nandy ni staa mkubwa,hivyo kuonekana tu kwenye ukarasa wake wa Instagram kama kungwi, mwalimu wake kumenifanya nijulikane,”anasema Migomba.


Lilian Mwasha

Mke halali wa MC Luvanda akiwa ndani ya ndoa yao kwa miaka 15 na ni mama wa watoto wanne ambaye pia ni mtumishi wa Mungu. Mwasha ni mtangazaji na anafanya kazi za kijamii na taasisi yake iitwayo Pink Tie Foundation inayomtetea mtoto wa kiume.

Mwanamama huyo mwenye shahada ya Mawasiliano ya umma, aliyoisoma nchini Afrika Kusini anaendesha kipindi cha Sunda Worship kwenye kituo cha matangazo cha Wasafi.

“Nashukuru Nandy ameniamini na nilizungumza naye kwa nafasi ya mtumishi wa Mungu na ndiyo jambo nililolifanya”anasema.

Anasema, “Kazi yangu haikuwa ngumu kwa sababu Billnass na Nandy licha ya kuwa wasanii wanamtumikia Yesu, hivyo tulizungumza lugha moja masuala ya kiroho yanayopaswa kufanyika ndani ya ndoa.

Anasema msisitizo mkubwa kwa wawili hao ulikuwa ni kumtanguliza Mungu katika kila kitu kwenye safari yao ya ndoa.

“Pia nimemuasa kuwa mvumilivu kukorofishana ndani ya ndoa ni vitu vya kawaida kwani hata mimi na miaka yangu 15 ndani ya ndoa sio kwamba hawakosoni na mumewe ni kuwekana sawa pale unapomuona mwenzako anakwenda ndivyo sivyo.

“Watu labda wasichojua ni bora kuacha kufanya harusi lakini sio kupeana talaka,nayasema yote haya kwa kuwa ni maisha ambayo nimeyapitia kwani nilishwahi kuachwa ndoa yangu ya kwanza ikiwa na miezi kumi tu,”anasema Mwasha.


Patricia Hillary

Nguli huyu wa taarabu anafanya Sanaa kwa miaka 42 sasa, alianza mwaka 1980. Lakini kufunda wali ameanza miaka mitano iliyopita.

Mkali huyo wa kibao “Njiwa”, alibarikiwa kupata watoto wawili, ingawa kwa sasa amebaki mmoja na amedumu katika ndoa kwa miaka 33. Mbali na ‘Njiwa’, Patricia ameimba pia nyimbo kali zinazopendwa mpaka sasa akitumia mafumbo katika tungo zake.

Baadhi ya nyimbo ni ‘Chura’, ‘Nahodha’, ‘Mapenzi Yananitatiza’, ‘Kuku na Yai’ na ‘Ni Mdodo’ wimbo unaochezwa sana kwenye hafla za harusi.

“Nandy anajua anakwenda wapi na anataka nini kwenye ndoa na ndiyo maana yeye akwa miongoni mwa aliowapa jukumu la kumsindikiza vema.

“Nilizungumza naye mengi lakini mtoto wangu huyu nilimsihi kuwa msikivu kwa mume wake.

“Usikivu kwa mume wangu ulinisaidia kuishi kwa amani katika miaka yangu 33 ya ndoa sikuwahi kupeleka mashtaka nyumbani kwetu mpaka mume wangu alipofariki mwaka 2013 “anasema Patricia.