Nape mgeni rasmi Tamasha la pasaka
Dar es Salaam. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka.
Tamasha hilo la bure linatarajiwa kufanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam Aprili 9, 2023.
Akizungumza leo Aprili 1 2023 na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotion ambaye ndio waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama amesema awali walikuwa wamemualika Rais Samia Suluhu Hassan lakini kutokana na kubanwa na majukumu Waziri Nape atamwakilisha siku hiyo.
"Naomba watu wajitokeze kwa wingi siku hiyo kwa kuwa Waziri wetu Nape atakuwa nasi katika tamasha hilo njooni kwa pamoja tumtukuze Mungu ," amesema Msama.
Akielezea kuhusu maandalizi ya tamasha yalipofika, Mkurugenzi huyo amesema yapo vizuri na wasanii wapo wanaendelea na mazoezi.
Kwa upande wake Mratibu wa tamasha hilo, Emmanuel Mabisa amesema wasanii wote ambao wanatangazwa kwenye tangazo lao watakuwepo siku hiyo na kuwataka watu wasikose .
Ukiacha wasanii wa hapa nchini wapo pia kutoka nchi ya Kongo, Rwanda, Kenya na Uganda.
"Pia hatujawasahau wasanii wa zamani wakiwemo wakina Jenifer Mgendi na wengine wengi kwa kuwa tunatambua mchango wao katika muziki wa injili, na kila tamasha kamwe hatujawahi kuwaacha nyuma" amesema Mabisa
Hata hivyo mratibu huyo amesema ukiacha kuwepo kwa vyakula na vinywaji pia siku hiyo kutakuwepo na michezo ya watoto hivyo utakuwa mtoko wa maana kwa familia.