Nandy: 911 yaja kufungua sura mpya
Muktasari:
- Kwa Nandy, miaka 10 siyo safari ya kawaida. Ni kipindi ambacho kimeshuhudia akitoka hatua za mwanzo za muziki hadi kujenga jina kama mmoja wa wasanii wa kike wenye nafasi kubwa kwenye Bongofleva.
BAADA ya miaka 10 ya safari ya muziki, Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy sasa anafungua ukurasa mwingine wa kazi yake kupitia albamu mpya inayokwenda kwa jina la 911, ikiwa inakuja baada ya tamasha la Nandy Festival lililobeba pia kumbukumbu katika muziki wake.
Kwa Nandy, miaka 10 siyo safari ya kawaida. Ni kipindi ambacho kimeshuhudia akitoka hatua za mwanzo za muziki hadi kujenga jina kama mmoja wa wasanii wa kike wenye nafasi kubwa kwenye Bongofleva.
Zaidi ya nyimbo, Nandy amekuwa akijenga vitu vinavyokwenda sambamba na muziki wake, ikiwemo Nandy Festival na The African Princess Label. Na sasa, baada ya hatua hizo macho yanaelekezwa kwenye 911, mradi wake unaokuja kufungua sura nyingine ya safari yake.
NANDY NA HISTORIA YA FESTIVAL
Mojawapo wa vitu vilivyomtofautisha Nandy katika safari yake ni Nandy Festival, tamasha aliloanzisha mwaka 2019 na ambalo limeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Tamasha hilo limekuwa sehemu ya utambulisho wa Nandy, huku likimpa nafasi ya kwenda zaidi ya kufanya show za kawaida na kujenga jukwaa linalobeba jina lake.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za vyombo vya habari, Nandy amekuwa akihusishwa na rekodi ya kuwa msanii wa kike nchini Tanzania aliyeanzisha na kuendesha tamasha lake kubwa linalobeba jina lake.
Pia amekuwa miongoni mwa wasanii wa kike wenye lebo ya muziki na kukuza vipaji vya wasanii wadogo, kwa sababu Nandy si msanii wa kwanza wa kike nchini Tanzania kumiliki lebo.
Wasanii kama Shilole, Vanessa Mdee na Shaa waliwahi kuwa na lebo zao kabla ya Nandy. Tofauti kubwa ni kwamba Nandy amejenga The African Princess Label ikiwa na msisitizo wa kuwapa nafasi wasanii wanawake.
TAMASHA LAKE
Nandy Festival imeendelea kukua kutoka tukio la burudani hadi kuwa sehemu ya brand ya Nandy.
Mwaka huu, tamasha hilo limepewa uzito zaidi kutokana na kuhusishwa na sherehe za miaka 10 ya safari yake ya muziki.
Katika matukio yake, Nandy amekuwa akiwapa nafasi wasanii wengine kupanda jukwaani, huku tamasha likiendelea kuwa sehemu ya kuwakutanisha mashabiki wake katika maeneo mbalimbali.
Nandy pia amewahi kueleza kuwa festival hiyo haimuhusu yeye pekee, bali inagusa pia fursa za vijana, wafanyabiashara na watu wengine wanaoshiriki katika shughuli zinazozunguka matukio hayo.
Na hivi karibuni, safari hiyo imefikia hatua nyingine jijini Dar es Salaam, ambako Nandy Festival 2026 imehitimisha sehemu ya sherehe kwenye muziki.
THE AFRICAN PRINCESS LABO
Mbali na tamasha, Nandy ameingia pia kwenye upande wa kujenga vipaji kupitia The African Princess Label.
Lebo hiyo ilizinduliwa rasmi Januari 2023 na msanii Yammi akiwa miongoni mwa wasanii wa mwanzo kutambulishwa chini yake.
Tofauti na lebo nyingine zilizowahi kuhusishwa na wasanii wa kike Tanzania, Nandy aliweka wazi msisitizo wake wa kuipa nafasi zaidi miziki na vipaji vya wanawake.
Lengo lake limekuwa kujenga jukwaa ambalo si la Tanzania pekee, bali lenye uwezo wa kuwafikia wasanii wanawake kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Hivyo, Nandy anapokuja na 911, anakuja akiwa tayari amejenga zaidi ya upande mmoja wa kazi yake.
Ana muziki, ana festival na ana lebo yake.
NANDY NA ZUCHU
Katika safari yake, jina la Nandy limekuwa likitajwa pamoja na Zuchu, hasa kutokana na nafasi ambazo wasanii hao wamejijengea kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Mashabiki wamekuwa wakiwalinganisha mara kwa mara, lakini Nandy mwenyewe amewahi kusema hana tatizo na hilo.
Pia amewahi kueleza kuwa Zuchu ni rafiki yake na mdogo wake katika muziki, hivyo ushindani unaojengwa na mashabiki si lazima uwe tafsiri ya uhusiano wao binafsi.
Kwa sasa, kinachobaki ni mashabiki kuendelea kusubiri kama siku moja sauti hizo mbili zitaungana kwenye kazi moja, ingawa hakuna tangazo rasmi la kolabo yao.
SASA 911
Mapema mwaka huu, Nandy ameweka wazi mpango wa kutoa albamu mbili mwaka 2026, baada ya kuchelewa kutimiza ahadi ya albamu aliyokuwa ameitangaza awali.
Aliwahi kusema albamu ya kwanza ingetoka baada ya Ramadhan na nyingine mwishoni mwa mwaka. Sasa jina limewekwa wazi 911. Hapo ndipo sura mpya inaanza.
Baada ya miaka 10 ya kujenga muziki, kuanzisha festival na kuingia kwenye biashara ya lebo, Nandy sasa anahitaji kazi yake mpya kubeba uzito wa safari yote aliyopitia.
911 inakuja ikiwa si albamu nyingine tu kwenye orodha ya kazi zake, bali ni mradi unaofuatia kipindi ambacho Nandy amekuwa akipanua jina lake kutoka kuwa msanii kwenda kuwa brand yenye matawi kadhaa.
Kuanzia jukwaani hadi festival, kutoka festival hadi lebo, sasa macho yapo kwenye muziki wenyewe.