Kisa ‘nikumbuke’ Nkone asusia gari aamuru liuzwe
Muktasari:
- Hayo yamejiri baada ya Upendo kutoa mtazamo wake kuhusu kumtumikia Mungu, uliopelekea baadhi ya watu kuutafsiri kama anakosoa wimbo wa Joel Lwaga 'Nikumbuke' aliomshirikisha msanii wa Bongo Fleva Diamondplatnumz
Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Upendo Nkone amesusia gari alilochangiwa na Watanzania na kutaka liuzwe kisha pesa wasaidiwe watoto yatima.
Hayo yamejiri baada ya Upendo kutoa mtazamo wake kuhusu kumtumikia Mungu, uliopelekea baadhi ya watu kuutafsiri kama anakosoa wimbo wa Joel Lwaga 'Nikumbuke' aliomshirikisha msanii wa Bongo Fleva Diamondplatnumz
Alichosema Nkone "Niko hapa kuwakumbusha kwamba Mungu hadhihakiwi, ataniwi, achezewi. Unachopanda ndicho utachovuna tusimame upande wa Mungu tusichanganye mambo.
“Unaweza ukafanya vitu ya kumuudhi Mungu na ukaona upo salama kwa sababu hafanyi chochote kukuadhibu lakini ipo siku ukiendelea na mambo hayo kitakuramba. Tusimame na Mungu tuache kuchanganya mambo,"alichosema Nkone awali.
Kauli hiyo ikapelekea mashabiki wamjie juu mwanamuziki huyo na kuibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii huku kati ya watu waliokosoa vikali ni dada wa Diamond, Esma.
Mbali naye msanii Shilole wakati akifanya mahojiano na kituo cha redio alisema kama Nkone analeta ubaguzi wa kidini arudishe gari alilochangiwa na Watanzania "Arudishe gari letu" na baadhi ya komenti zikigusia suala hilo.
Utakumbuka Upendo Nkone alichangiwa gari na mashabiki mbalimbali kutoka mitandaoni baada ya mfanyabiashara Resty Bura kuanzisha arambee hiyo ya Nkone apate gari. Ambapo mapema mwaka huu michango ilitimia na kununuliwa gari
Baada ya maoni ya wengi Nkone ametoa ufafanuzi kuhusu ujumbe wake wa awali akisema.
"Watu wa mungu,bwana yesu asifiwe natumaini Mungu amewatunza mko salama. Nilitoa ushauri wa kiroho kwa watumishi wote wa Mungu na sikumtaja jina mtu yeyotee. Ila naona nimetajwa duniani kote sijui hapo sheria inasemaje kwa walionitaja jina hata sielewii ila nawashukuru mno kwa upendo wenu mkubwa kwangu.
"Narudia tena kuwashukuru kwa kunichangia gari la injili sasa nawaombeni mniitie dada Resty Bura ili tupate mteja chapu tuuze gari yetu (ndinga) halafu pesa yote tuipeleke kwa yatima tuitoe huko,halafu nibakie na Yesu wangu nianze upya, nipige zangu injili ya Yesu Kristo kwa amani halafu nimngoje bwana atanipa tena au mnasemaje watu wa Mungu?