Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwigizaji Hashim Kambi afariki dunia

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Rajabu Amir, Kambi alianza kujisikia vibaya ghafla akiwa katika eneo la kazi zake za kisanii (location), kabla ya kuwahishwa hospitali kwa matibabu. Hata hivyo, jitihada za madaktari hazikuweza kuokoa maisha yake na ndipo umauti ulipomkuta.

KIFO hakipigi hodi! Ndivyo ilivyotokea kwa nguli wa filamu nchini, Hashim Kambi ambaye alianza kujisikia vibaya akiwa anatekeleza majukumu yake ya uigizaji, akakimbizwa katika Hospitali ya Mico iliyopo Sinza Makaburini jijini Dar es Salaam ambako umauti umempata.

Taarifa kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Rajab Amiry, amesema alipokea simu kutoka kwa Mzee Chillo kumuelezea kufariki kwa Kambi.

"Amefariki dunia leo Aprili 27, 2026 katika Hospitali ya MICO iliyopo Sinza, wakati madaktari wakiwa katika mapambano ya kuokoa maisha yake, lakini kitu kikipangwa na Mwenyenzi Mungu hakizuiliki," amesema na kuongeza;

"Walikuwa wanafanya kazi ya kuingiza sauti (Dubbing) katika ofisi za Kampuni ya Pilipili Entertainment, hivyo angekuwa anaumwa toka kwake asingefika hadi kazini."

Nguli huyo enzi za uhai wake, ameigiza filamu kama Simu ya Kifo, Kipusa, The Lost Twins, Kipuri, Zuadiswa, Honey Moon, Surprise, Ripple of Tears, Miss Call, Romance, 20%, Furaha Iko Wapi, The Passion na Damu ya Mjomba.

Rais wa zamani wa TAFF, Eliya Mjatta, amesema: "Kambi atakumbukwa kwa uhodari wake wa kazi na kuibua vipaji vya watu wengine zaidi, mchango wake utaendelea kuishi."

Mbali na kuigiza, Kambi alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu nchini, ambapo alichezea Yanga SC.

Kutokana na mapenzi yake kwa Yanga, wakati wa uhai wake, aliwahi kumsifia aliyekuwa straika wa timu hiyo, Fiston Mayele kuwa miongoni mwa wachezaji waliyokuwa wanatikisa pia alikuwa anapendelea kwenda uwanjani kushuhudia mechi mbalimbali za ligi akiwa amevalia jezi ya kijani na njano.

Mbali na Mayele, Kambi aliwahi kusema mchezaji ambaye anacheza kama alivyokuwa yeye ni beki wa kati ya Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca' ingawa kipindi cha nyuma alikuwa anajiona katika miguu ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro'.