Mwaka unakwisha, Stars haina msingi
Muktasari:
Hata hivyo ukimuuliza mwenyekiti wa kamati ya ufundi, mdogo wangu Wilfred Kidau kwamba baada ya kuwa wamemaliza mwaka mmoja ndani ya hizo ofisi zetu tukufu anaweza kutuambia wapi Taifa Stars inaweza kuwa imejenga msingi wake wa kuwapata wachezaji.
IMEBAKI miaka mitatu uongozi wa raisi wetu wa awamu ya pili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umalize muda wake.
Hata hivyo ukimuuliza mwenyekiti wa kamati ya ufundi, mdogo wangu Wilfred Kidau kwamba baada ya kuwa wamemaliza mwaka mmoja ndani ya hizo ofisi zetu tukufu anaweza kutuambia wapi Taifa Stars inaweza kuwa imejenga msingi wake wa kuwapata wachezaji.
Na vipi kwa mwenyekiti wa kamati ya soka la vijana kaka yangu Ayoub Nyenzi kama kweli misingi ya wachezaji alionao wapo katika umri sahihi wa kuijenga Stars yakweli ya baadaye?
Bila shaka watakuwa na majibu mazuri lakini bado watakuja kwa muuliza maswali au mwandishi wa makala hii na watajazwa maneno tu kwamba Kana katumwa. Mbona hana leseni za ukocha zinazoweza kumfanya aulize maswali haya.
Haya ndiyo matatizo yetu Watanzania, badala ya kushughulikia tatizo tunahangaika na anayeliona na kulitoa hadharani ingawa ni wazi tunatakiwa tupate ufumbuzi wa tatizo hili kwa faida ya soka letu baadaye.
Kinachofanya tushindwe kupanga mipango mizuri ya maendeleo ya soka si uwezo mdogo wa wachaguliwa wetu kuanzia Raisi wa TFF, bali ni muda mdogo waliotengenezewa kwenye katiba ya TFF.
Katika soka miaka minne ni michache lakini kwa kufikirika watu wanaweza kuiona mingi sana, hapa ndipo tunapoanza kupoteza mipango yetu ya muda mrefu.
Lakini ningekuwa mimi ndiye Kidau au Nyenzi nisingeiona miaka hii kwa kuifikiria uchache wake kwani umri walionao wenyeviti hawa bado unawawezesha kufanya makubwa kwa leo na baadaye.
Katika hali hiyo ningetengeneza programu ndefu za mafanikio kwa miaka mingi tu ijayo hata kama mafanikio hayo yataonekana baada ya kuondoka kwao madarakani lakini yeyote mwenye macho ataona na hivyo kuwafanya viongozi hawa wa leo kukumbukwa baadaye na hata watakapokuwa wanataka kurudi tena wadau hawatakuwa na kinyongo nao.
Mwaka ndio umekwisha, ile mikakati mikubwa iliyokuwa imewekwa na TFF ili kuijenga Taifa Stars yetu ya leo na baadaye imeshindwa kufanya kazi, si dhambi kwa kitu fulani kushindwa kufanya kazi, hata watafiti wanasayansi na wasomi huwa wanajaribu kitu kikishindwa wanakiacha na kujaribu kingine.
Kulikuwa na suala zima la kuiboresha timu yetu ya taifa na nadhani hatukutakiwi kusema ‘Maboresho’ bali tulitakiwa tuyaite haya tuliyoyajaribu ‘Mageuzi’.
Ni mageuzi kwa sababu ni hali ya kutoka kuchagua wachezaji wanaotakiwa kuunda timu ya taifa kwa kuwaangalia nyota wanaocheza vizuri Ligi Kuu au Ligi Daraja la Kwanza hadi kumchagua mchezaji asiyecheza pengine ligi yoyote ya maana au wale wanaocheza ligi ndogo wasiojulikana na kufanikiwa kuvaa uzi wa timu ya taifa si mchezo, yangekuwa mageuzi ya kweli ambayo hayajawahi kutokea.
Suala hili la kuiboresha Stars ni zuri kimtazamo lakini hatutakiwi kuboresha timu ya taifa, tunachotakiwa ni kuboresha mbinu zetu za kuwachagua wachezaji wanaotakiwa kujiunga na timu yetu ya taifa.
Kaka yangu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi msianzie huko juu sana hata hawa mliowateua juzi juzi mkawapeleka kambini bado mpo eneo la juu sana, hawa bado hawana tofauti sana na kaka zao, shukeni kidogo chini walipo vijana wa kati angalau mngeanza na wale vijana wanaoshiriki mara kwa mara Kombe la Uhai ambao wanatakiwa wawe na miaka isiyozidi 20 hata ikiwa 23 siyo mbaya.
Nendeni tena mkasaidie kuyaboresha mashindano ya Umisseta yaliyo chini ya TAMISEMI, watume makocha wako kaka, wapo kina Marsh, Mayanga, yupo Jamhuri, Minziro, Mwambusi na wengine vijana wafanye kazi ya kufuatilia mashindano yao toka ngazi ya kanda.
Huko watapata vijana sahihi wa kuijenga Stars ya kesho, huko angalau kuna misingi bora ya kujenga soka letu la baadaye, ndani ya miaka miwili watakuwa wameanza kutukomboa.