Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mule mule FBI: Kutoka kuimba na JB Mpiana hadi kufananishwa na Koffi Olomide

DAKIKA 5 Pict

Muktasari:

  • Miongoni mwao ni Mule Mule FBI, mwanamuziki ambaye amekuwa kwenye muziki wa dansi kwa miaka kadhaa, akipita katika mazingira tofauti ya muziki na kujijengea jina kupitia uimbaji, uchezaji na uwezo wake wa kuliteka jukwaa.

Muziki wa dansi una historia ndefu ya wanamuziki waliopita katika bendi mbalimbali, wakakutana na mastaa wakubwa na kuacha kumbukumbu ambazo huendelea kusimuliwa na mashabiki.

Miongoni mwao ni Mule Mule FBI, mwanamuziki ambaye amekuwa kwenye muziki wa dansi kwa miaka kadhaa, akipita katika mazingira tofauti ya muziki na kujijengea jina kupitia uimbaji, uchezaji na uwezo wake wa kuliteka jukwaa.

Mulemule amewahi kuwa sehemu ya FM Wana Ngwasuma na FM Academia, baadaye akahusishwa na The Bambazi, kabla ya kuendelea na safari yake katika Bogoss Musica chini ya Nyoshi El Saadat.

Lakini katika safari yake hiyo kuna matukio ambayo yanaweza kumfanya msomaji amwangalie kwa jicho tofauti.

Miongoni mwa matukio hayo ni safari yake ya Dubai, ambako alipata nafasi ya kupanda jukwaani na mwanamuziki mkubwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, JB Mpiana.

Wakati huo huo, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimfananisha Mulemule kwa sura na namna anavyocheza akiwa stejini na gwiji wa muziki wa Congo, Koffi Olomide.

Mwanaspoti limezungumza na Mulemule kuhusu safari yake, muziki, JB Mpiana, Koffi Olomide na maisha yake ya sasa ndani ya Bogoss Musica.


DAKI 01

MWANASPOTI: Mulemule, jina lako limekuwepo kwa muda katika muziki wa dansi. Safari yako ilianza vipi?

MULE MULE FBI: Safari yangu ni ndefu. Nimepita kwenye mazingira tofauti ya muziki na nimefanya kazi na wanamuziki mbalimbali. Kila sehemu niliyopita imenipa uzoefu na kunifundisha kitu ambacho hadi leo ninakitumia. Nilipita FM Wana Ngwasuma, baadaye nikawa sehemu ya FM Academia na safari ikaendelea katika hatua nyingine.


MWANASPOTI: FM Academia imekuwa na nafasi gani katika safari yako?

MULE MULE FBI: FM Academia ni sehemu muhimu sana ya historia yangu. Nilipata nafasi ya kujifunza mambo mengi kuhusu muziki wa dansi, uimbaji na namna ya kuishi na mashabiki.

Muziki wa dansi hauishii kwenye kuimba tu. Kuna jukwaa, kuna watu unaofanya nao kazi na kuna mashabiki ambao ndiyo wanaokupa nguvu ya kuendelea.


MWANASPOTI: Baadaye ukaondoka CP Academia. Nini kilisababisha uondoke?

MULE MULE FBI: Kila mwanamuziki ana wakati ambao anaona anahitaji kubadilisha mazingira. Mimi niliona ni wakati wa kwenda kufanya kitu kingine na kujaribu hatua nyingine katika muziki. Baada ya hapo nikawa sehemu ya mipango ya The Bambazi, ambayo nayo ilikuwa hatua muhimu katika safari yangu.


MWANASPOTI: Ulishawahi pia kuongoza bendi yako?

MULE MULE FBI: Ndiyo. The Bambazi ilikuwa moja ya hatua ambazo zilinipa nafasi ya kuuona muziki kwa upande mwingine. Sikuwa tu mwimbaji au mwanamuziki wa jukwaani, bali nilipata pia uzoefu wa upande wa uongozi na mipango ya bendi.


DAKI 05

MWANASPOTI: Kuna tukio moja linatajwa sana kwenye historia yako, la Dubai. Ni kweli uliwahi kuimba na JB Mpiana?

MULE MULE FBI: Ndiyo. Hilo ni moja ya matukio ambayo sitayasahau katika safari yangu ya muziki. Nilikuwa Dubai kwa shughuli za muziki, ndipo JB Mpiana alipofika katika eneo ambalo tulikuwa tukitumbuiza. Baadaye akapanda jukwaani na tukapata nafasi ya kuimba pamoja. Kwa mwanamuziki, kukutana na mtu mkubwa kama JB Mpiana na kupata nafasi ya kuwa naye jukwaani ni jambo kubwa.

DAKI 04
DAKI 04

MWANASPOTI: Mliimba wimbo gani?

MULE MULE FBI: Tulipata nafasi ya kuimba pamoja wimbo wa JB Mpiana, “48 Hrs Gecoco.” Ilikuwa ‘experience’ kubwa kwangu kwa sababu unakutana na mwanamuziki mkubwa ambaye unamheshimu, halafu ghafla unajikuta mko pamoja kwenye jukwaa.


MWANASPOTI: Tukio hilo lilikufundisha nini?

MULE MULE FBI:  Kila unapokutana na mwanamuziki mkubwa unapata kitu. Unaangalia namna anavyotawala jukwaa, anavyowasiliana na mashabiki na namna anavyofanya kazi. Kwangu lilikuwa ni tukio la kujifunza na pia kuniongezea kujiamini.


MWANASPOTI: Sasa kuna jambo jingine linalozungumzwa na mashabiki. Baadhi yao wanakufananisha kwa sura na Koffi Olomide. Umeshawahi kusikia hilo?

MULE MULE FBI: Ndiyo, nimewahi kusikia watu wakisema hivyo. Mimi nalichukulia kama maoni ya mashabiki. Koffi Olomide ni mwanamuziki mkubwa sana na nina heshima kwake. Kama mtu anaona kuna sehemu fulani kwenye sura yangu inayomkumbusha Koffi, hiyo ni namna alivyoniona.


MWANASPOTI: Wengine wanasema si sura tu, hata uchezaji wako ukiwa stejini unawakumbusha Koffi. Unasemaje?

MULE MULE FBI: Mimi napenda sana jukwaa. Napenda kuwasiliana na mashabiki na ninapokuwa mbele yao lazima niwape burudani. Kila mwanamuziki ana namna yake ya kucheza na kuwasiliana na watu. Kama mashabiki wanaona uchezaji wangu unawapa kumbukumbu ya Koffi, hilo ni jambo ambalo wameliona wao. Mimi ninaendelea na style yangu.

DAKI 03

MWANASPOTI: Je, wewe mwenyewe unampenda Koffi Olomide?

MULE MULE FBI: Koffi ni mkubwa. Ni mwanamuziki ambaye amefanya mambo makubwa kwenye muziki wa Congo na Afrika kwa jumla. Kama mwanamuziki, unawaheshimu watu waliotengeneza historia kwenye muziki.


MWANASPOTI: Kwa sasa uko Bogoss Musica. Umefikaje hapo?

MULE MULE FBI: Kwa sasa niko Bogoss Musica chini ya Nyoshi El Saadat. Ni hatua nyingine katika safari yangu ya muziki. Nimeingia hapa nikiwa na uzoefu wangu wa miaka mingi, lakini bado ninaamini mwanamuziki anatakiwa kujifunza kila siku.


MWANASPOTI: Kufanya kazi na Nyoshi El Saadat kuna tofauti gani kwako?

MULE MULE FBI: Kila bendi ina mfumo wake na changamoto zake. Kitu muhimu ni kufanya kazi kwa bidii na kuwapa mashabiki kile wanachokitarajia. Mimi nimekuja kufanya muziki, kuimba na kuhakikisha mashabiki wanapata burudani nzuri.

DAKI 02

MWANASPOTI: Ukiangalia safari yako yote, ni kitu gani unajivunia zaidi?

MULE MULE FBI: Najivunia nimeendelea na muziki ninaoupenda licha ya kupitia vipindi tofauti. Nimepita kwenye bendi mbalimbali, nimefanya kazi na watu tofauti na nimepata nafasi ya kukutana na wanamuziki wakubwa. Kukutana na JB Mpiana Dubai ni moja ya kumbukumbu kubwa, pia kila bendi niliyopita imenipa historia yake.


MWANASPOTI: Kuna wakati uliwahi kufikiria kuacha muziki?

MULE MULE FBI:  Muziki ni maisha yangu. Kuna changamoto, lakini changamoto hazimaanishi unatakiwa kuacha. Nimepita kwenye mambo mbalimbali, lakini nimeendelea kwa sababu napenda muziki na napenda jukwaa.


MWANASPOTI: Mashabiki waliokufuatilia tangu FM Academia hadi sasa unawaambia nini?

MULE MULE FBI: Nawashukuru sana. Bila mashabiki mwanamuziki hawezi kwenda mbali. Wale walionifahamu tangu FM Academia, The Bambazi na wale wanaoniona sasa Bogoss Musica, nawashukuru kwa sapoti yao. Waendelee kutupa nguvu.


DAKI 06

MWANASPOTI: Kwa sentensi moja tu, Mule Mule FBI ni nani?

MULE MULE FBI:  Mule Mule FBI ni mwanamuziki ambaye bado ana safari ndefu ya kuwapa mashabiki burudani.


MWANASPOTI: Asante sana kwa mazungumzo.

MULE MULE FBI:  Asanteni Mwanaspoti.