Mshindi BSS kuondoka na kiwanja, Startimes kurusha mubashara
BARAZA la Sanaa Taifa (BASATA) limesifu juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi wa shindano la Bongo Star Search (BSS), Rita Paulsen kwa kuzalisha vipaji vya vijana wengi nchini kupitia sanaa ya muziki.
Ofisa Mwandamizi wa BASATA, Agustino Makame amesema hayo leo Januari 16 wakati wa kutangazwa fainali za BSS ambapo alieleza baraza hilo linatambua mchango mkubwa unaofanywa katika kufufua, kukuza na kuwapa nafasi ya kutumia jukwaa hilo kutimiza ndoto za vijana wengi.
Mkurugenzi wa Masoko kutoka Startimes, David Malisa amesema msimu huo wa 14 ulikuwa wa kitofauti kutokana na timu hiyo kufika mji wa Kigoma ambapo aliwahi kupatikana supastaa Peter Msechu.
Pia amesema Startimes wataendelea kuunga mkono jitihada za mama huyo kwakuwa jukwaa la BSS linawafikia vijana walio mikoani kwa lengo la kutimiza ndoto zao kupitia muziki.
"Fainali hizo zitarushwa mubashara kupitia St Swahili bila chenga ili kuwapa fursa ya kuwaona burudani mbalimbali usiku wa kilele cha fainali hizo," amesema Malisa
Naye Jaji mkuu wa shindano hilo, Madam Rita ameelezea utofauti wa msimu wa 14 wa shindano hilo umekuwa na vipaji vingi na vizuri tofauti na misimu iliyopita na sasa kutakuwa ba sita bora na siyo tano bora kama zamani.
"Msimu wa 14 vijana wamejitokeza wengi na mikoa mengine ilitulazimu tuchukue watu wengi na baadae tulipofanya mchujo tumebaki na washiriki sita ambao wameingia kwenye mchakato wa kupata mshindi."
Madam Ritha ameweka wazi zawadi ya mshindi wa kwanza ni kiwanja pamoja na fedha Sh20 milioni, wakati mshindi wa pili atapewa Sh3 milioni huku washindi waliobakia wakipatiwa kifuta jasho Sh1 milioni kila mmoja.
"Kiukweli tunahitaji nguvu kubwa mno katika shindano hili bado tunahitaji wadau tunaomba wizara husika watupe nguvu na waombe udhamini kwa Taasisi na Wizara mfano Wizara ya Utalii inakuwa rahisi wenyewe kwa wenyewe wizara za serikali kusikilizana kwa haraka na kupatikana majibu kwa wepesi zaidi,"