Mpango wa Zuchu 2026 una maana gani?
Muktasari:
- Zuchu, mshindi wa tuzo za AFRIMMA 2020 & 2022, amesema albamu hiyo itajumuisha nyimbo za Bongofleva pekee ikiwa ni mara ya kwanza kufanya jambo kama hilo tangu atoke kimuziki miaka mitano iliyopita.
MWANAMUZIKI kutoka WCB Wasafi, Zuchu anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanamuziki watakaotoa albamu mwaka huu wa 2026, lakini akiwa amepanga kuja tofauti kidogo akiwa na maana yake nyuma ya pazia.
Zuchu, mshindi wa tuzo za AFRIMMA 2020 & 2022, amesema albamu hiyo itajumuisha nyimbo za Bongofleva pekee ikiwa ni mara ya kwanza kufanya jambo kama hilo tangu atoke kimuziki miaka mitano iliyopita.
Hii itakuwa ni albamu ya pili kwake baada ya hapo awali kuachia Peace and Money (2024) yenye nyimbo 13 na kuwashirikisha wasanii saba akiwemo bosi na mumewe, Diamond Platnumz.
Peace and Money Album (2024) ilishirikisha wasanii kadhaa wa kimataifa akiwemo mkali wa Afrobeats, Yemi Alade kutokea Nigeria ambaye kipaji chake kiliibuliwa na shindano la uimbaji la Peak Talent Show 2009.
Hata hivyo, awali Zuchu alishatoa Extended Playlist (EP) iliyomtambulisha, I Am Zuchu (2020) yenye nyimbo saba huku akiwashirikisha wasanii wawili Khadija Kopa na Mbosso, mwanzilishi wa Khan Music.
Utakumbuka baadhi ya wasanii wa Bongofleva waliotoa albamu mwaka uliopita, ni Darassa (Take Away The Pain), Jay Melody (Addiction), Lady Jaydee (Silver), Moni Centrozone (Watoto wa Mtaani) na kadhalika.
Kwa upande wa EP kulikuwa na Nedy Music (The Voice of The Island), Lava Lava (Time), Yammi (After All), Phina (Melanin Therapy), Jux (A Day To Remember), Mbosso (Room Number 3) na kadhalika.
Je, ina maana gani kwa Zuchu kuja na albamu ya Bongofleva pekee? Kwanza lengo ni kuhakikisha anaendelea kulishikilia soko lake ndani pengine ameona mashabiki wake wa nyumbani kuna kitu wamekosa.
Nyimbo zake tatu za mwisho kuachia Amanda (2025), Inama (2025) na Reason (2025), mbili kati ya hizo ameimba kwa lugha ya Kiingereza kwa asilimia kubwa ikiwa na maana alilenga soka la nje.
Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, alitangaza mpango kama huo mwaka uliopita lakini hakuutekeleza licha ya kuwa ana miaka mingi tangu alipotoa albamu yake ya mwisho, A Boy From Tandale (2018).
Hata hivyo, mpango huo kwa Zuchu unatoa picha jinsi muziki wake umegawanyika katika makundi matatu tofauti ambapo kila kundi linakuwa limekusudia kulenga aina fulani ya mashabiki.
Mosi; ukimsikia Zuchu katika nyimbo za Singeli kama Nyumba Ndogo (2021), Hujanizidi (2024) akiwa na D Voice, au Afande (2025) akiwa na Dogo Paten tambua hapo anawalenga mashabiki wake wa uswahilini.
Pili; nyimbo kama Nobody (2020) akiwa na Joeboy (Nigeria), Nani Remix (2023) akiwa na Innoss’B (DR Congo), na Lollipop (2024) akiwa na Yemi Alade (Nigeria), hizo kwa Zuchu zinalenga soka la kimataifa.
Tatu; akija nyimbo kama Wana (2020), Litawachoma (2020), Sukari (2021), Kwikwi (2022), Mwambieni (2022) na Utaniua (2023), hapo ni kwa mashabiki wote wa Bongo na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Sasa Zuchu anaposema anakuja na albamu ya Bongofleva, maana yake anamaanisha kundi la tatu kwa sehemu kubwa na kundi la pili kwa uchache, huku kundi la pili akiliacha kabisa.
Ndivyo ilivyo hata kwa Diamond, naye ana mgawanyiko wa makundi matatu katika kuachia nyimbo zake, kuna nyimbo zinazolenga soko la Tanzania (Bongofleva), Afrika na Dunia (kimataifa zaidi).
Diamond akitoa nyimbo na Ne-Yo (Marry You), Morgan Heritage (Hallelujah), Omario (African Beauty) Rick Ross (Waka) au Ciara (Low), hapo analenga zaidi soko la kimataifa.
Akiwashirikisha kina Tiwa Savage (Fire), Koffi Olomide (Waah!), Focalistic (IYO), P-Square (Kidogo), Teni (Sound), Mr. Flavour (Nana), Fally Ipupa (Inama), Rema (Gimmie), ujue analenga soka la Afrika.
Ila ukimsikia Diamond anaimba nyimbo kama Msumari, Nani, Zuwena, Mapoz, Sikomi, Yatapita, Baba Lao, Haunisumbui, Chitaki, Naazaje au Kanyaga basi ujue hapo analenga soko la hapa Bongo.
Hata hivyo, utaratibu kama huu unaonekana kama mzigo au mpango unaoweza kuwachelewesha kina Zuchu na ndipo washindani wao kwa hapa Afrika kama kina Tyla na Ayra Starr wanawapiga bao.
Mathalani Ayra Starr anapoachia nyimbo kama Rush (2022), Commas (2024), Hot Body (2025) na Who’s Dat Girl (2025), hizo ni kwa ajili ya mashabiki wa nyumbani kwao Nigeria, Afrika na duniani kote.
Hana nyimbo kwa ajili ya watu wa Nigeria na sijui wapi kwingine, ngoma yake moja inatosha maeneo yote, na pengine ndio sababu wao wafanikiwa zaidi kwa sababu kila kazi wanayotoa tayari ina viwango vya kimataifa.
Na kwa upande mwingine, huenda Zuchu anakuja na albamu mwaka huu ili kuendana sawa na mshindani wake wa karibu, Nandy, ambaye naye huenda albamu yake ikatoka baada ya kuahirishwa.
Albamu hiyo ambayo ni ya pili kwa Nandy, ilipangwa kuachiwa Novemba 2025 lakini haikuwa hivyo licha ya The African Princess huyo kueleza kuwa maandalizi yake yamekamilika kwa asilimia kubwa. Ikumbukwe kwa miaka sasa Zuchu na Nandy amekuwa wakiwekwa katika ushindani hasa na mashabiki kutokana wote wanafanya vizuri lakini kiundani zaidi kila mmoja ana vitu vingi alivyomzidi mwenzake.