MAUA SAMA: Miaka kumi na mbili ya kibabe zaidi
Muktasari:
Kwa sanaa ya muziki, wapo wasanii wa kike wamepambana kudumu kwa muda mrefu wakionyesha uwezo mkubwa. Mfano mzuri ni Lady Jaydee, ambaye kwa zaidi ya miaka 25 tangu alipoachia albamu yake ya kwanza ya Machozi mwaka 2000, hadi sasa yupo katika gemu la Bongo Fleva.
KATIKA sekta mbalimbali kumekuwa na mijadala kuhusu nguvu ya wanawake, sanaa, siasa, uongozi na hata mambo ya kiuchumi.
Kwa sanaa ya muziki, wapo wasanii wa kike wamepambana kudumu kwa muda mrefu wakionyesha uwezo mkubwa. Mfano mzuri ni Lady Jaydee, ambaye kwa zaidi ya miaka 25 tangu alipoachia albamu yake ya kwanza ya Machozi mwaka 2000, hadi sasa yupo katika gemu la Bongo Fleva.
Ukiachana na Jide a.k.a Commando, ambaye anatajwa kama mmoja wa wasanii waliopambania kipaji chake licha ya ugumu wa tasnia hiyo, kuna mwanadada anayeitwa Maua Sama, miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika tasnia hiyo nchini na kimataifa.
Mwimbaji huyo mwenye sauti ya kipekee alianza rasmi kazi miaka 12 iliyopita na hadi leo bado jina lake linatajwa kama miongoni mwa waimbaji bora wa kike nchini.
Maua Sama alipojitokeza kwa mara ya kwanza, alitazamwa kama nyota mpya atakayekuja kurithi nafasi za wakongwe kama Jide, Ray C, Stara Thomas na wengineo.
Uimbaji wake uliojaa hisia, mashairi ya mapenzi na uwezo wa kupanda jukwaani bila kuhitaji playback vilimfanya kuwa tofauti na wengi wa kizazi chake.
Wimbo kama Mahaba Niue ulianza kumtambulisha, lakini Iokote alioshirikiana na Hanstone mwaka 2018 ulimpa nafasi kubwa ya kuvuma kitaifa na kimataifa, ukimfanya atambulike kama nyota mpya wa muziki wa Bongo Fleva.
Ni ukweli usiopingika kwamba ana sauti na kipaji halisi, lakini bado hajafika kwenye kilele kikubwa cha mafanikio ya muziki wake kimataifa kama ambavyo mashabiki na wadau walitarajia.
Kama huamini hilo, nenda YouTube tafuta wimbo Zamani utajua namaanisha nini — yaani ukitaka aimbe ngoma za mbele, yuko vizuri, Bongo Fleva ndio usiseme.
Wadau wanajiuliza kwa nini Maua Sama hajafikia huko ilhali ana kila kitu ambacho mwimbaji au wasanii wa nje wanavyo au hata kuwazidi?
Mwanaspoti inakuchambulia miaka 12 ya msanii huyo, mafanikio na wapi anakwama kwenda kimataifa zaidi, kwani nchini ashaonyesha ukubwa wake.
ALIPOANZA
Maua Sama alianza kazi yake ya muziki mwaka 2013 baada ya kugunduliwa kipaji chake na msanii wa muziki wa hip hop na Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Mwana FA.
Walishirikiana kwenye wimbo So Crazy mwaka huohuo. Wimbo wa So Crazy ulirekodiwa kwa mara ya kwanza na Maua Sama, ukatayarishwa na kushirikisha wasanii wa nyumbani kwao Moshi, Kilimanjaro, na baadaye ukarekodiwa upya na kumshirikisha Mwana FA.
Mwaka 2015, alitoa wimbo wake wa kwanza rasmi, Let Me Know, ambao ulimtambulisha kwa hadhira kubwa zaidi ya Kitanzania. Akaendelea kutoa ngoma ya Mahaba Niue, ambapo alionyesha tofauti yake kwa miondoko ya taratibu, sauti tamu na midundo yenye mchanganyiko wa Bongo Fleva na R&B.
Katika kipindi ambacho wasanii wa kike walikuwa wachache, akapata nafasi ya kupanda kwenye majukwaa kama Fiesta.
ZILIZOTAMBA
Wimbo Iokote aliomshirikisha Hanstone mwaka 2018 ndio wimbo uliompa nafasi ya juu zaidi, ukawa gumzo nchini na kuvuka mipaka. Hadi leo hii, ni miongoni mwa vibao vilivyoweka alama kubwa kwa upande wa Maua Sama.
Ameendelea kutoa nyimbo zinazofanya vizuri kama Nionyeshe, Zai, Nitampata Wapi ft Jay Melody, Poa, I Don’t Care na nyinginezo.
KADUMU LAKINI!
Katika kipindi ambacho wasanii wengi wa kike hukata tamaa au huingia na kutoka, Maua amedumu kwa zaidi ya muongo mmoja, jambo linaloonyesha uvu-milivu na mafanikio.
Wasanii kama Vanessa Mdee (miongoni mwa vipaji vya levo nyingine), Recho Kizunguzungu, Malaika na wengineo walifanya makubwa lakini hawakuwa na muendelezo, wakaishia njiani.
Ni sauti inayoweza kulinganishwa na viwango vya kimataifa, hasa upande wa Afro-soul na R&B, lakini changamoto inaonekana kwenye uongozi. Kukosekana kwa menejimenti kunamfanya ashindwe kufanikisha mikakati mikubwa ya kimataifa licha ya kipaji chake.
USHINDANI
Muziki wa Bongo Fleva kwa muda mrefu umekuwa na changamoto kwa upande wa wanawake. Miaka 10 iliyopita, wasanii wengi walikuwa wanaume, wanawake walikuwa wanahesabika ukimtoa Jaydee utamkuta Ray C.
Lakini hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wasanii wa kike ambao wanafanya vizuri. Abigail Chams, siku chache zilizopita, alitajwa kuwania tuzo za BET katika kipengele cha Best New International Act.
Kizazi kipya cha wasanii kama Zuchu, Nandy na wengine kimekuja na nguvu kubwa, wakichukua nafasi za juu na kuwapiku wasanii wengine.
Tangu kuonekana ushindani wa wasanii wa kike, ni kama Sama amebweteka. Anaweza kutoa ngoma inayofanya vizuri kwa mwaka kisha kukaa kimya — jambo ambalo linamrudisha nyuma kwenye muziki wake wakati ambao mashabiki wanategemea kumuona mbali zaidi.
CHANGAMOTO
Muziki wa sasa umebadilika; si tena kuwa na sauti pekee, bali una mambo mengi ya kuufanya kibiashara zaidi. Wasanii kama Ayra Starr wa Nigeria ni miongoni mwao.
Hii inasababishwa na kutokuwa na chapa bora kimataifa. Moja ya upungufu mkubwa wa Maua Sama ni kushindwa kujitengenezea chapa imara inayomtofautisha kibiashara.
Mashabiki wanamkumbuka kwa nyimbo, lakini si kwa ‘uwepo mkubwa’ kwenye mitandao ya kijamii, fasheni, au uhusiano wa kibiashara na kampuni kubwa.
Miaka ile sio ya sasa. Ngoma nyingi za Sama zimekuwa na namba ndogo YouTube na kwenye streams nyingine za muziki, na hiyo inatokana na ukosefu wa promotion kubwa. Sauti yenye ubora ipo, lakini push haipo.
Hata hivyo, hayupo active. Mara nyingi huachia nyimbo baada ya muda mrefu na kukaa kimya, jambo linalopoteza mwendelezo wake kwenye gemu.
KOLABO ZA NJE
Tofauti na Zuchu au Nandy ambao wanashirikiana na majina makubwa barani Afrika, Maua Sama mara nyingi amefanya kolabo ndani ya mipaka ya Tanzania. Hii inamkwamisha kupenya kimataifa.
Mwanadada huyo amefanya kolabo nyingi za ndani kama na Ben Pol This Love, Harmonize Niteke, Dully Sykes Zali na nyinginezo, lakini kimataifa chache.
Wasanii wa nje kama Tyla, mbali na kipaji, wamekuwa na menejimenti ambayo inawasimamia vizuri na kuwapa promo kubwa, kupata uwezekano wa kolabo na wasanii wanaosikilizwa duniani.
Wazungu wanasema: “Sitting on a gold mine but not making use of it”, wakimaanisha mtu au jamii ina kitu cha thamani kubwa kama dhahabu, lakini hakitumiki au hakithaminiwi ipasavyo. Msemo huu unaendana na hili la Sama, ambaye amekuwa kwenye gemu kwa muda mrefu, lakini mashabiki hawajapata kile walichotarajia kwake kwenda kimataifa zaidi.
Lakini bado hajachelewa. Ni mipango. Kama makampuni yataangalia fursa kwake, itakuwa rahisi kushirikiana naye ili kuendeleza kipaji chake.