Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WCB ya zamani inavyozitesa sherehe za Diamond platnumz

DIAMOND Pict

Muktasari:

  • Harmonize, Rayvanny, Mbosso na Lava Lava walipokuwa WCB, uwepo wao kwenye matukio ya Diamond na familia yake ulikuwa jambo la kawaida. Walifika kama mastaa, lakini pia walikuja na watu wao, marafiki zao na mastaa wengine waliokuwa karibu nao.

UKIRUDI nyuma kwenye sherehe za familia ya Diamond Platnumz za miaka ya nyuma, kuna kitu ambacho ni rahisi kukiona; wasanii wa WCB hawakuwa wageni wa kawaida. Walikuwa sehemu ya burudani yenyewe.

Harmonize, Rayvanny, Mbosso na Lava Lava walipokuwa WCB, uwepo wao kwenye matukio ya Diamond na familia yake ulikuwa jambo la kawaida. Walifika kama mastaa, lakini pia walikuja na watu wao, marafiki zao na mastaa wengine waliokuwa karibu nao.

Katika sherehe, walitumbuiza, wakaimba, wakacheza, wakataniana, wakanywa na kufurahia pamoja na wengine.

Matokeo yake, tukio la kifamilia liliweza kuwa burudani kubwa iliyozalisha picha, video, vichwa vya habari na gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

DIAM 01


TIFFAH ALIKUWA MFANO

Ukianza na 40 ya Princess Tiffah, unakutana na picha ya WCB ambayo mashabiki wengi wanaikumbuka.

Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa sherehe kubwa za kifamilia za Diamond zilizofuatiliwa kwa karibu, huku mastaa mbalimbali wakihudhuria. Kipindi hicho WCB ilikuwa ikikua kwa kasi na wasanii wake walikuwa karibu na Diamond katika kazi na maisha ya kijamii.

Katika mazingira kama hayo, wasanii wa WCB walikuwa sehemu ya burudani. Uwepo wao uliifanya sherehe isiishie kwenye familia pekee; mastaa walikuja, muziki ukapigwa, watu wakacheza na matukio yaliyokuwa yakitokea katika sherehe yakawa habari yenyewe.

Ndiyo maana ukirudi kwenye picha za zamani, unakuta Diamond, WCB na mastaa wengine wakiwa kama kundi moja la burudani.


DIAM 02

BIRTHDAY ZA DIAMOND, MAMA DANGOTE

Haikuwa 40 za watoto pekee. Birthday za Diamond na Mama Dangote nazo zilikuwa sehemu ambayo wasanii wa WCB walionekana karibu. Diamond akiwa mwenyeji, wasanii wake walikuwa miongoni mwa watu walioweza kufanya tukio liwe na burudani zaidi.

Hata mwaka 2016, WCB ilifanya birthday ya Rayvanny nyumbani kwa Diamond Madale, huku Rayvanny akikabidhiwa gari aina ya RAV4. Harmonize naye alikuwa amepokea Mark X katika kipindi hicho.

Hii ilikuwa picha ya kipindi ambacho mafanikio ya wasanii hao na maisha ya Diamond yalikuwa yakionekana kwa karibu sana.


DIAM 03

SHEREHE ZA WASAFI ZENYEWE

Halafu kulikuwa na matukio ya WCB yenyewe uzinduzi, hafla na sherehe mbalimbali za lebo.

Hapa ndipo nguvu ya kundi ilipoonekana zaidi. Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Lava Lava na Diamond walipokuwa pamoja, haikuwa lazima kila mmoja awe amepangiwa kutumbuiza. Uwepo wao wenyewe ulikuwa burudani.

Mmoja angeimba, mwingine akacheza, mwingine akatoa utani, huku mastaa wengine waliokuwa marafiki zao wakiongeza idadi ya watu maarufu kwenye tukio.

Kwa hiyo, WCB ilikuwa kama mtandao wa mastaa ndani ya mtandao wa mastaa.


DIAM 04

MMOJA BAADA YA MWINGINE

Lakini picha hiyo ilianza kubadilika baada ya wasanii hao kuondoka mmoja baada ya mwingine. Harmonize aliondoka mwaka 2019, Rayvanny mwaka 2022, Mbosso mwaka 2025 na Lava Lava mwaka 2025.

Kwa maana hiyo, ndani ya miaka michache, Diamond alipoteza kwenye kundi lake la awali wasanii wanne ambao walikuwa si waimbaji tu, bali pia walikuwa na majina yao, mashabiki wao na circle zao za watu maarufu. Hapo ndipo suala la sherehe linapopata maana nyingine.


SI WASANII TU, WALIKUWA NA WATU WAO

Harmonize alikuwa na watu wake, Rayvanny alikuwa na watu wake, Mbosso na Lava Lava nao walikuwa na marafiki na mastaa waliokuwa karibu nao.

Walipofika kwenye sherehe ya Diamond, hawakuja peke yao kila wakati. Uwepo wao uliweza kuvuta watu wengine maarufu.

Ndani ya ukumbi ukapata mchanganyiko wa mastaa, wanamuziki, marafiki wa Diamond na watu waliokuja kusherehekea pamoja.

Na hawa wasanii walipokuwa wanaingia kwenye burudani, kamera zilikuwa zinawafuata.

Video ya Harmonize akicheza, Rayvanny akitumbuiza, Mbosso akishiriki burudani au Lava Lava akifanya utani inaweza kusambaa Instagram, Facebook, YouTube na TikTok, huku vyombo vya habari vikifanya habari kutokana na kilichotokea ndani ya sherehe. Kwa hiyo, walikuwa sehemu ya burudani na maudhui ya sherehe.


DIAM 05

SANDRA, PICHA MPYA

Sasa njoo kwenye 40 ya Sandrah Naseeb, mtoto wa Diamond na Zuchu, iliyofanyika Septemba 12, 2026, Saint Laurent Garden, Kawe.

Sherehe ilikuwa na familia, mastaa na burudani. Lakini kwa mtu aliyefuatilia kwa muda mrefu matukio ya Diamond, kuna tofauti ambayo inaweza kuonekana.

Wale mastaa wanne wa WCB ya zamani hawakuwepo.

Si kwamba hakuna wasanii wengine walioweza kuburudisha, lakini ukikumbuka namna Harmonize, Rayvanny, Mbosso na Lava Lava walivyokuwa wakishiriki matukio ya zamani, unaona pengo lao.

Zamani ungeweza kupata msanii akichukua kipaza sauti bila hata kuwa sehemu rasmi ya ratiba, mwingine akicheza na wageni, mwingine akifanya utani, huku video zikisambaa mitandaoni. Hilo lilifanya sherehe iwe na matukio mengi ya kuzungumziwa hata baada ya wageni kuondoka.


JE, BADO WANA UKARIBU?

Kuondoka WCB hakumaanishi moja kwa moja wamekuwa maadui wa Diamond. Baadhi yao wameendelea kuonekana wakizungumza kwa heshima kuhusu Diamond na watu wa Wasafi.

Kwa hiyo, wanapokosekana kwenye sherehe za familia, maswali yanabaki: Wanaalikwa? Wamealikwa lakini ratiba zinawazuia? Au ule utamaduni wa kuwa sehemu ya matukio ya familia uliishia pamoja na kipindi chao cha WCB?

Bila kauli ya wahusika, hakuna sababu ya kusema hawajaalikwa au kuna ugomvi.


KINACHOKOSEKANA NI ULE MCHANGANYIKO

Labda si ukubwa wa sherehe za Diamond unaobadilika. Labda si idadi ya wageni.

Kilichobadilika ni watu waliokuwa wakifanya sherehe hizo ziwe na matukio mengi ndani ya tukio moja.

WCB ya zamani ilikuwa na mastaa ambao kila mmoja alikuwa na jina lake na circle yake, lakini wote walikuwa ndani ya kundi moja. Walipokutana kwenye sherehe ya Diamond, burudani ilijitengeneza yenyewe muziki, kucheza, utani, marafiki, picha na video. Leo kila mmoja ana safari yake.

Harmonize yuko nje ya WCB, Rayvanny ana Next Level Music, Mbosso anaendelea na safari yake binafsi na Lava Lava naye yuko nje ya lebo.

WCB bado ipo. Diamond bado anafanya sherehe. Mastaa bado wapo. Lakini ile timu ya zamani iliyokuwa ikifika kwenye sherehe na kuifanya iwe habari yenyewe haipo tena.

Na labda hapo ndipo jibu la kwa nini sherehe za Diamond za sasa zinaweza kumfanya shabiki wa zamani aseme: “Kuna kitu hakipo kama zamani.”