Mambo sita yanayouweka mziki wa Hip hop rehani
Muktasari:
- Hali hiyo sio tu kwenye chati za Billboard pekee hata Bongo kwenye wasanii 10 wanaosikilizwa zaidi mitandaoni, Hip Hop au Rap inaingiza msanii mmoja au hakuna kabisa.
KWA mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 35, hakuna hata wimbo mmoja wa Hip Hop ulioingia ndani ya 40 bora za Billboard Hot 100, chati maarufu zaidi ya muziki duniani.
Tukio hili limeibua mjadala mkubwa kuhusu hatma ya muziki wa Hip-Hop na nafasi yake katika soko la muziki wa kimataifa.
Hali hiyo sio tu kwenye chati za Billboard pekee hata Bongo kwenye wasanii 10 wanaosikilizwa zaidi mitandaoni, Hip Hop au Rap inaingiza msanii mmoja au hakuna kabisa.
YouTube mwezi uliopita ilitoa orodha ya wasanii 10 wanaongoza kwa kusikilizwa lakini Darassa peke yake alishika nafasi ya 10 huku nyingine zikikamatwa na Bongo Fleva.
Diamond Platnumz mwenye takribani wasikilizaji milioni (9.7M), akifuatiwa na Mbosso (6.79M), Harmonize (6.54M), Marioo (6.43M), Jux (6.48M). Wengine katika 10 bora ni Rayvanny (4.81M), Zuchu (3.8M), Jay Melody (3.2M), Alikiba (3.12M), na Darassa (2.39M).
HISTORIA ILIYOVUNJIKA
Kwa mujibu wa jarida la Billboard, hali hiyo imejitokeza baada ya wimbo wa Kendrick Lamar na SZA, ‘Luther’, uliowahi kushika namba moja kwa wiki 13 mfululizo, kuondolewa rasmi kwenye chati ya Oktoba 2025.
Wimbo huo uliondolewa kufuatia kanuni mpya za Billboard Hot 100, ambazo zinataka kwamba nyimbo ambazo zimekuwa kwa muda mrefu kwenye chati na kushuka chini ya nafasi fulani, zinatolewa ili kutoa nafasi kwa nyimbo mpya.
Baada ya kuondoka kwa ‘Luther’, haikubaki wimbo hata mmoja wa rap katika chati za nyimbo 40 za juu jambo ambalo halijawahi kutokea tangu Februari 1990.
Mara ya mwisho hali kama hiyo kutokea ilikuwa kipindi ambacho wimbo wa Biz Markie ‘Just a Friend’ ulikuwa ukishika nafasi ya 41, kabla ya kupanda wiki iliyofuata hadi nafasi ya 29 na kuanzisha historia ya miaka 35 ya uwepo wa nyimbo za rap ndani ya Top 40.
MMOJA TU
Kwenye chati ya Oktoba 2025, wimbo wa rap uliofanya vizuri zaidi ulikuwa mmoja tu ‘Shot Callin’ wa YoungBoy Never Broke Again, ulioshika nafasi ya 44, huo pekee ndio ulikaribia kufanya vizuri.
Wengine waliokuwa karibu na Top 40 ni Cardi B kupitia wimbo wake ‘Safe’ akiwa na Kehlani, ulioshika nafasi ya 48, na BigXthaPlug kupitia ‘Hell at Night’ akiwa na Ella Langley, ulioshika nafasi ya 49.
Hata hivyo, hakuna kati ya nyimbo hizo zilizoweza kupenya ndani ya Top 40, hali iliyodhihirisha kuporomoka kwa nguvu ya kibiashara ya rap kwa sasa.
KANUNI IMECHANGIA
Billboard ilifanya marekebisho ya kanuni zake mwezi Oktoba mwaka huu, hatua iliyoweka vigezo vipya vya kuondoa nyimbo kongwe kutoka kwenye chati kuu.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, wimbo wowote unaoshuka chini ya nafasi ya 25 baada ya kukaa zaidi ya wiki 26, huondolewa moja kwa moja kwenye chati.
Mabadiliko hayo ndiyo yaliyosababisha ‘Luther’ ya Kendrick Lamar na SZA kuondolewa, ikiwa ilikuwa imedumu kwa wiki 46 kwenye chati.
Kwa bahati mbaya, hata baada ya nyimbo nane ikiwemo Luther kuondolewa wiki hiyo, hakuna wimbo wa rap uliokuwa karibu kupanda ni kama uliporomosha zaidi.
Hali hii imezidishwa zaidi na albamu mpya ya Taylor Swift, The Life of a Showgirl, ambayo nyimbo zake zote 12 zimekuwa kwenye Top 40 kwa wiki tatu mfululizo, ikiziba nafasi ambazo rap ingeweza kuchukua.
KIBIASHARA
Kwa miaka mingi, muziki wa rap na Hip-Hop umekuwa ukitawala sekta ya muziki duniani. Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kupungua kwa kasi kwa ushawishi huo.
Mwaka 2020, rap ilikuwa inashikilia karibu asilimia 30 ya soko la muziki nchini Marekani. Mwaka 2023, sehemu hiyo ilishuka hadi asilimia 25 na kufikia Oktoba 2025 imeripotiwa kushuka hadi asilimia 24 pekee.
Hii inamaanisha kuwa muziki wa rap unapoteza sehemu ya mashabiki wake kwa aina nyingine za muziki kama pop, R&B, na Country, ambazo zimeanza kushika kasi kubwa katika majukwaa ya kusikiliza muziki mtandaoni kama Spotify na Apple Music.
Kwa kulinganisha kwenye chati ya Oktoba 24, 2020 nyimbo 16 kati ya 40 bora zilikuwa za rap. Mwaka 2023, nyimbo nane pekee za rap ndizo zilikuwa ndani ya Top 40 na sasa mwaka 2025 hakuna hata moja.
MASTAA KUKAA KIMYA
Wataalam wa muziki wanaona kuwa kuporomoka huko kumechangiwa pia na ukimya wa wasanii wakubwa wa rap.
Drake ambaye ndiye msanii mwenye nyimbo nyingi zaidi kuwahi kuingia Billboard Hot 100, bado hajatoa albamu yake inayosubiriwa kwa muda mrefu tangu atangaze kuiachia ‘Iceman’.
Kwa upande mwingine, Kendrick Lamar naye amepumzika kidogo baada ya kipindi cha mafanikio makubwa kilichodumu kwa miezi 18 na aliweka rekodi kadhaa na kushinda tuzo nyingi.
Ingawa muziki wa rap haujanyamaza kabisa, Cardi B na BigXthaPlug wameachia albamu mpya tangu Agosti, huku Drake akiendelea kutoa nyimbo za kujenga hamasa kabla ya albamu yake rasmi kutoka.
WIKI HII
Kwenye chati mpya ya Billboard Hot 100 ya mwezi Novemba 2025, hali bado ni ile ile hakuna wimbo wa rap ndani ya Top 40. Hii inamaanisha ni wiki ya pili mfululizo bila rap kwenye nafasi za juu.
Hata hivyo, “Shot Callin” ya YoungBoy Never Broke Again imepanda hatua moja kutoka nafasi ya 44 hadi 43, ishara huenda hali hii ikabadilika muda si mrefu.
WASIKIE WATAALAMU
Mtaalam wa muziki kutoka Chuo Kikuu cha New York, Profesa Andrea Mills anasema hali hiyo ni ishara ya mabadiliko ya ladha ya wasikilizaji wanahitaji vitu vipya.
“Mashabiki wa muziki sasa wanataka nyimbo zenye vionjo mchanganyiko si rap pekee. Hii ndiyo sababu pop na R&B zimeanza kuchukua nafasi zaidi kwenye chati,” anasema Mills
Mchambuzi wa muziki Marekani, Jon Pareles anasema kupanda kwa umaarufu wa nyimbo za TikTok na muziki wa dansi kumechangia kushusha nguvu ya rap, kwani nyimbo hizo huenea haraka zaidi mitandaoni.
“Tik Tok imekuwa ikisaidia muziki wa R&B, Amapiano ambao unachezeka zaidi na kufanya watu wafanye chalenji nyingi umeongeza soko na kuzima kabisa muziki wa Rap.”
Kutokuwepo kwa nyimbo za rap kwenye orodha ya juu 40 za Billboard Hot 100 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990 ni ishara ya mabadiliko makubwa katika tasnia ya muziki.
Wakati muziki wa rap ukijaribu kurejea kileleni, changamoto kubwa ipo kwa wasanii na wazalishaji kuhakikisha wanatoa kazi zenye mvuto mpya na zinazokidhi ladha ya kizazi kipya cha wasikilizaji.
Kwa sasa, dunia inasubiri kuona kama Drake, Kendrick Lamar, Cardi B au kizazi kipya cha rappers kitaweza kuirudisha rap kwenye nafasi yake ya kifahari kwenye chati za muziki duniani.