Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Diamond awakutanisha Zuchu na mama Dangote

DIAMOND Pict

Muktasari:

  • Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond ametangaza kuwa sherehe hiyo itafanyika Septemba 12, 2026, kuanzia saa tisa alasiri.

MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, ameibua gumzo baada ya kutangaza sherehe ya siku 40 ya mtoto wake wa kike aliyempata na mke wake, Zuchu, huku sherehe hiyo ikitarajiwa kufanyika nyumbani kwa mama yake, Mama Dangote, eneo la Tegeta Madale jijini Dar es Salaam.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond ametangaza kuwa sherehe hiyo itafanyika Septemba 12, 2026, kuanzia saa tisa alasiri.

Tangazo hilo limekuwa gumzo kutokana na eneo lililochaguliwa, kwani Madale ni nyumbani kwa Mama Dangote, hivyo safari hii sherehe hiyo inawaweka pamoja Zuchu na mama mkwe wake katika tukio la kifamilia litakalovuta macho ya mashabiki.

Kwa muda mrefu, uhusiano wa Mama Dangote na Zuchu umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na mashabiki, huku mitandao ya kijamii ikiwa na simulizi mbalimbali kuhusu ukaribu wao.

Hata hivyo, si sahihi kuchukulia tetesi hizo kama ushahidi kwamba wawili hao hawaelewani, kwa kuwa hakuna uthibitisho wa wazi unaoonyesha kuwa wana ugomvi.


DIAM 02

HOSPITALI MACHO YALIKUWA KWA MAMA DANGOTE

Baada ya Zuchu kujifungua Agosti 2, 2026, watu kadhaa wa karibu na familia walionekana mitandaoni wakifika hospitalini kumjulia hali mama na mtoto, huku Diamond pia akionekana kuwapokea baadhi ya wageni.

Katika hali hiyo, baadhi ya mashabiki waliendelea kujiuliza kuhusu uwepo wa Mama Dangote hospitalini, hasa kwa kuwa walikuwa wakitarajia kumuona katika kipindi hicho muhimu kwa mtoto wake na mjukuu mpya.

Lakini baada ya Zuchu kuruhusiwa kutoka hospitalini, yeye, Diamond na mtoto wao walielekea Madale, nyumbani kwa Mama Dangote.

Hatua hiyo ilitoa picha kwamba pamoja na mijadala inayozunguka mitandaoni, familia iliendelea kushirikiana katika kumpokea mtoto huyo mpya.

Na sasa Diamond ameongeza kitu kingine, akichagua Madale kuwa sehemu ya 40 ya mtoto wake.


DIAM 01

40 HII INAKUJA NA HISTORIA

Diamond kufanya sherehe ya 40 kwa mtoto wake si jambo geni, kwani watoto wake kadhaa wamewahi kupata hafla kama hiyo.

Mtoto wake mkubwa, Tiffah, aliyempata na Zari Hassan, aliwahi kufanyiwa sherehe ya siku 40 mwaka 2015. Tiffah alizaliwa Agosti 6, 2015 na sherehe yake ya 40 ikafanyika Septemba 20, mwaka huo, katika mazingira ya kifamilia yaliyohudhuriwa na watu mbalimbali.

Baadaye, mtoto mwingine wa Diamond na Zari, Nillan, naye alifanyiwa sherehe ya 40. Nillan alizaliwa Desemba 6, 2016, akatimiza siku 40 Januari 16, 2017, huku sherehe yake ikifanyika baadaye nyumbani Madale.

Si Tiffah na Nillan pekee, kwani Naseeb Junior, mtoto wa Diamond aliyempata na mwanamitindo Tanasha Donna, naye aliwahi kufanyiwa sherehe ya 40 mwaka 2019.

Sherehe hiyo ilifanyika Madale na ilikuwa pia miongoni mwa matukio yaliyomfanya Diamond na Tanasha kumuonyesha mtoto wao kwa umma.

Hivyo, Madale imekuwa na historia katika sherehe za 40 za watoto wa Diamond, na sasa mtoto wake na Zuchu anaingia kwenye orodha hiyo.


DIAM 03

SASA MACHO MADALE

Kinachofanya tukio la Septemba 12, 2026 kuwa na mvuto zaidi si sherehe yenyewe pekee, bali ni watu watakaokuwa sehemu yake.

Baada ya Diamond na Zuchu kupata mtoto na baadaye kwenda Madale, sasa familia inatarajiwa kukutana tena katika sherehe rasmi ya 40.

Macho ya mashabiki yataelekezwa kwa Mama Dangote na Zuchu, wakisubiri kuona namna watakavyoshirikiana katika kumsherehekea mtoto huyo.

Pia, kutokana na historia ya Tiffah, Nillan na Naseeb Junior, 40 hii inaweza kuwa nyingine ya matukio makubwa ya kifamilia ya Diamond yatakayozungumzwa kwenye mitandao.

Kwa kifupi, Diamond amewakutanisha Zuchu na Mama Dangote katika tukio moja huko Madale.