Maisha mapya Ciara nje ya NFL
Muktasari:
- Ciara ambaye alimshirikisha staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz katika wimbo wake, Low (2025), uhusiano wake na Wilson ni wa miaka mingi, na hata mapenzi yake kwa NFL ni ya muda marefu.
STAA wa RnB na Pop, Ciara ameanza maisha mengine baada ya mume wake, Russell Wilson kustaafu rasmi Ligi ya Soka Marekani (NFL), ambapo mwimbaji huyo alikuwa akiimunga mkono na kufurahia kila hatua aliyopiga katika mchezo huo.
Ciara ambaye alimshirikisha staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz katika wimbo wake, Low (2025), uhusiano wake na Wilson ni wa miaka mingi, na hata mapenzi yake kwa NFL ni ya muda marefu.
Juni 3, Wilson alitangaza kustaafu NFL baada ya kuitumikia ligi hiyo kwa miaka 14 kwa mafanikio makubwa, ambapo aliwahi kushinda ubingwa wa Super Bowl 2014 akiwa na timu ya Seattle Seahawks, wakiifunga Denver Broncos.
"Siku zote ninajivunia kuwa na wewe, ni baraka kubwa kuambatana nawe katika safari hii. Wewe ndiye sababu kubwa ya mimi kupambana, unanipa hamasa kubwa.." alieleza Ciara muda mfupi baada ya Wilson kutangaza uamuzi huo.
Hata hivyo, Wilson ambaye hadi anastaafu alikuwa akiichezea New York Giants, bado anaendelea kuwepo katika ulimwengu wa michezo kwani tayari amejiunga na kituo cha CBS Sports ambapo anafanya kazi kama mchambuzi wa michezo ya NFL.
Wilson ambaye kwa mara ya kwanza alionekana akiwa na Ciara Aprili 2015 huko Seattle, katika tangazo lake la kustaafu alimshukuru mwanamuziki huyo akitamja kama baraka katika maisha yake binafsi na ya kazi pia.
"Asante sana Ciara kwa kuwa umekuwa baraka yangu kubwa zaidi niliyowahi kuipata katika maisha yangu. Wewe ni rafiki yangu wa karibu na mshirika wangu katika kila jambo. Safari hii ya maisha isingeenda sawa bila uwepo wako," amesema Wilson kupitia video aliyoposti katika mitandao ya kijamii.
Januari 2023, Ciara kupitia Instagram aliandika ujumbe wa kumtia moyo Wilson akisema amemuona akivumilia mambo mengi na bado akaba kikuwa imara. Ujumbe huo ulikuja baada ya mchezaji huyo kuwa na msimu mbaya katika timu yake ya Denver Broncos.
"Siku zote kile ninachojua ni kwamba mshindi ni mtu anayesimama tena baada kuanguka, mtu ambaye haachi kuamini. Mtu anayekumbatia changamoto na kubaki mtulivu katikati ya yote," aliandika na kuongeza.
"Mshindi ni mtu ambaye hawezi kuathiriwa na maneno ya watu au maoni ya wengine. Ni mtu anayependa kuwapenda wengine, kuwahudumia wengine, na kila mara yupo kwa ajili ya familia yake. Yote hayo ni wewe!" alieleza Ciara, mkali wa kibao cha How We Roll (2023).
Hata hivyo, Machi 2024, NFL walitangaza Wilson hatakuwa sehemu ya kikosi cha Denver Broncos, jambo lililomfanya kuwa mchezaji huru kisha kuja kusaini mkataba wa mwaka moja na New York Giants, na baada ya mkataba huo kuishi ndipo akatangaza kustaafu.
Miezi mitatu baada ya Wilson kustaafu, Ciara alitangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa nne katika ndoa yao. Huyo atakuwa mtoto wa kwanza wa Ciara ambaye hatapata bahati ya kushuhudia live baba yake akicheza uwanjani.
Ciara ambaye alifanya vizuri na ngoma yake na Bow Wow, Like You (2005), anaenda kuwa mama kwa mara ya kwanza katika kipindi ambacho mume wake Wilson si mchezaji tena wa NFL.
Akizungumza na mtandao wa Entertainment Tonight mnamo Septemba, Ciara amesema mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka tisa, Sienna ndiye alikuwa wa kwanza kugundua kuwa alikuwa mjamzito kabla hajawaambia watoto wake kuhusu ujauzito huo.
"Sienna aliniambia kwamba nilikuwa mjamzito kabla sijawaambia watoto wote. Aliniambia wakati huo bado tumbo langu halikuwa kubwa. Nilikuwa bado sijaonyesha mabadiliko yoyote katika mwili lakini yeye ana hisia za kugundua," amesema Ciara.
Ikumbukwe kabla ya kuolewa na Wilson, tayari Ciara alikuwa na mtoto mmoja ambaye alimpata katika uhusiano na mwanamuziki wa rap, Future. Hivyo kwa ujumla mtoto ajaye atakuwa watano kwa Ciara, ila wanne katika ndoa yake na Wilson.
Ciara na Wilson walifunga ndoa Julai 6, 2016 katika sherehe ya faragha iliyofanyika Peckforton Castle, Cheshire nchini Uingereza. Waliohudhuria ni familia na marafiki wa karibu wakiwemo wanamuziki, Jennifer Hudson na Kelly Rowland, msanii wa zamani wa kundi la Destiny's Child.