Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VYUMA: Kolabo Bongo zilizoweka rekodi tamu

KOLABO Pict

Muktasari:

  • Ushirikiano huo umewasaidia wasanii wa Bongo sio tu kuongeza mashabiki wapya, bali pia kupata nafasi ya kuingia kwenye majukwaa makubwa ya muziki duniani kama vile Billboard, Apple Music na MTV Base.

KIPINDI cha hivi karibuni muziki wa Bongo Fleva umeendelea kukua na kuvuka mipaka ya Tanzania hadi kufikia jukwaa la kimataifa. Hii ni kutokana na wasanii wa Bongo kufanya kolabo na mastaa wakubwa kutoka mataifa mbalimbali duniani, jambo ambalo limechangia kukuza muziki huo na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Ushirikiano huo umewasaidia wasanii wa Bongo sio tu kuongeza mashabiki wapya, bali pia kupata nafasi ya kuingia kwenye majukwaa makubwa ya muziki duniani kama vile Billboard, Apple Music na MTV Base. Mwanaspoti linakuletea kolabo za mastaa wa Bongo walioshirikisha mataifa mbalimbali na zikafanya vizuri na kushika chati mbalimbali za muziki duniani.

KOLA 01

1. Jux ft Phyno (God Design)

Hii ilikuwa kolabo ya kwanza ya Jux kufanya na msanii kutoka Nigeria na ngoma hiyo iliachiwa miezi mitano iliyopita ikiwa na zaidi ya wasikilizaji milioni tatu kwa audio na watazamaji milioni sita katika video.

Wimbo huo ulitoka siku chache baada ya Jux kutangaza harusi na mkewe Priscila Ojo, raia wa Nigeria, na ulitumika kwenye promo ya sherehe ya msanii huyo iliyofanyika Nigeria na ile ya hapa Tanzania.

Kolabo na Phyno ilifanya ngoma hiyo ishike namba moja Nigeria ambako ni kati ya masoko magumu ya kuuzia muziki kutokana na ushindani wa mastaa wengi wanaovuma kimataifa wanaozaliwa katika taifa hilo. Ndani ya wiki nzima, ngoma hiyo ilifanya vizuri zaidi Nigeria na kuzipiga chini hadi albamu ya mkali wa Afrobeat, Davido (5ive), iliyotarajiwa kufanya vizuri.

Hata hivyo, ndoa ya Jux na mtoto wa muigizaji maarufu nchini humo, Iyabo Ojo, ni kati ya sababu zilizochangia ngoma hiyo kupendwa kutokana na umaarufu wa familia hiyo na ushawishi wake kwenye sanaa.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Jux ngoma yake kuingia trending namna hiyo tangu aanze kufanya muziki mwaka 2008.

Kolabo hiyo pia ilimfanya achaguliwe kuwa Best East African Artist of the Year kwenye tuzo za muziki za The Headies zinazotolewa kila mwaka nchini Nigeria.

KOLA 02

2. Diamond Platnumz ft Jason Derulo (Komasava)

Kwenye chati za wasanii wa Afrika wanaofanya vizuri kimataifa huwezi kuliacha jina la mkali wa ngoma ya Msumari, Diamond Platnumz. Diamond ameshafanya kolabo na wasanii mbalimbali duniani kama Alicia Keys (Wasted Energy), Ciara (Low), Rick Ross (Waka Waka), Ne-Yo (Marry You) na nyinginezo.

Hizo ni baadhi tu ya ngoma alizofanya na wasanii wakubwa, lakini Komasava ilifanya vizuri zaidi na kuingia kwenye chati maarufu za muziki nchini Marekani ziitwazo USA Billboard na kuweka rekodi.

Wimbo huo ulioachiwa Julai mwaka 2024 uliingia katika chati hizo ukiwa ingizo jipya na kushika nafasi ya 39 katika kipengele cha Afrobeats Songs Top 50.

Jambo hilo liliifanya Komasava kuwa wimbo wa kwanza kutoka Tanzania kuingia katika chati hizo kubwa Marekani na duniani kwa ujumla. Mei 3, 2024, Diamond aliiachia audio ya Komasava akiwa amewashirikisha wakali wawili wa Amapiano kutoka Afrika Kusini, Khalil Harisson na mwanadada Chley. Baadaye akafanya remix na Derulo aliyeweka verse nyingine.

Baada ya hapo, wimbo huo uliendelea kukaa katika nafasi za juu kwenye chati mbalimbali za muziki duniani mpaka Agosti 6, 2024, ilipotoboa hadi Billboard.

Wasanii kutoka Nigeria na Afrika Kusini wamekuwa wakitawala kwenye chati hizo ambapo wakati Komasava ikiwa namba 39, mwanadada Tyla kutoka Afrika Kusini ndiye alishika namba moja na ngoma yake Water.

KOLA 03

3. Rayvanny ft Shreya Ghoshal, Nora Fatehi (Ooh Mama Tetema)

Kama kuna kolabo aliyofanya Rayvanny ikafanya vizuri zaidi basi ni wimbo wa Mama Tetema ambao umekuwa kama filamu ukitolewa remix nne.

Wimbo rasmi ulitoka mwaka 2019 ambapo Rayvanny alimshirikisha Diamond Platnumz na ukatesa siyo Tanzania tu, bali Afrika na duniani, kabla ya kuwashirikisha baadhi ya wasanii akiwamo Patoranking na Zlatan, na hadi sasa una zaidi ya watazamaji milioni saba.

Mwaka 2021 alifanya remix nyingine na Maluma raia wa Colombia, ambayo ilifanya vizuri na kupata zaidi ya watazamaji milioni 56. Hivi karibuni, wimbo huo umetolewa tena remix ya nne, na safari hii ukiwashirikisha wasanii kutoka Afrika na Asia, Nora Fatehi ambaye ni muigizaji na dansa maarufu wa India, pamoja na Shreya Ghoshal ambaye ni miongoni mwa waimbaji bora wa Bollywood.

Kwa mujibu wa YouTube na takwimu za muziki wa kimataifa, video hiyo ilikusanya watazamaji 7,402,890 ndani ya saa 24, ikizipita nyimbo kutoka kwa mastaa wa dunia kama Bruno Mars & ROSÉ, Yo Yo Honey Singh na Ed Sheeran.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa msanii wa Tanzania kushika namba moja kwenye orodha ya Most Viewed Videos ndani ya muda huo duniani kote. Hii sio mara ya kwanza kwa wimbo huo kufanya vizuri duniani kwani hata mwaka 2021 ulimpa mafanikio makubwa Rayvanny baada ya kumshirikisha Maluma.

Ushirikiano na msanii Maluma (Colombia) kwenye wimbo huo mwaka 2021 ulimfanya kuandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs).

Kwa mantiki hiyo, ngoma ya Tetema ambayo ilitoka rasmi mwaka 2019, imekuwa na bahati ya kushirikishwa mara nyingi na inaweza kuwa ngoma ya nyota huyo iliyofanya vizuri zaidi na kumfungulia milango kimataifa.

KOLA 04

4. Zuchu ft Spice (Amanda Remix)

Tangu atambulishwe na lebo ya Wasafi mwaka 2020, amekuwa moja ya wasanii wanaofanya vizuri Afrika Mashariki na Kati na kuleta ushindani kwenye soko la muziki wa Bongo Fleva. Wimbo rasmi wa Amanda ulitoka miezi miwili iliyopita akiimba Zuchu peke yake na ni kati ya nyimbo zilizokosolewa na baadhi ya mashabiki. Licha ya baadhi ya mashabiki kutopendezwa na wimbo huo, lakini ndani ya muda mchache ulifanya vizuri na kuingiza zaidi ya watazamaji milioni nane.

Sasa baada ya kufanya vizuri, Zuchu akatoa remix ya wimbo huo akimshirikisha rapa maarufu kutoka Jamaica, Spice.

Remix hiyo imetoka wiki mbili zilizopita na imeandika historia kimataifa baada ya kutajwa na jarida maarufu la muziki Billboard kwenye orodha ya September Reggae/Dancehall Fresh Picks of the Month.

Billboard imeorodhesha nyimbo 10 mpya za reggae, dancehall na soca zinazotakiwa kusikilizwa, zikijumuisha majina makubwa kama Prince Swanny, Skillibeng & Vybz Kartel, Chronic Law pamoja na Zuchu.

Kolabo hiyo imempa hatua kubwa Zuchu kuonekana kwenye ramani ya muziki wa dunia, jambo ambalo linaendelea kuonyesha nguvu ya wasanii wa kike kwenye soko hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na nyota wa Afrika Kusini, Tyla.