Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Diamond, Zuchu walivyotawala Henna Night

HINA Pict

Muktasari:

  • Zuchu amefanyiwa sherehe hiyo ambayo ni ya kifamilia na kitamaduni kuelekea tukio la 40 ya mtoto wake aliyejifungua Agosti 2, 2026.

TUKIO la Henna Night kwa ajili ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuchu, lilikuwa la aina yake, huku mapenzi, taarabu, dansi, mavazi na furaha vikitawala katika hafla hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Mama Dangote, Sanura Abdul, eneo la Madale jijini Dar es Salaam.

Zuchu amefanyiwa sherehe hiyo ambayo ni ya kifamilia na kitamaduni kuelekea tukio la 40 ya mtoto wake aliyejifungua Agosti 2, 2026.

Mwanaspoti lilikuwepo kushuhudia namna sherehe hiyo ilivyokuwa ikichanganya burudani na bashasha, huku Zuchu akiwa kwenye furaha muda wote, akicheza na wageni wake na kufurahia kila kilichokuwa kikiendelea.

Lakini kama kuna sehemu iliyovuta macho ya wengi, ni namna Mama Dangote alivyokuwa sambamba na Zuchu. Wawili hao walionekana kucheza, kukumbatiana na kutunzana, huku nyimbo za taarabu zenye mafumbo zikichangia kuipa sherehe hiyo ladha nyingine.

Hilo likawa kama jibu la vitendo kwa wale ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisema Mama Dangote na Zuchu hawaelewani. Usiku huo, haikuwa picha ya watu wasiopatana, bali Mama Dangote alionekana kumkubali na kufurahia uwepo wa Zuchu katika tukio hilo.

Kwa upande mwingine, Diamond Platnumz ambaye ni mume wa Zuchu, alikuwa karibu na mkewe muda mwingi, wakionyeshana mahaba na kuonekana kufurahia kila dakika ya sherehe hiyo.

Hata muda wa chakula ukawa sehemu ya burudani. Diamond alimnyanyua Zuchu na kwenda naye eneo ambalo chakula kilikuwa kikichukuliwa, kisha wawili hao wakatumia sahani moja kula huku Diamond akionekana kumlisha Zuchu mara kadhaa.

Kilichozidi kuvutia ni kwamba muziki ulipowashwa, Diamond naye hakuwa mtazamaji. Alionekana kuzijua nyimbo za taarabu zilizokuwa zikipigwa, akiimba pamoja na kuucheza muziki huo huku mara kadhaa akimkumbatia Zuchu, hasa nyimbo zilipokuwa za mapenzi.

Usiku huo muziki ulikuwa mwingi kuliko maneno. Taarabu na kibao kata vilitawala, huku nyimbo za Khadija Kopa zikitawala sehemu kubwa. 

Khadija mwenyewe alikuwepo na alitoa burudani, huku DJ Mtasha akiendelea kuweka nyimbo za taarabu zenye mafumbo ambazo ziliwafanya wageni kucheza na kufurahia.

Hassan Ally naye aliongeza ladha ya kibao kata, kiasi kwamba wageni hawakuwa wakikaa chini muda wote. Muziki ulipowaka, watu waliinuka na kuingia kwenye dansi, huku sherehe ikiendelea kwa shamrashamra.

Miongoni mwa walioutia uzito usiku huo walikuwa wanamuziki wenye ndoa, Nandy na mumewe Bilinas, pamoja na Jux na mkewe Priscilla Ojo, ambao nao walionekana kufurahia sherehe hiyo huku wakikaa pamoja na kuonyesha mahaba.

Sare zilizovaliwa na wageni nazo ziliongeza uzuri wa tukio hilo. Wengi walifika wakiwa wamevalia kwa kuendana na maudhui ya sherehe, hali iliyofanya eneo la tukio kuonekana lenye mvuto wa aina yake.

Zaidi ya yote, aliyekuwa kitovu cha usiku huo alikuwa Zuchu. Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa tukio, alionekana kuwa na furaha, akicheza, akicheka na kufurahia uwepo wa ndugu, marafiki na mastaa waliokuja kusherehekea naye.