Lamar alianza kwa kulipa Sh50,000 Bongo Records
Muktasari:
- Jina la Lamar lilianza kuvuma tangu mwaka 2007 akiwa 41 Records, na tangu wakati huo aliendelea kufanya vizuri hadi sasa anapotambulika kuwa mmoja wa watayarishaji muziki wakali kuwahi kutokea Bongo.
WENGI wanamfahamu Lamar kama mmoja wa watayarishaji muziki Bongo ambao wana uwezo mkubwa na waliofanya mengi katika kiwanda hicho cha burudani.
Jina la Lamar lilianza kuvuma tangu mwaka 2007 akiwa 41 Records, na tangu wakati huo aliendelea kufanya vizuri hadi sasa anapotambulika kuwa mmoja wa watayarishaji muziki wakali kuwahi kutokea Bongo.
1. Mwaka 2001, ndipo Lamar alianza rasmi kujifunza kutayarisha muziki ambapo mara nyingi alienda internet cafe ili kupata kompyuta, kisha kuweka CD yake na kuanza kufanya mazoezi. Kwa sehemu kubwa mazoezi yake yalijikita kwenye kuweka mdundo katika mfumo wa software maana tayari alikuwa ameshajua kutengeneza midundo.
2. Mwaka 2002, Jay Moe akamkutanisha Lamar na mtayarishaji mkubwa wa muziki nchini, P-Funk Majani ambaye ndiye mwanzilishi wa Bongo Records.
3. Jay Moe ambaye ni mmoja wa wasanii wa kwanza kusainiwa Bongo Records, aliwakutanisha wawili hao ili Lamar apete nafasi studio kwa Majani lakini jambo hilo halikufanikiwa. Ikumbukwe mnamo 2000 ndipo Jay Moe alisaini Bongo Records akiwa ndani ya kundi la Wateule, na mwaka uliofuatia akasaini kama msanii wa kujitegemea (solo).
4. Mwaka 2005, Lamar akapata nafasi ya kujiunga G Records ambapo aliendelea kujifunza kutayarisha muziki chini ya usimamizi wa marehemu Roy ambaye naye alitengeneza ngoma zilizovuma sana. Huyu Roy kipindi cha uhai wake alifanya kazi na mastaa kama Mr. Blue (Mapozi, Blue Blue), Noorah (Ice Cream), Suma Lee (Chungwa), Matonya (Vailet), Marlaw (Busu la Pinki) na kadhalika.
5. Mwaka 2006, Dunga wa Madungu Digital akamkutanisha tena Lamar na P-Funk Majani, awamu hii nafasi ikapatikana na akaanza kufanya kazi chini ya Bongo Records akiwa kama msaidizi wa Majani.
6. Kazi kubwa ya Lamar ndani ya Bongo Records ilikuwa ni kuwarekodi wasanii, kisha Majani yeye anakuja kutengeneza midundo na kufanya mixing na mastering. Kwa mujibu wa Lamar, kwa kazi hiyo tu alianza kulipwa Sh50,000, kisha Sh100,000 hadi ikaja kufikia Sh200,000 kwa wimbo mmoja tu.
7. Mwaka 2007, Lamar akaitwa na Dunga ndani ya 41 Records ambapo walianza kufanya kazi pamoja na walifanikiwa kutoa nyimbo nyingi ambazo zilifanya vizuri wakati huo.
8. Ndani ya 41 Records, ndipo Lamar akatoa wimbo wake wa kwanza ambao yeye ndiye alihusika katika kila kitu, na wimbo huo ni wake Joh Makini, Mfalme (2007). Ngoma zake nyingine alizotengeneza akiwa 41 Records ni Heshima (Afande Sele), Mimi (Geez Mabovu), Hao (Mwasiti) na kadhalika.
9. Mwaka 2008, tayari Lamar akawa ndani ya studio yake ya Fishcrab, sehemu ambayo historia kubwa ya muziki wake imeandikwa kwa kutengeneza nyimbo nyingi zilizofanya vizuri. Baadhi ya nyimbo alizotengeneza akiwa Fishcrab ni Asha (TID), Moyo Wangu (Diamond Platnumz), My Everything (Alikiba), Adela (Mrisho Mpoto), Popompoo (Chid Benzi), Mapenzi Gani (Ngwea) na kadhalika.
10. Mwaka 2010, Lamar akashinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Mtayarishaji Bora wa Mwaka akiwazidi kete washindani wake ambao ni Marco Chali, Allan Mapigo, Man Water na Hermy B.