Nandy arejea na ‘911’: Safari ya miaka nane tangu ‘The African Princess’
Muktasari:
- Nandy, mkali wa kibao cha Nimekuzoea (2021), anakuja na 911 ikiwa imepita takribani miaka minane tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records, huku uzinduzi wake ukifanyika Nairobi Kenya.
HATIMAYE staa wa Bongo Fleva, Nandy ameweka wazi jina la albamu yake ijayo ambayo imesubiriwa kwa miaka mingi na mashabiki. Albamu hiyo inakwenda kwa jina la 911, ikiwa ni ya pili kwa mwanamuziki huyo aliyetoka chini ya Tanzania House of Talent (THT).
Nandy, mkali wa kibao cha Nimekuzoea (2021), anakuja na 911 ikiwa imepita takribani miaka minane tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records, huku uzinduzi wake ukifanyika Nairobi Kenya.
Utakumbuka albamu ya The African Princess iliyoachiwa ikiwa na nyimbo 10, ilitoka na ngoma maarufu kama Aibu na Hazipo, huku ukijumuisha ambazo tayari zilikuwa zimetoka awali - One Day, Wasikudanganye, Kivuruge na Ninogeshe.
Hata hivyo, bado Nandy hajaweka wazi namba 911 ina maana gani katika albamu hiyo au katika safari ya muziki wake na hata maisha yake kwa jumla. Lakini kwa sasa wasanii wengi wa Bongo Fleva wanaonekana kutoa albamu na EP zenye majina ya namba ambazo hubeba maana fulani.
Kabla ya Nandy kuja na 911, alianza Lady Jaydee na albamu yake ya nane iliyoitwa 20 (2021), jina ambalo lilikuwa linawakilisha miaka yake 20 katika muziki, na baadaye Mimi Mars akaja na albamu, 17 (2026) yenye maana sawa na hiyo.
Staa wa Konde Music Worldwide, Harmonize, albamu yake ya sita iliyotoka 2026, ameipa jina la 31, ikiwa inawakilisha umri wake ingawa ilipaswa kutoka mwaka uliopita. Kitu kama hicho amekifanya Marioo kupitia EP yake, MMMCXII (2026) inayokilisha tarehe ya kuzaliwa kwake.
Nandy alitambulisha jina la albamu yake (911) katika tamasha lake la Nandy Festival lilofanyika Dar es Salaam wikiendi iliyopita, ikiwa ni msimu wa tano wa tamasha hilo ambalo hupita katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa jumla Nandy anaungana na mastaa wengine wa Bongo Fleva ambao wameshaachia albamu kwa mwaka huu, baadhi yao ni Mimi Mars (17), Harmonize (31), Aika & Nahreel au Navy Kenzo (Steppa).
Utamaduni wa wanamuziki hao kutoa albamu umerudi baada ya kuimarika kwa njia za kuuza muziki mtandaoni (digital streaming), pamoja na kuwepo kampuni za usambazaji muziki kidijitali ambazo hugawa mirabaha kwa wasanii hao kulingana na mikataba yao.
Nandy ni miongoni mwa wasanii wenye nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao, kitu kinachofanya nyimbo zake kupata idadi kubwa ya wasikilizaji, jambo ambalo ni wazi pia analitarajia katika albamu hiyo ambayo imezungumziwa kwa miaka kadhaa sasa.
Hata hivyo, kuna mambo mengi yamejiri katika muziki wa Nandy tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) hadi sasa anapoelekea kuachia ya pili, 911 (2026). Mambo hayo ni kama ifuatavyo;.
Mosi, EP tatu: Ingawa hakutoa albamu, bado Nandy aliweza kuwapatia mashabiki wake kifurushi cha burudani kupitia Extended Playlist (EP) tatu alizoachia ambazo kila moja ilifanya vizuri kwa kiasi chake kwani kila moja ilikuwa na wimbo mmoja au nyimbo mbili zilizopelewa vizuri zaidi.
EP hizo ni Maturity (2022), Taste (2021) na Wanibariki (2021) yenye muziki wa Injili pekee. EP yake ya Injili (Wanibariki), ilikuja kukumbushia kile alichofanya katika cover ya wimbo wa Angel Benard, Nikumbushe (2018), mradi ulioshinda Maranatha Awards 2018, tuzo zinazotolewa Kenya.
Pili, tuzo nne za TMA: Licha ya albamu yake ya kwanza kufanya vizuri, haikuishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa sababu wakati huo hazikufanyika, zilikuwa zimesimama tangu 2015.
Hata ziliporejea mwaka 2023 na 2023 na Nandy alishinda tuzo nne kwa jumla, hakushinda wala kuwania kipengele cha Albamu Bora kwa sababu hakuwa nayo. Iwapo tuzo hizo zitafanyika mwakani, kwa ukubwa wa kazi yake anaweza kupata nafasi upande wa albamu bora
Tatu, ndoa na Billnass: 911 itakuwa ni albamu ya kwanza kwa Nandy akiwa ndani ya ndoa yake na mwanamuziki mwenzake, Billnass ambaye wameshirikiana katika nyimbo takribani saba hadi sasa.
Katika albamu ya kwanza Billnass hakushirikishwa na ilikuwa kabla ya kolabo yao yoyote ile, lakini ni vigumu sana albamu hii ijayo yake itoke bila kuwepo kolabo na Billnass, ambaye hivi karibuni amefikisha streams milioni 100 Boomplay Music bila kuwa na albamu wala EP.