Kauli ‘nisipotoa wimbo, Bongo Fleva inayumba’ ya Marioo inafikirisha
Muktasari:
- Alipowasili uwanja wa ndege Marioo alizungumza kuwa “Nisipotoa wimbo, Bongo Flava inayumba, game imepoa.”
MWANAMUZIKI OMARY Mwanga maarufu ‘Marioo’ amerejea nchini akitokea Marekani, alikokwenda kwa shughuli za muziki, akiwa na tuzo yake ya AFRIMMA aliyoshinda katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki.
Alipowasili uwanja wa ndege Marioo alizungumza kuwa “Nisipotoa wimbo, Bongo Flava inayumba, game imepoa.”
Kauli hiyo imeacha swali je, kweli muziki wa Tanzania unafika pabaya Marioo anapokuwa kimya?
Marioo aliibuka mshindi wa Best Male East Africa katika AFRIMMA 2026 iliyofanyika Dallas, Marekani, akiwabwaga baadhi ya majina makubwa ya Afrika Mashariki, akiwamo Diamond Platnumz, Juma Jux, Mbosso, Barnaba na Bien.
Ushindi huo unaongeza uzito kwenye jina lake, lakini sasa ni wakati wa kupima kauli yake kwa kuangalia hali halisi ya Bongo Flava katika kipindi hiki.
SEPTEMBA KIMYA
Chati za muziki Tanzania katika kipindi hiki, kuanzia Septemba hadi sasa hazijaonyesha dalili ya kupoa kwani wasanii wakubwa na wadogo wameendelea kutoa kazi mpya kwa ushindani mkubwa.
Harmonize ndiye aliyeanza kutikisa mwezi huo, Septemba 4, alipoachia albamu yake ‘31’, iliyowakutanisha mastaa mbalimbali akiwamo Rayvanny na Jay Melody.
Baadaye, Diamond Platnumz aliungana na msanii wa Injili Joel Lwaga kwenye wimbo ‘Nikumbuke’ uliotoka Septemba 26.
Septemba 30, Zuchu naye aliachia wimbo wa ‘Unajua Kucheza’ wimbo wenye ladha ya singeli, hivyo ni wazi Septemba gemu iliendelea kusonga bila yeye.
HII SIO MARA YA KWANZA
Hii si mara ya kwanza kwa Marioo kujiamini kiasi cha kuhoji uamuzi unaomuhusu kwani hata tuzo za TMA 2022, albamu yake The Kid You Know ilikuwa kwenye kinyang’anyiro cha Albamu Bora ya Mwaka, lakini tuzo ikaenda kwa Love Sounds Different ya Barnaba.
Uamuzi huo Marioo hakukubaliana nao, kwani aliamini kazi yake ilikuwa na nguvu zaidi na ilistahili kutwaa tuzo hiyo, alizungumza baada ya matokeo hayo na kusisitiza msimamo wake.
“Kwa upande wangu, naamini The Kid You Know ndiyo ilikuwa albamu bora, kwa sababu nimefanya kazi kubwa na nimeweka kila kitu ndani yake.” alisema Marioo
Kauli hiyo ilizua mjadala kwa mashabiki wa muziki, huku kila upande ukiwa na hoja yake kuhusu nani alistahili tuzo hiyo. Lakini kwa Marioo, hilo lilikuwa somo la kuendelea kuamini kazi yake.
Kwa kuangalia kilichotokea kuanzia Septemba hadi sasa, ni vigumu kusema Bongo Flava imepoa kwa sababu Marioo hakuwa akitoa wimbo. Harmonize, Diamond, Zuchu na wengine wameendelea kutoa kazi na kulifanya soko liendelee kuwa na ushindani.