Ndani ya Boksi: Kwenye kolabo ya Lwaga na Mondi mnataka nini?
Muktasari:
- Haikuwa dhamira yangu kukaa. Nguvu ya shetani au mipango ya Mola? Sijui! Nikajikuta nipo pale na kuteketeza laki nzima ndani ya muda mfupi. Mchana nilikuwa Kariakoo. Uchovu wa misele, joto na kelele za kule zilinichosha. Kariakoo inakera sana.
Nipo eneo tulivu. Huduma ni bora na wahudumu wake ni warembo sana. Wanavutia kuwatazama hata uchungu wa pombe yangu sikuusikia mpaka namaliza. Nipo mkoani Dar es Salaam, wilaya ya Kinondoni, kitongoji cha Sinza.
Haikuwa dhamira yangu kukaa. Nguvu ya shetani au mipango ya Mola? Sijui! Nikajikuta nipo pale na kuteketeza laki nzima ndani ya muda mfupi. Mchana nilikuwa Kariakoo. Uchovu wa misele, joto na kelele za kule zilinichosha. Kariakoo inakera sana.
Kimsingi safari ya Goba ilikufa. Ni eneo tamanishi kuweka pozi, na wahudumu na huduma bora. Anza na mavazi kabla ya shepu zao na ukarimu. Doh! Mwenye namba ya Wakili Katuga anipatie niwafungulie kesi mbichi niwadai hawa kenge maji.
Jamaa ni wapotoshaji wa jamii wa wazi kabisa. Wanachofanya ni kuzifanya familia zetu ziishi kwa shida sana. Mazingira yake yanafanya umsahau mke, watoto na mama mzazi. Uwezo wao wa kurubuni ni zaidi ya makanisa ya wokovu.
Wakati kwa wafukuza mapepo ni sadaka, maji na mafuta. Pale ni mwendo wa ununuzi wa bierre, nyama na ‘tipu’ kwa wahudumu. Usipolewa tungi utaleweshwa na mbwembwe za wahudumu. Eneo hili kila kitu ni kilevi na utalewa tu, utake usitake.
Kando yangu kulikuwa na ‘totozi’ kadhaa. Kwa maongezi na aina ya mavazi ni wazi ni ‘jinzedi’. Ni wale ‘bintizi’ ambao ukiwasalimia hawaitikii kwa sauti wanainua tu kope zao. Wanamuita ‘anko’ kila mwanaume hata kama ana mvi kama Askofu Desmund Tutu.
Kadiri pombe ilivyozidi kuchukua utawala wake ‘hedini’. Nikaanza kuwaona kama watu wazima na wanaofaa kunihudumia kizinzi. Lishetani la uasherati likaanza kupiga jeramba. Likisubiri tu ubongo ufanye kazi ya Arajiga na kuruhusu boli lianze.
Hata wao walishachangamka na kusahau tumbo langu. Kusahau kipara changu. Hawakujali tena mvi zangu wala pozi zangu za kishua. Wakaanza kunisemesha kama mi ndo Marioo au Mbosso Khan. Nikaanza kulala ubavu kila dakika na kusambaza ofa.
Nikagawa sana bierre na nyama choma kwa wale viumbe. Pombe ni kitu cha kibwege, unavyolewa ndipo ujasiri wa “Kesho nitapata pesa nyingi zaidi”, unaongezeka. Nikawa kama mazao yaliyoliwa na nzege, jinsi walivyonipukuta wale mbwa wa kike.
Mabinti wa kizazi hiki. Ambao ni wadogo zake na Paula wa Kajala, Tunda wa Afande Sele na Lissa wa Prof. Jay. Wengi wao walevi wa pombe ama bange. Hawajui kutafakari au kuwaza ya kesho. Wao ni leo leo, hayo ya kesho ni udwanzi kwao.
Wa kiume ambao ni wadogo wa Aslay, Pateni au masela zake na Krish wa Uwoya, Collins wa Levy ambao ni kaka zake na Sasha wa Sugu. Hawa wengi wao hawajui mila na desturi za makabila yao wala Utanzania. Hao wameikuta Tanzania kiganjani kwao.
Wanapajua AirPort, Coco Beach na Mlimani City tu. Hawajui kama kuna kabila zaidi ya 120, wao ni kiingereza na kiswahili. Kihehe na Kimanyema kwao ni mambo ya ajabu. Jina la Nyerere hawajui linaandikwaje achana na Chifu Mkwawa au Mtemi Isike.
Kizazi siyo cha Juma na Roza. Kuna majina yalitoweka kwenye kizazi hiki. Ni ngumu mzazi wa sasa kumpa mtoto jina la Abedi, Zebedayo, Zakayo, Rajabu, Said au Seleman kama siyo Ismaili. Haya majina mwisho illikuwa miaka ya 80 kutoa kwa watoto.
Kama ulidhani watoto wa sasa hawaeleweki. Nenda RITA soma majina ya watoto. Utadhani ni watoto wenye asili ya Uingereza au Qatar. Ni Bryan, Aliyah, Nicole, Toya, Samir, Mahlez, Al Riyan,Nassr au Saiya. Juma au Lazaro kwao ni ubwege.
Haya majina huyakuti kliniki ama shuleni. Kama Samson, Andrew, Solomon, Abdul, Mohammed, Zaituni, Sharifa, Fatuma, Bakari, Hassan, Benjamini, Twaha ama Joseph. Majina ya wakati huu ni majina yanayofanana na movie za Hollywood au wachezaji wa Saudi Pro Ligi.
Watoto hawa hata ndoto nyevu hawaoti, wao huona ‘laivu’ kitaa au kwa simu. Ngumu kuwakuta na chunusi au alama ya ndui begani ni ‘Watizedi nyu modeli’. Stori za Deborah Mwenda sijui Mama na Mwana kwao ni kituko. Utawakata!
Wengi hulelewa upande mmoja wa mzazi. Hawajui mdako wala komborela, ukuti ukuti achana na sarakasi. Sijui hata kama balehe zao ni kama za nyakati zile. Na unaweza kudhani ubakaji kwa sasa umedhibitiwa kumbe kuna shida ya vitendea kazi.
Kwa namna hii wanapokutana Diamond na Lwaga. Wakatoa pini kama lile walilotoa. Halafu kuna mtu anatolea kavimba macho na shingo, anaponda. Eti sijui kuna mdhambi ndani yake. Naumia sana. Badala kuwapongeza wale madogo, vilaza wanaponda.
Hawa ngisi wanajua kilichopo huku mitaani? Hawajui kama uwepo wa Mondi ndani ya lile pini ni chambo ya ndoano ya kunasa samaki wengi walioko upande wa pili? Nyie ndugu zetu mnataka mkutane, mle na kuzagamuana wenyewe kwa wenyewe?
Kizazi cha ‘singo maza’ wengi kuliko mchanga. Bachela wengi wa kuliko nyasi. Nyimbo au upako wa Lwaga na Mondi unahitajika haraka kuliko Katiba Mpya. Mondi akiimba kidunia mnaponda, akiimba kimbunguni, mnaponda.
Mnataka nini?