Kama ulikuwa hujui, huyu ndo Uchebe sasa
Muktasari:
Sasa Uchebe ambaye ni fundi wa magari aliyepata umaarufu kutokana na uhusiano wake huo na Shilole na kutengeneza magari ya baadhi ya wasanii, amefunguka ukweli wa kinachoendelea katika maisha yake na hasa madai ya siku nyingi, hajui kusoma na kuandika.
UNAMKUMBUKA Ashraf Uchebe, aliyekuwa mume msanii na mjasiriamali maarufu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’.
Sasa Uchebe ambaye ni fundi wa magari aliyepata umaarufu kutokana na uhusiano wake huo na Shilole na kutengeneza magari ya baadhi ya wasanii, amefunguka ukweli wa kinachoendelea katika maisha yake na hasa madai ya siku nyingi, hajui kusoma na kuandika.
Mbali na madai hayo, pia amezungumzia kazi yake na wasanii na kusisitiza umaarufu wake hautokani tu kufanya nao kazi bali ni umakini alionao katika majukumu yake hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, ikiwa ni muda mrefu kupita tangu azushiwe hajui kusoma na kuandika, Uchebe alisema kwa aliyesambaza uvumi huo huenda kwa sasa anajutia alichokisema kwani sio kweli na ni wazi alionge akiwa ana hasira.
“Nilivyosikia habari hizo wala sikupatwa na hasira kutokana na mtu aliyeongea maneno hayo, ndiyo maana huwa tunaambiwa tukiwa na hasira tusijaribu kuongeaongea maana tunaweza kuongea vitu na baadae ikaja kuwa majuto.”
“Hivi unavyoniona hapa, naweza kweli kutojua kusoma au kuandika? Mimi nimesoma, nimeishia kidato cha pili kutokana na changamoto za maisha, nikaingia ufundi magari. Nimepambana hadi kufikia hapa nilipo na uzuri hii kazi ya gereji nilikuwa naipenda tangu nikiwa mdogo,” alisema.
Madai hayo aliyasema Shilole akihojiwa na moja ya vyombo vya habari baada ya ndoa yao kuvunjika na zaidi aliandika hadi katika ukurasa wake wa Instagram.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliamini hivyo kutokana na kuona kwenye ukurasa wa Instagram wa Uchebe akiweka picha pekee bila kuandika chochote au huandika tu ‘Say ayeyee’.
Kuhusu umaarufu wake kutokana na wasanii, alisema amekuwa akitengeneza magari ya watu mbalimbali maarufu na wasio maarufu na hata wanaokuja kutoka mikoani, kutokana na umakini kwenye kazi na bei nafuu anayowatajia na hivyo kumwamini.
Aidha alisema, changamoto ambazo huzipata katika kazi yake ni mtu kudharau kutokana na muonekano wake kutokana na kazi anayofanya ya ufundi gereji.
“Kuna mtu sitaki kumtaja jina niliwahi kumpigia simu kipindi hicho ndio naanza kutokatoka, kwa hiyo nikampigia simu kisha nikajitambulisha mimi fulani akanijibu kwa dharau sana, halafu kikapita kama kipindi fulani hivi hali yangu ikabadilika nikawa najulikana sana, nikakutana naye, alivyoniona akaona aibu kweli, yaani kiufupi hii ni changamoto sana, watu wanapaswa kuheshimu kazi ya mtu wasiweke dharau, hata kama napata 30000 au 10000 ni ya kwangu na siyo kudharau.”
Uchebe alisema kwa watu ambao hawamjui ni mtu tofauti sana, halafu naishi maisha yake maisha ambayo mwenyezi Mungu anataka niishi, pia napenda kuishi na watu vizuri.
“Mimi maisha yangu ni ya swala, mimi naswali swala tano, maisha ambayo Mungu anataka tuishi hivi, hili jina la Uchebe limetokana na mimi kupenda swala, nilikuwa na washikaji zangu ambao wanapenda mambo ya anasa kama uvutaji wa bangi, sigara, pombe, ilikuwa kila wakati nawaambia vitu wanavyofanya havipendezi na ilikuwa ikifika muda wa kuswali nawaacha naenda kuswali, basi wakaamua kunipa jina la Uchebe na huwezi kulikataa jina ndio limekuwa hadi leo,” alisema.
Uchebe alisema anaye mpenzi kwa sasa na ameshayasahau mahusiano yake yaliyopita.
“Nina mpenzi ambaye natarajia kufunga naye ndoa, kuhusu mahusiano ya zamani nimeshayasahau, mwishowe mimi ninafanya mazoezi ya mwili wangu na kutafuta pesa, mapenzi yapo tu, bali ninafanya kazi na ibada tu,” alisema
Mwanaspoti lilimuuliza Uchebe kuhusu kuelewana na Shilole hata kwa salamu tu, alisema haya :
“Sina tatizo na Shilole, mambo yaliyopita yameshapita kwa nini kuwa na kinyongo hadi leo?” alisema.
Ndoa ya Uchebe na Shilole imedumu kwa miaka miwili tu, walifunga Desemba 2017 na ilivunjika 2020. Na sababu ya kuvunjika ni Shilole alichodai alikuwa akipigwa na kuteswa sana katika ndoa yake.