Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Juma Jux: Maisha ya kimuziki yalibadilikia hapa...!

JUX Pict

Muktasari:

  • Enjoy ulikuwa wimbo wa pili kwa Jux kumshirikisha Diamond baada ya hapo awali kuachia, Sugua (2019), ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la The Love Album.

Mafanikio makubwa ya Jux kimuziki hasa upande wa kimataifa, yalianza kuonekana mara baada ya kuachia kolabo yake na Diamond Platnumz, Enjoy (2023) ambayo ilitayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic.

Enjoy ulikuwa wimbo wa pili kwa Jux kumshirikisha Diamond baada ya hapo awali kuachia, Sugua (2019), ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la The Love Album.

Hadi kufikia sasa, ni wazi Enjoy ni miongoni mwa nyimbo za Bongo Fleva zilizofanya vizuri Tanzania na Afrika kwa jumla zikiwa na namba za juu katika mitandao ya kusikikia muziki kama Spotify, YouTube Music, Boomplay n.k.

Wimbo wa Enjoy unahamasisha watu kufurahia maisha na mambo mengine mazuri yaliyomo ndani yake.

JU 04

Ujumbe wake unaweka wazi ugumu wa kumpa mpenzi sahihi, jambo ambalo mara nyingi husababisha maumivu na kukata tamaa.

Kutokana na hali hiyo, Jux anaamua kupumzika kwa muda masuala ya mahusiano na badala yake anajikita katika kufurahia maisha, akiamini maisha ni mafupi sana na yanapaswa kufurahiwa.

Ni wimbo uliobamba sana, ulishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2023, lakini Jux alidai ulipaswa kuwania vingi zaidi na sio hicho kimoja tu ambacho ulipewa nafasi katika TMA.

Kwa mujibu ujumbe alioutoa Jux kupitia Instagram, alieleza kuwa wimbo huo ulistahilishi kuwania vipengele vya Video Bora, Wimbo Bora wa Bongofleva, Msanii Bora wa Bongo Fleva, Msanii Bora wa Kiume, Mtunzi Bora na Mtumbuizaji Bora.

Video ya wimbo huo iliyoongozwa na Director Fole X, ilifanya vizuri muda mfupi baada ya kuachiwa kwake na ndani ya miezi mitatu tu tayari ilikuwa imeshatazamwa (views) katika mtandao wa YouTube zaidi ya mara milioni 40.

JU 01

Huu ulikuwa ni wimbo wa kwanza wa Jux kufanya hivyo, na pili katika Bongo Fleva kwa jumla baada ya ule na Diamond, Waah! (2020) aliomshirikisha mkongwe wa muziki kutokea DR Congo, Koffi Olomide.

Kufikia Oktoba 2024, video ya wimbo huo iliweka rekodi ya kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikiwa ni video ya kwanza ya Bongo Fleva kufanya hivyo ndani ya muda mfupi zaidi.

Ni video ya kwanza kwa Jux kufikia namba hizo ila ndani ya Bongo Fleva ilikuwa ni video ya nane huku Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, akiwa msanii wa nne kwa jumla kufanya hivyo.

Hadi sasa Diamond ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube. Anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020), Nana (2015), na African Beauty (2018).

JU 04

Katika orodha ya nyimbo za Bongo Fleva zilizofanya vizuri zaidi YouTube kwa muda wote, Enjoy inakamata nafsi ya tatu na imeshatazamwa mara milioni 182, huku ikiwa imetanguliwa na nyimbo mbili za Diamond ambazo ni Yope Remix na Waah!.

Nyimbo za Bongofleva ambazo sasa zimetazamwa zaidi mara milioni 100 YouTube ambazo zilitangulia kutoka lakini sasa zimezidiwa namba na Enjoy, ni Kwangwaru (Harmonize), Sukari & Kwikwi (Zuchu), Tetema & Number One (Rayvanny), pamoja na hizo za Diamond.

Kwa sehemu kubwa, wimbo wa Enjoy ulichangia Jux kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 1 YouTube akiwa ni msanii wa 11 wa Bongo Fleva kufanya hivyo baada ya Diamond, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Alikiba, Lava Lava, Nandy, Marioo na Aslay.

Kuanzia hapo Jux hakuwa tena yule wa miaka ya nyuma, safari yake kimuziki ilichukua sura nyingine akijiweka kama mwanamuziki wa kimataifa.

JU 03

Huko kimataifa ameshinda tuzo mbalimbali ikiwemo African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026 na alitakata kipengele cha Muziki Uliovuka Mipaka.

Uhusiano wake na Priscilla kutokea Nigeria ambao ulianza mwaka uliofuatia baada ya kuachia wimbo wa Enjoy, ulizidi kuongeza ushawishi wa muziki wa Jux barani Afrika. Hadi sasa Prisiclla ameonekana katika video saba za nyimbo za Jux, akiwa ndiye mrembo pekee mwenye rekodi hiyo.

Ikumbukwe Jux alianza muziki katika kundi la Wakacha liloanzishwa mwaka 2008, nyimbo zao zilizofanya vizuri ni Facebook Gail na Here We Go. Msanii mwenzake wa kundi hilo, Cyrill ndiye alimshauri kuachana na Rap badala yake aanze kuimba.

Anakiri kwa kiasi fulani alishawishika kimuziki na Trey Songz ambaye alianza kumfuatilia tangu alipoachia albamu yake, Ready (2009), lakini kwa asilimia kubwa alivutia na namna anavyojiweka kimuonekano, hivyo mikato mingi ya mavazi amejifunza kwake.