JASON STATHAM: Filamu zinavyomfanya aishi anavyotaka
Muktasari:
- Tangu mwishoni mwa miaka ya 1990 alianza kuigiza na filamu yake ya kwanza ni Lock, Stock and Two Smoking Barrels ya mwaka 1998, alivyoanza kupata heshima kutokana na mtiririko wa filamu zake hasa akionyesha ufundi wa mapigano dhidi ya maadui, jina lake limekuwa halisahauliki na kila akitoa filamu mpya, basi mashabiki na wapenda movie watataka kujua kaja na chuma kipi kipya.
LONDON, ENGLAND: KUTOKA 'Transporter' hadi 'Working Man', kama hujatazama filamu za mkali wa mapigano Jason Statham basi umekosa mengi.
Tangu mwishoni mwa miaka ya 1990 alianza kuigiza na filamu yake ya kwanza ni Lock, Stock and Two Smoking Barrels ya mwaka 1998, alivyoanza kupata heshima kutokana na mtiririko wa filamu zake hasa akionyesha ufundi wa mapigano dhidi ya maadui, jina lake limekuwa halisahauliki na kila akitoa filamu mpya, basi mashabiki na wapenda movie watataka kujua kaja na chuma kipi kipya.
Statham ana movie mbalimbali kali na zaidi ya hizo mbili, kuna Bee Kepper iliyoteka hisia za wengi, Wrath of Man, The Mechanic, Homefront na nyingine nyingi, huku pia akiwa mmoja wa washiriki katika mfululizo wa filamu za The Expendables.
Kutokana na filamu zote hizo, nyota huyu ambaye ni raia wa England aliyezaliwa miaka 57 iliyopita, amejikusajia kijiji cha mashabiki huku pia mfuko wake ukiendelea kunona kwa kuingiza pesa nyingi.
Statham ni miongoni mwa wasanii wakongwe waigizaji wenye mafanikio makubwa kuanzia katika filamu na hata nje ya filamu na wenye utajiri mkubwa ambao umetokana na mapato ya filamu pamoja na madili mengine. Leo tumekusogezea hapa utajiri wake wote na namna anavyopiga pesa.
ANAPIGAJE PESA
Statham huingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia uigizaji. Kwa wastani, hupokea kati ya Dola 10 hadi Dola 20 milioni kwa kila filamu anayoigiza.
Movie ya Fast & Furious Presents: Hobbs & Shaw ya mwaka 2019 alilipwa takribani Dola 13 milioni, pia The Meg ya mwaka 2018 alipata takriban Dola 10 milioni
Mbali ya kuigiza pia amekuwa akitayarisha filamu mbalimbali ambazo kwa kawaida kila moja humpa zaidi ya Dola 10 milioni.
Mbali ya filamu, staa huyu anapata pesa kupitia mikataba ya udhamini aliyoingia na kampuni mbalimbali kubwa.
Kwa sasa huyu ni balozi wa LG (Smartphones), Audi na French Connection (mavazi) ambazo zoye kwa mwaka zinampa zaidi ya Dola 10 milioni kijumla.
Mbali ya pesa anazopata kupitia filamu na mikataba ya udhamini, staa huyu anaripotiwa kumiliki mijengo ambayo anapangisha.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, utajiri wake ulikadiriwa kufikia Dola 120 milioni.
MIJENGO
Ripoti zinaeleza ana nyumba tatu, mbili ziko Marekani na moja England.
Nyumba ya kwanza iliyopo Marekani ni ile ya Malibu, California yenye thamani ya Dola 20 milioni, mjengo huu uliopo karibu na bahari una vyumba vitano vya kulala, bwawa la kuogelea, ukumbi wa sinema na gym binafsi.
Pia kuna mjengo mwingine upo Beverly Hills ambao thamani yake inadaiwa kufikia Dola 13 milioni na hii ndiyo muda mwingi huishi na familia yake.
Nyumba yake ya London ndiyo ya kwanza kabisa kuinunua na inadaiwa kuwa na thamani ya Dola 10 milioni.
NDINGA
Ferrari F12 Berlinetta -Dola 320,000
McLaren 720S -Dola 300,000
Audi R8 -Dola 200,000
Jaguar E-Type Series 1-Dola 150,000
Aston Martin DBS Volante -Dola 290,000
MSAADA KWA JAMII
Statham amekuwa akiunga mkono mashirika yanayopigania haki za binadamu, mazingira. Amewahi kuchangia pesa na kushiriki kwenye kampeni za Make-A-Wish Foundation, Help for Heroes (England).
Kwa jumla, mchango wake kwa taasisi hizi unakadiriwa kufikia zaidi ya Dola 2 milioni kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.
MAISHA NA BATA
Yupo kwenye ndoa na Rosie Huntington-Whiteley, ambaye ni mwanamitindo na mwigizaji maarufu.
Walianza uhusiano wao mwaka 2010 na walifunga ndoa rasmi mwaka 2016. Kwa sasa wana watoto wawili, wakwanza ni Jack Oscar Statham aliyezaliwa mwaka 2017 na wa pili alizaliwa mwaka 2022 lakini wameamua kutomweka mitandaoni.