Mose Iyobo kunogesha kilele cha Tamasha la Bagamoyo
Muktasari:
- Tamasha hilo lililoanza Oktoba 28, 2026, linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, 2026, likiwa na maonesho ya muziki, ngoma za asili, maigizo na sanaa nyingine za maonesho.
DANSA wa mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Mose Iyobo, anatarajiwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaopamba jukwaa la kufunga Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Oktoba 31, 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, Gabriel Kiiza, amesema siku ya mwisho ya tamasha hilo kutakuwa na wasanii wengi watakaotoa burudani, akiwamo Mose Iyobo na Vitali Maembe.
“Tutakuwa na wasanii wengi watakaotumbuiza siku ya mwisho ya tamasha, wakiwamo Mose Iyobo na Vitali Maembe,” amesema Kiiza.
Mose anatarajiwa kupanda jukwaani akiambatana na kundi lake la Iyobo’s Family, akileta burudani ya dansi. Umaarufu wake umetokana na umahiri wake wa kucheza dansi akiwa sehemu ya timu ya burudani ya Diamond Platnumz.
Mbali na wawili hao, wasanii na makundi mengine yanayotarajiwa kutumbuiza ni Gifted Muneka kutoka Zambia, Ras Gwandumi na Bongo Roots, Sauti Marley and The Band, Siza Segere Stars na Watupamawe.
Tamasha hilo lililoanza Oktoba 28, 2026, linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, 2026, likiwa na maonesho ya muziki, ngoma za asili, maigizo na sanaa nyingine za maonesho.