Hapa Zuchu ameshuka, Tyla amepanda!
Muktasari:
- Tunaliona hilo baada ya hivi karibuni Zuchu kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 5 katika mtandao wa YouTube akiwa ni mwanamuziki wa tatu wa kike kutokea Afrika kufanya hivyo.
MSHINDI wa Grammy mara mbili, Tyla, 24, anaendelea kuweka rekodi mbalimbali kubwa katika soko la muziki Afrika huku staa wa Bongofleva, Zuchu, 32, akizidi kupoteza rekodi zake mbele ya Tyla!.
Tunaliona hilo baada ya hivi karibuni Zuchu kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 5 katika mtandao wa YouTube akiwa ni mwanamuziki wa tatu wa kike kutokea Afrika kufanya hivyo.
Zuchu aliyevuma zaidi Afrika kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Sukari (2021), katika eneo hilo ametanguliwa na mwimbaji wa Misri, Sherine, na Tyla kutokea Afrika Kusini.
Kwa wengi wameichukulia kama rekodi kubwa kwa Zuchu, lakini kwa upande wa pili, inaonyesha kuwa mwanamuziki huyu ameshuka kutoka nafasi ya pili aliyokuwepo mwanzo hadi nafasi ya tatu baada ya kupitwa na Tyla.
Awali, Zuchu alikuwa ni mwanamuziki wa pili wa kike Afrika kwa kuwa na wafuatiliaji wengi YouTube nyuma ya Sherine, huku akiwa namba moja kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hata hivyo, baada ya ujio wa Tyla, Zuchu amepoteza rekodi zote mbili, kwa sasa zipo mikoni mwa Tyla ambaye kwa mara ya kwanza alivuma Afrika na duniani kwa ujumla kupitia wimbo wake, Water (2023) ulioshinda tuzo ya Grammy.
Lebo ya WCB Wasafi katika post yao ya kumtangaza Zuchu na kumpongeza kwa kufikisha wafuatiliaji milioni 5 YouTube, wamesema ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufanya hivyo!.
Hata hivyo, hapo awali walikuwa wakimpongeza Zuchu kama mwanamuziki wa kwanza wa kike Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini kwa sasa ameshuka hadi Afrika Mashariki baada ya Tyla kumpika.
Kwa sasa Tyla ana wafuatiliaji milioni 6.1 YouTube, huku Sherine akiwa na milioni 6.5, hivyo muda si mrefu Tyla anaenda kuwa namba moja Afrika pia. Hivyo rekodi kubwa za Zuchu YouTube, zinaendelea kusalia ndani ya Afrika Mashariki.
Hadi mwanzoni mwa 2023, ulikuwa huoni jina la Tyla katika muziki wa Afrika kwa ukubwa huo ukilinganisha na Zuchu ambaye tayari alishafanya vizuri na kolabo zake mbili na Diamond Platnumz, Cheche (2020) na Litawachoma (2020).
Tayari Zuchu alishafunika na wimbo wake, Sukari (2021) ambao video yake iliongozwa Afrika kwa kutazamwa YouTube mwaka huo, ukiuzidi hata ule wa Wizkid na Tems, Essence (2021) uliokuja kushinda tuzo ya BET.
Ukubwa wa Zuchu wakati huo ulipelekea kuchaguliwa kuwania tuzo za MTV EMAs 2022 zilizofanyika Duesseldorf, Ujerumani, ambapo alitajwa kipengele cha Msanii Bora Afrika, akiwa ni msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kuwania.
Aliendelea na moto huo hadi kuja kuweka rekodi kama mwanamuziki wa kike mwenye wafuatiliaji wengi YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwapita mastaa wakubwa kama Yemi Alade na Tiwa Savage, mshindi wa MTV EMAs 2018.
Cha kushangaza, kipindi Zuchu akifanya yote hayo, Tyla bado alikuwa akijitafuta, mathalani Desemba 2022, alikuja Tanzania kutambulisha kazi zake katika vyombo vya habari, kwa sababu alikuwa msanii mdogo ujio wake hakuzungumziwa sana.
Miezi saba baada ya kuondoka Tanzania, Tyla akaachia wimbo wake, Water (2023) uliofanya vizuri duniani ukiingia chati ya Billboard Hot 100 - akiwa ni msanii mdogo zaidi na wa pili Afrika Kusini kuingia katika chati hizo baada ya miaka 55.
Wimbo huo wa Amapiano, video yake ilifanya vizuri zaidi YouTube Afrika kwa mwaka 2023 ikitazamwa zaidi ya mara milioni 100 ndani ya miezi mitatu tu, huku ukifikisha streams (idadi ya kusikilizwa) bilioni 1 Spotify hapo Februari 2025.
Kubwa zaidi mafanikio ya wimbo huo yalipelekea Tyla kushinda tuzo kubwa kama Grammy 2024, MTV VMAs 2024, tuzo mbili za Billboard 2024, pamoja na tuzo mbili za BET 2024 akiwa msanii wa kwanza Afrika kufanya hivyo.
Alishinda tuzo tatu kwa mkupuo za MTV EMAs 2024 zilizofanyika Manchester, Uingereza. Hizi ndio zile alizowania Zuchu 2022 lakini akashindwa kufua dafu mbele ya Burna Boy aliyeibuka mshindi.
Kitendo cha Tyla kufikisha tuzo tatu za MTV EMAs, kilimfanya kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kushinda idadi hiyo ya tuzo kwa msimu mmoja, huku akiwa Mwafrika wa kwanza kushinda kipengele cha Best R&B.
Tyla ambaye ni msanii wa kwanza Afrika kushinda tuzo mbili za Grammy katika kipengele cha Best African Music Performance, ujio wake na mafanikio yake si tu yametikisa rekodi za Zuchu, bali na wanamuziki wengi Afrika waliomtangulia kama Davido, Diamond, Burna Boy, Wizkid na kadhalika.