Haji Manara afichua ukweli wa ndoa zake
Muktasari:
- Manara ambaye ameoa zaidi ya mara tatu, alisema kilichomkuta katika mahusiano yake ya nyuma hasa na wanawake maarufu na wa mitandaoni hataki kijirudie na anataka asiyefahamika katika jamii ili kuepuka usumbufu ambao anaweza kuupata endapo atakubali kuolewa na mwanamume maarufu.
MWANACHAMA wa Yanga, Haji Manara amesema ndoa zake zote alizowahi kuoa zilikuwa za ujanja ujanja tu na sasa ana mpango wa kuoa tena, lakini si mwanamke maarufu na anayependa mitandao ya kijamii.
Manara ambaye ameoa zaidi ya mara tatu, alisema kilichomkuta katika mahusiano yake ya nyuma hasa na wanawake maarufu na wa mitandaoni hataki kijirudie na anataka asiyefahamika katika jamii ili kuepuka usumbufu ambao anaweza kuupata endapo atakubali kuolewa na mwanamume maarufu.
“Ndoa zangu zote zilikuwa hazina uhalisia wowote, zote ni ujanja ujanja tu,” alisema.
Kauli hiyo imezua gumzo mitandaoni, hasa kwa mashabiki wake waliokuwa wakiamini maisha ya Manara nje ya siasa na soka yalikuwa na utulivu wa kifamilia.
Alisema kuoa ama kuolewa ni jambo ambalo mtu anatakiwa kulifanya kwa umakini, ili kuepuka kuingia kwenye mtego ambao baadaye unaweza kuwa ni majuto kwake.
“Ninasema hivyo kwa sababu nimeshuhudia mambo ambayo yamenikuta kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu maarufu, ama wapenda mitandao ya kijamii hivyo sitaki tena,” alisema.
“Kwa sasa nikitaka kuoa, nitakuwa makini sana sitaki kukurupuka kuoa mtu maarufu ambaye nina uhakika ninaweza kujikuta kwenye matatizo,” alisema.
Manara aliwahi kufunga ndoa na wanawake kadhaa akiwemo Rubynah, Naheedah Rushaynah na ZayLissa.