Esma avunja ukimya baada ya Zuchu kujifungua
Muktasari:
- Katika ujumbe huo, Esma amesema sala ya siku hiyo ilikuwa ya kipekee kwa sababu alipata nafasi ya kumuombea mtoto mpya aliyezaliwa katika familia yao, akisisitiza kuwa mtoto huyo hana hatia yoyote na hastahili kubeba hisia au tofauti za watu wazima.
DADA wa msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Esma Platnumz, ameandika ujumbe wenye hisia kupitia ukurasa wake wa Instagram baada ya taarifa za Zuchu kujifungua mtoto wa kike.
Katika ujumbe huo, Esma amesema sala ya siku hiyo ilikuwa ya kipekee kwa sababu alipata nafasi ya kumuombea mtoto mpya aliyezaliwa katika familia yao, akisisitiza kuwa mtoto huyo hana hatia yoyote na hastahili kubeba hisia au tofauti za watu wazima.
Esma amesema haoni sababu ya kuendelea kuwa na kinyongo kwa mtoto asiye na hatia, akieleza kuwa dini ya Kiislamu inafundisha kusameheana na kuishi kwa upendo.
Mbali na hilo, Esma amekanusha madai yaliyokuwa yakisambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ana uadui na mama wa Zuchu, Khadija Kopa, akisisitiza kuwa ukweli ni kwamba hawana tofauti zozote.
Katika sehemu ya ujumbe wake, Esma ameandika: "Bismillah. Huwa nafanya swala kila siku ukifika muda huu lakini leo swala yangu imekuwa ya tofauti sana. Nimepata wasaa wa kumuombea malaika mpya kwenye familia yetu asiye na hatia yoyote. Nitakuwa natenda dhambi endapo nitamuwekea kinyongo."
Ameendelea kueleza kuwa, watu wamekuwa wakitengeneza taswira ya uhasama kati yake na Zuchu, jambo ambalo amesema si la kweli.
"Kwa akili ya kawaida watu walikuwa wanatengeneza uadui baina yangu na Mama Sanura (Zuchu), lakini ukweli ni kwamba sisi hatuna uadui wowote. Hakika dini yetu imetukataza kuacha kusameheana pale tunapokoseana, hasa ikiwa Allah tunamkosea na anatusamehe, sisi nani?"
Esma pia amemuelekea Zuchu moja kwa moja katika ujumbe wake, akifichua kuwa mume wake alimwonyesha ujumbe ambao Zuchu alimwandikia, jambo lililomgusa na kumfanya aamue kuondoa tofauti zozote zilizokuwa zikidaiwa kuwepo.
"Mama Sanura Naseeb (Sandra), mume wangu amenionyesha ujumbe ulionitumia. Kiukweli nimejisikia vibaya kweli. Tusiruhusu kufa bila kuongeleshana. Mimi ni Muislamu, sitakuwa natenda haki kama sitakusafishia nia. Umeshakuwa mama sasa hivi na mimi nimeshakuwa aunty, basi tuwalee watoto wetu katika misingi bora ya kidini na upendo."
Katika kuhitimisha ujumbe wake, Esma amemshukuru mume wake kwa hekima aliyoionyesha, akisema ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu sasa imetimia.
Ujumbe huo umeibua hisia mbalimbali miongoni mwa mashabiki, wengi wakiupongeza kwa kuhimiza msamaha, upendo na umoja wa familia wakati wa kuupokea mwanachama mpya wa familia ya Diamond Platnumz.