Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ESMA PLATNUMZ: Tusiwahukumu wanaume kwa usaliti, tujitathimini

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja wakati ambao maisha yake ya ndoa na mumewe Rashid Shaibu maarufu Jembe One yamekuwa yakizungumzwa sana kufuatia sakata la video iliyosambaa mtandaoni.

KAULI ya Esma Platnumz kuhusu wanawake kujitathmini badala ya kulaumu wanaume pekee katika masuala ya kuchepuka imezua mjadala mkubwa mitandaoni.

Kauli hiyo imekuja wakati ambao maisha yake ya ndoa na mumewe Rashid Shaibu maarufu Jembe One yamekuwa yakizungumzwa sana kufuatia sakata la video iliyosambaa mtandaoni.

Kutokana na uzoefu wake wa ndoa mbalimbali zilizowahi kuandikwa na vyombo tofauti vya habari ndani na nje ya Tanzania, Mwanaspoti imekaa naye katika mahojiano maalumu ya dakika tano ili kufahamu kwa undani mtazamo wake kuhusu mapenzi, ndoa, usaliti, msamaha na masomo aliyojifunza katika maisha yake.


MWANASPOTI: Kauli yako kuhusu wanawake kujitathmini kabla ya kulaumu wanaume imeibua mjadala mkubwa. Ulikuwa unamaanisha nini hasa?


ESMA PLATNUMZ: Nilimaanisha kwamba kwenye mahusiano si sahihi upande mmoja pekee kulaumiwa. Wakati mwingine ni muhimu kila mmoja kujiangalia na kuona amechangia nini kwenye changamoto zinazotokea.


MWANASPOTI: Wapo wanaosema kauli yako ilionekana kuwatetea wanaume wanaochepuka. Unalizungumziaje hilo?


ESMA: Hapana. Sikutetea usaliti. Usaliti ni kosa. Nilichosema ni kwamba kabla ya kutoa hukumu kwa mwingine, ni vyema pia kujitathmini kama kuna jambo la kuboresha upande wako.


MWANASPOTI: Kauli hiyo imekuja baada ya sakata lililokuhusisha wewe na mume wako. Je, kuna uhusiano wowote?


ESMA: Kila jambo linalotokea maishani linakufundisha kitu. Inawezekana uzoefu wangu umenifanya kuona mambo kwa mtazamo mpana zaidi kuliko zamani.


MWANASPOTI: Baada ya yaliyotokea, kwa nini uliamua kumsamehe mume wako?


ESMA: Msamaha ni sehemu ya maisha. Hakuna mwanadamu mkamilifu. Nilichofanya ni kuangalia mustakabali wa maisha yangu na kufanya uamuzi ambao niliona unanifaa.


MWANASPOTI: Je, kuomba radhi kwa mwanaume kunatosha kufuta kosa la usaliti?


ESMA: Inategemea mazingira. Kuomba radhi pekee haitoshi, lazima kuwe na mabadiliko ya kweli yanayoonekana kwa vitendo.


MWANASPOTI: Umeshawahi kupitia ndoa tofauti katika maisha yako. Ni somo gani kubwa ulilojifunza?


ESMA: Nimejifunza kwamba ndoa si sherehe wala picha nzuri mtandaoni. Ndoa ni uvumilivu, mawasiliano na kuheshimiana kila siku.


MWANASPOTI: Vyombo mbalimbali vya habari viliwahi kuandika kuhusu kuvunjika kwa ndoa yako na Yahya Msizwa mwaka 2020. Leo ukiangalia nyuma unaona nini?


ESMA PLATNUMZ: Naona ilikuwa sehemu ya safari yangu. Kila hatua ina mafunzo yake. Kuna mambo mengi nilijifunza kuhusu watu, mapenzi na maisha kwa ujumla.


MWANASPOTI: Pia kulikuwa na ndoa yako na Petit Man iliyovuta hisia za wengi. Je, bado mnawasiliana?


ESMA PLATNUMZ: Tunawasiliana kama wazazi kwa sababu tuna majukumu yanayotuhusu. Jambo muhimu ni kuhakikisha mtoto anapata malezi bora.


MWANASPOTI: Unadhani umaarufu wa familia yako unaathiri mahusiano yako?


ESMA PLATNUMZ: Kwa kiasi fulani ndiyo. Watu wengi wanafuatilia kila kinachotokea, hivyo hata jambo dogo linaweza kuwa habari kubwa.


MWANASPOTI: Je, ni vigumu kuishi maisha ya ndoa ukiwa mtu maarufu?


ESMA PLATNUMZ: Ni vigumu kwa sababu unakosa faragha. Wakati mwingine watu wanatoa maoni bila kujua ukweli wote.


MWANASPOTI: Kuna wakati uliwahi kusema ndoa si jambo la lazima tena maishani mwako. Leo bado una mtazamo huo?


ESMA PLATNUMZ: Maisha hubadilika na watu hubadilika. Kila hatua ina namna yake ya kufikiri. Kikubwa ni kutafuta amani ya moyo.


MWANASPOTI: Wanawake wengi wanakuona kama mtu mwenye uzoefu mkubwa wa maisha ya mahusiano. Unawashauri nini?


ESMA PLATNUMZ: Wasikimbilie maamuzi kwa hasira. Pia wasijidharau wala kujiona wakamilifu. Kila siku kuna jambo jipya la kujifunza.


MWANASPOTI: Kwa mtazamo wako, nini siri ya ndoa yenye mafanikio?


ESMA PLATNUMZ: Kumuweka Mungu mbele, kuwasiliana kwa uwazi, kuheshimiana na kujifunza kusamehe pale inapobidi.


MWANASPOTI: Mwisho, je, uzoefu wako ndio unaokupa ujasiri wa kuzungumza kuhusu mapenzi na ndoa?


ESMA PLATNUMZ: Kabisa. Nimepitia mengi kama mwanamke. Sijifanyi mkamilifu, lakini naamini uzoefu wangu unaweza kuwasaidia wengine kuona maisha kwa mtazamo tofauti.