Diddy kumbe alimkaanga Biggie kwa mafuta yake mwenyewe
Muktasari:
- Makala hiyo inaitwa Sean Combs: The Reckoning, imefichua mambo mengi sana ambayo hayakujulikana kabla, kuhusu uchafu wa P. Diddy.
JUMANNE ya Desemba 2 mwaka huu, mtandao wa Netflix uliachia makala ya kushtua kuhusu maisha ya gizani ya nyota aliyeko mikononi mwa sheria, Sean Combs au kwa jina la kisanii, P. Diddy.
Makala hiyo inaitwa Sean Combs: The Reckoning, imefichua mambo mengi sana ambayo hayakujulikana kabla, kuhusu uchafu wa P. Diddy.
Katika mambo yote yaliyofichuliwa, hakuna lililovunja nyoyo za watu hasa wa muziki kama ukatili dhidi ya mtu aliyeonekana kuwa ni rafiki yake wa karibu, Christopher Wallace maarufu kama Notoriuos B.I.G au Biggie Smalls.
Mkasa unaanzia wakati wa kilele cha ugomvi wa Pwani mbili kubwa za Marekani, Mashariki ikiongozwa Notorious B.I.G na Magharibi ikiongozwa na Tupac Shakur.
Mbaya zaidi ni P.Diddy alihusika kuwaua wote wawili, akianza na Tupac mwaka 1996 kisha Notorious mwaka 1997.
Kwa mujibu wa Kirk Burrowes, mtu ambaye alishirikiana na P.Diddy kuanzisha lebo ya Bad Boy, siyo tu P.Diddy alimuua Notorious, pia alitumia pesa za Notorious kuandaa mazishi ya gharama kubwa ambayo hayakuwahi kuonekana jijini New York.
Mbele ya vyombo vya habari, P.Diddy alijisifu atamzika mpendwa wake kwa gharama kubwa sana...lakini kumbe hiyo gharama ni pesa ya marehemu mwenyewe.
Watu wakamsifia sana P.Diddy kamheshimisha rafiki yake...lakini nyuma ya pazia kumbe yeye ndiye aliyemuua na akaenda benki kuchukua hela zake na kuzitumbua kwenye mazishi.
Notoriuos aliuawa Machi 9, 1997 (ikumbuke hii tarehe) huko Los Angeles California, ambako pia Tupac aliuawa miezi kadhaa iliyopita, Septemba 7, 1996.
Los Angeles ni Pwani ya Magharibi, kwa kina Tupac...Notorious na P.Diddy kwao ni New York, ambako ni Pwani ya Mashariki.
Baada ya kifo cha Tupac, kambi ya Mashariki ya kina Biggie na P.Diddy iliogopa kabisa kwenda Magharibi wakihofia usalama wao.
Lakini ghafla P.Diddy akamlazimisha Notorious waende kule...Notoriuos alikataa akisema anahofia usalama wake na alitaka kwenda kujificha Uingereza, lakini P.Diddy akamlazimisha waende Los Angeles.
Wakaenda na ndipo Notorious akauawa...kumbe P.Diddy alimpeleka Biggie kwenye kifo.
Kuhusika kwa P.Diddy kwenye mauaji ya Tupac na Notorious, siyo kitu kipya sana kwa sababu kilizungumzwa sana kama tetesi kwa miaka mingi tangu walipouawa.
Lakini makala ya 50 Cent imetoa taarifa za ndani ambazo ni za kushtua sana.
Muuaji wa Tupac, Keefe D alihojiwa na kusema waliendelea kubakia eneo la tukio hadi gari la wagonjwa lilipokuja...na P.Diddy akawapigia simu wakiwa hawapo, kuwapongeza...pata picha!
P.Diddy alimuajiri mtu mmoja wa kuitwa Clayton Howard kama mfanyakazi wa ngono. Yaani huyu jamaa kazi yake ni kuletwa wanawake afanye nao mapenzi huku P.Diddy anaangalia.
Huyu jamaa naye alitoa ushuhuda wa kushangaza sana.
Jamaa anasema kila ifikapo Machi 9 ya kila mwaka, Diddy alikuwa anamsafirisha yeye na mwanamke aliyeitwa Cassie Ventura, ambaye alikuwa mpenzi wa P.Diddy.
Wanakwenda sehemu ya mbali halafu Clayton anafanya mapenzi na Cassie P.Diddy akiangalia...na akizidiwa na yeye anakwenda kuuungana na Howard kufanya mapenzi na Cassie.
Kule juu nilisema ikumbuke tarehe ya kifo cha Biggie, yaani Machi 9...hapa ndipo mahala pake sasa.
Kwamba uchafu huu P.Diddy alikuwa anaufanya kila ikifika Machi 9 ya kila mwaka, tarehe ya kifo cha Biggie...yaani P.Diddy alikuwa anaikumbuka tarehe ya kifo cha rafiki yake wa karibu kwa kufanya dhambi hii?
Kwa kweli makala hii ya 50 Cent imefichua mambo makubwa sana.
Yaani P.Diddy alimuua rafiki yake...akatumia pesa zake kumuandalia mazishi ya gharama, halafu akaitumia siku yake ya kufa kufanya ushenzi uliopindukia.
Makala ya Sean Combs: The Reckoning imeandaliwa na 50 Cent, mtu ambaye pia ni mhanga wa P.Diddy.
Mwaka 2021, P.Diddy alitoka kimapenzi na Daphne Joy. Mwanamitindo ambaye ni mzazi mwenzake na 50 Cent...wana mtoto wa kiume anayeitwa Sire Jackson.
Hii ni kashfa nyingine ya P.Diddy katika maisha yake ya gizani. Amekuwa akipenda sana kutoka kimapenzi na waliokuwa wapenzi wa watu wake wa karibu.
Mwaka 2019 alitoka kimapenzi na mwanamke aliyeitwa Lori Harvey, ambaye alikuwa mpenzi wa mwanaye, Justin Combs...yaani P.Diddy alikuwa mroho kiasi cha kutembea na mpenzi wa mwanaye wa kumzaa.
Justin Combs ni mtoto wa P.Diddy aliyezaa na mwanamke mmoja anayeitwa Misa Hylton. Huyu mwanamke awali alikuwa mpenzi wa Erick Sermon, rapa wa kundi la EPMD.
P.Diddy alimuoa mwanamke wa kuitwa Kim Porter na alizaa naye watoto watatu. Lakini mwanamke huyu awali aliwa mpenzi wa rapa mwingine wa kuitwa Al B. Sure!
Rapa huyu jamaa alikuwa msanii katika lebo ya Uptown Records ambayo P.Diddy alianzia kufanya kazi...akampora jamaa!
Kule juu tuliona mkasa wa Cassie Ventura. Huyu mwanamke kabla hajawa mpenzi wa P.Diddy alikuwa mpenzi wa prodyuza aliyeitwa Ryan Leslie.
Prodyuza alimpeleka Cassie kwa P.Diddy ili asaidiwe kimuziki kwenye lebo yake ya Bad Boy...Diddy akampora.
Diddy alikuwa mchafu sana. Makala ya 50 Cent imefichua vitu vingi sana kuhusu P.Diddy.
Lakini katika yote...hili la mshikaji wake wa karibu Notoriuos B.I.G ni la kuhuzunisha sana. Alimkaanga kwa mafuta yake mwenyewe!