D Voice anavyoongoza singeli ikizidi kupaa
Muktasari:
- D Voice ni miongoni mwa watu wanao ongoza katika matumizi ya muziki wa Singeli mtandaoni, huku chaneli yake ya YouTube ikiwa imevuka milioni 200 za watazamaji. Takwimu za ufuatiliaji wa chaneli zinaonyesha zaidi ya milioni 201 za watazamaji katika video zake.
MSANII wa Singeli, Abdul Hamisi Mtambo maarufu kama D Voice, ameandika historia mpya katika muziki huo baada ya kufikisha zaidi ya watazamaji milioni 200 kwenye YouTube, inazidi kuonyesha nguvu ya Singeli ndani na nje ya Tanzania.
D Voice ni miongoni mwa watu wanao ongoza katika matumizi ya muziki wa Singeli mtandaoni, huku chaneli yake ya YouTube ikiwa imevuka milioni 200 za watazamaji. Takwimu za ufuatiliaji wa chaneli zinaonyesha zaidi ya milioni 201 za watazamaji katika video zake.
Hii si namba ndogo kwa msanii wa Singeli, kwani inaonyesha jinsi muziki huo ulivyoendelea kutoka kwenye mitaa ya Dar es Salaam na kuingia zaidi kwenye soko la kidijitali.
Kwa msanii aliyekulia Temeke, Dar es Salaam, mafanikio hayo ni hatua kubwa katika safari yake, hasa ukizingatia namna Singeli ilivyokuwa ikihusishwa zaidi na watu wahuni.
SAFARI YAKE WCB
D Voice alianza kupata jina kubwa kupitia Singeli kabla ya kuingia rasmi WCB Wasafi mwaka 2023. Tarehe 16 Novemba mwaka huo, Diamond Platnumz alimtambulisha kama msanii mpya wa lebo hiyo.
Siku iliyofuata, Novemba 17, 2023, D Voice akaachia albamu yake ya kwanza, Swahili Kid, ikiwa na nyimbo 10. Kwenye albamu hiyo alifanya kazi na Diamond Platnumz, Zuchu, Mbosso na Lava Lava.
Kazi hiyo ilionyesha kuwa D Voice si msanii anayefungwa na Singeli pekee, kwani alichanganya muziki huo na Bongo Fleva pamoja na Amapiano.
Miongoni mwa nyimbo zilizobeba albamu hiyo ni BamBam na Zuchu, Mpeni Taarifa na Mbosso, Nimezama, Turudiane na Lava Lava pamoja na Kama Wengine aliyoshirikiana na Diamond.
D VOICE AKIWA JUU, NANI ANAMFUATA?
Wakati D Voice akiongoza kwa kasi ya kidijitali, ushindani nyuma yake nao unazidi kuwa mkali.
Riphati Jumanne Omary Maarufu kama Msomali ni miongoni mwa majina yanayofanya vizuri na amekuwa akionekana mara kwa mara kwenye playlist za Singeli.
Anaendelea kutoa kazi mpya, huku mwaka huu akiwa na nyimbo kadhaa zikiwemo Yeye, Nitampeleka kwa Mama na Mtu Kazi Mtu Mapenzi.
Jina jingine kubwa ni Abdallah Ahmed maarufu kama Dulla Makabila, ambaye licha ya kuwa mkongwe katika Singeli bado anaendelea kutoa kazi zinazopata nafasi kwenye majukwaa ya muziki.
Dulla amekuwa na mwaka wenye shughuli, akitoa Kidonda akiwa na Jay Melody, pamoja na Madee na Dakika Moja. Ushindani wa Dulla na wasanii wa kizazi kipya unaonekana pia kwenye majukwaa ya kusikiliza muziki. Kwa mfano, Spotify imeiweka Kidonda ya Dulla na Jay Melody miongoni mwa nyimbo zilizo juu kwenye playlist yake ya Singeli Sounds.
SINGELI HAINA MWISHO
Mbali na D Voice, Msomali na Dulla, majina kama Dogo Paten, Balaa MC, Meja Kunta, Ibrah Malume maarufu kama Malume,na wengine yanaendelea kufanya Singeli ibaki na ushindani.
Kinachoonekana sasa ni kwamba Singeli haitegemei tena msanii mmoja. Kuna kizazi kinachopanda wakongwe wanaorudi na kazi mpya, huku majukwaa kama YouTube, Spotify na Audiomack yakitoa nafasi ya kupima nguvu ya kila msanii. Na hapo ndipo D Voice anapoonekana kuwa ameweka tofauti.
Kutoka Temeke, kuingia WCB, kutoa Swahili Kid na sasa kuvuka milioni 200 za YouTube, D Voice ameweka rekodi ambayo kizazi kinachomfuata kitalazimika kufanya kazi zaidi kuivunja.