D’Lila & Jessie: Pacha wa Diddy hawapoi wala hawaboi!
Muktasari:
- D’Lila na Jessie ni watoto wa pili katika uhusiano wa Diddy na aliyekuwa mpenzi wake, mwanamitindo Kim Porter ambaye alifariki dunia mwaka 2018. Wawili hawa waliachana tangu 2007 baada ya Kim kubaini usaliti wa Diddy.
Hadi anaenda gerezani, Sean ‘Diddy’ Combs alikuwa ana watoto sita aliowapata na wanawake wanne tofauti, kati yao ni mapacha, D’Lila na Jessie ambao wameanza kufuata nyayo za marehemu mama yao katika tasnia mitindo.
D’Lila na Jessie ni watoto wa pili katika uhusiano wa Diddy na aliyekuwa mpenzi wake, mwanamitindo Kim Porter ambaye alifariki dunia mwaka 2018. Wawili hawa waliachana tangu 2007 baada ya Kim kubaini usaliti wa Diddy.
Diddy, mwanzilishi wa Bad Boy Records, watoto wake sita ni Justin (32), Christian (28), Chance (19), pacha D’Lila na Jessie (19) na Love (3), huku akimuasili mtoto mmoja wa Kim Porter, Quincy (35).
Picha linaanza asubuhi ya Desemba 21, 2006, na Diddy anapata zawadi ya kufungia mwaka, nayo ni kuzaliwa kwa watoto wake pacha, D’Lila na Jessie, huku akiwa pembeni ya mama yao, Kim Porter.
Mtoto wa kwanza alizaliwa saa 1:56 asubuhi akiwa na uzito wa kilo 2.27, huku mtoto wa pili akizaliwa dakika mbili baadaye akiwa na uzito wa kilo 2.38. Diddy alifika hospitalini muda mfupi kabla ya kuzaliwa akitokea Canada alipokuwa akishuti filamu, Raisin in the Sun.
Diddy akitangaza kuzaliwa kwa watoto hao alitaja sababu ya kupewa majina hayo akisema yametoka kwa bibi zao. Jina la bibi yake Di d dy lilikuwa Jessie Smalls, huku bibi yake Kim Porter akiitwa Lila Star. Pacha hao walizaliwa ikiwa ni miezi mitano na siku moja tangu Diddy kupata mtoto mwingine na aliyekuwa mpenzi wake wa siri, Sarah Chapman ambaye alijifungua mtoto wa kike hapo Julai 20, 2006 na kumpa jina la Chance.
Baada ya kupata taarifa za kuzaliwa kwa Chance, Kim Porter alihisi Diddy alikuwa amemsaliti vibaya mno katika uhusiano wao wa muda mrefu, hivyo aliamua kuvunja kabisa uhusiano wake na mwanamuziki huyo wa rap.
Katika taarifa yake hapo Julai 2007, Kim Porter alisema alichukua uamuzi huo kwa kuzingatia masilahi yake na ya familia yao. Alieleza anasonga mbele na maisha yake, huku akimtakia Diddy mafanikio, afya njema na furaha katika mahusiano yake mengine.
Hadi sasa huo ndio uhusiano wa Diddy uliodumu kwa muda mrefu zaidi, mtoto wao kwanza Christian ‘King Combs’ alizaliwa Aprili 1, 1998. Hata hivyo, waliachana mwaka mmoja baada kuzaliwa kwake lakini wakaja kurudiana na ndipo wakazaliwa mapacha hao, D’Lila na Jessie.
Kwa sasa mapacha hao wanafuata nyayo za mama yao, Kim Porter wakiwa tayari wameanzisha chapa yao ya mitindo inayoitwa 12TWINTY1, jina linalotokana na tarehe yao ya kuzaliwa, Desemba 21.
Katika mahojiano na V Magazine mnamo Mei 2023, ambapo walionekana pia ukurasa wa mbele pamoja na dada yao Chance, D’Lila na Jessie walieleza kuwa walikuwa na ndoto ya kuwa wanamitindo tangu wakiwa wadogo.
D’Lila alisema lilikuwa jambo la kuwavutia pale walipomuona mama yao akijaribu mavazi mbalimbali na kupiga picha za mitindo. Alieleza kuwa walikuwa wakimwangalia na kutambua kuwa uanamitindo ndio kazi wanayoipenda.
Mnamo Agosti 2021, mapacha hao pamoja na dada yao Chance walipanda jukwaani kuonyesha mavazi katika maonyesho ya mitindo ya Dolce & Gabbana Alta Moda yaliyofanyika Venice nchini Italia.
“Jamani, hii ni ndoto iliyotimia kweli! Tumefurahi sana kupata nafasi ya kutembea kwenye jukwaa la maonyesho ya mitindo ya Dolce & Gabbana,” waliandika mapacha hao kwenye Instagram.
Pia walishiriki maonyesho ya mitindo ya Liberty & Justice, na maonyesho ya kuadhimisha miaka 10 ya kampuni ya mavazi ya Ellae Lisque, huku akitokea ukurasa wa mbele katika majarida kama Fair na Essence, ambapo walipigwa picha pamoja na Chance na Diddy.
Desemba 2022, Jessie na D’Lila walisherehekea kutimiza miaka 16 ya kuzaliwa katika sherehe kubwa iliyoandaliwa na baba yao, Diddy ambaye aliwazawadia magari mawili aina ya Range Rover.
Mabinti hao ambao wanatumia akaunti moja Instagram, kila mara wamekuwa akieleza jinsi wanavyomkumbuka mama yao. Katika siku ya kina mama duniani mwaka 2023 na 2025, kupitia Insta Story waliandika ujumbe kwa ajili ya mama yao.
“Heri ya siku ya kina Mama. Mama tunakupenda sana na tunaendelea kukukumbuka kila wakati. Miaka hii michache iliyopita imekuwa migumu sana kwetu bila uwepo wako. Tutafuata nyayo zako na kuhakikisha kuwa tunakufanya ujivunie sisi,” walieleza.
Vilevile walihudhuria kesi ya baba yao, na wote wawili walitoa maelezo mbele ya mahakama. D’Lila alimuomba hakimu kutoa hukumu ya haki ambayo ingeisaidia familia yao kupona kutokana na maumivu waliyokuwa wakiyapitia.
“Mdogo wetu mwenye umri wa miaka miwili anauliza, ‘Baba yuko wapi?’ kama vile sisi tulivyokua bila mama. Hilo ni pengo ambalo haliwezi kuzibwa. Tumechoka mambo haya kila wakati, tayari tumepoteza mengi sana: mama yetu na baba yetu. Tafadhali, tupe nafasi ya kupona na kuendelea na maisha yetu pamoja,” alisema D’Lila
“Tunajua kwamba yeye si mkamilifu na amefanya makosa mengi, na hatupo hapa kutetea makosa hayo. Lakini, Mheshimiwa Hakimu, bado ni baba yetu na bado tunamuhitaji awepo katika maisha yetu,” alisema Jessie.
Baadaye Diddy alihukumiwa kifungo cha miezi 50 baada ya kukutwa na hatia katika makosa mawili yanayohusiana na kusafirisha binadamu kwa ajili ya biashara ya ngono.
Kwa sasa anatumikia kifungo katika gereza la Fort Dix, New Jersey, huku akitarajiwa kuachiwa huru mnamo Februari 2028, kwa mujibu wa taarifa za Bureau of Prisons.