Click Master anavyopita kiaina yake Bongofleva
Muktasari:
- Maprodyuza kama S2kizzy, Mocco Genius, Click Master, Genius Jini na wengineo ambao wanapiga kotekote yaani wanatengeneza muzki na kuimba pia.
MUZIKI wa Bongo Fleva umekuwa na mabadiliko makubwa kwa miaka ya hivi karibuni. Lakini kumezuka mtindo kwa watayarishaji wa muziki kushika maiki na kuimba.
Maprodyuza kama S2kizzy, Mocco Genius, Click Master, Genius Jini na wengineo ambao wanapiga kotekote yaani wanatengeneza muzki na kuimba pia.
Click Master ni mmoja wa maprodyuza wanaotamba kwa sasa na kutengeneza jina lake kiaina yake. Ameshafanya ngoma kama ‘Sherehe’, ‘Nilipe’, ‘Utukutu’ na ‘Mwizi’ ni miongoni mwa kazi zilizomfanya atambulike kwenye masikio na mioyo ya wapenzi wa burudani.
Ni kazi zilizothibitisha kuwa Click Master hana tu kipaji cha kutengeneza biti, bali pia anajua namna ya kucheza na sauti na mashairi.
NJIA YAKE
Katika tasnia ya Bongo Fleva, kuna mtindo au mfumo ambao umekuwa ukitumiwa na wasanii wengi wapya wanapoingia kwenye soko. Wasanii wengi waliopata mafanikio makubwa walianza safari zao kwa kutoa nyimbo za 'kulilia mapenzi' au nyimbo za majuto na maumivu ya moyo. Mtindo huu umethibitika kuwa njia ya kipekee ya kuteka hisia za mashabiki haraka sana.
Ukimwangalia msanii Zuchu kutoka lebo ya WCB Wasafi, alijitambulisha rasmi na kuingia kwenye masikio ya Watanzania na wimbo wake wa ‘Nisamehe’ uliotoka Mei 16, 2020. Wimbo huo ulijaa vilio, majuto na kuomba msamaha kwenye mapenzi, jambo lililowafanya mashabiki wamhurumie, na kumpokea kwa mikono miwili.
Vivyo hivyo kwa msanii Mac Voice ambaye alipopata nafasi ya kujitambulisha kwenye ulimwengu wa muziki Septemba 28, 2021 baada ya kusainiwa na lebo ya Next Level Music, alikuja na wimbo wa ‘Nenda’. Wimbo huo ulikuwa ni wa maumivu ya mapenzi.
Si hao tu hata D Voice ambaye kwa miaka mingi alikuwa akiimba nyimbo za singeli ni mmojawapo. Alipojiunga na lebo ya WCB na kutambulishwa Disemba 18, 2023, miongoni mwa ngoma zilizofanya vizuri kwenye EP yake Swahili ni ‘Umenifunza’. Wimbo huu nao ulibeba ujumbe wa maumivu ya kufunzwa adabu na mapenzi. Nyimbo hizi za kulilia mapenzi zimekuwa na nguvu kubwa ya kuunganisha msanii mpya na jamii kwa sababu mapenzi na maumivu ni vitu ambavyo karibu kila mtu anavipitia.
AMEKUJA KIVINGINE
Anapofanya kazi kama ‘Watajua’, anachanganya uzoefu wake wa kutengeneza midundo ya ngoma za jamii na uwezo wake wa kuimba kwa hisia. Hii inamfanya Click Master kuvuma kiaina yake na kuwa tofauti na waimbaji wengine wa kawaida.
Soko la muziki kwa sasa linahitaji wasanii wenye ubunifu na wanaoweza kubadilika kulingana na wakati. Click Master ameonyesha kuwa hana hofu ya kujaribu vitu vipya.
Kutoka kwenye ngoma za klabu kama ‘Sherehe’ hadi kwenye nyimbo za kutafakari maisha kama ‘Watajua’, safari yake inaonyesha wazi kuwa anajipanga kuwa mmoja wa wanamuziki tegemeo katika miaka ya mbele.
WATAJUA FUNZO LA KILA SIKU
Click Master anatamba na wimbo wake mpya uitwao ‘Watajua’. Huu si wimbo wa kawaida tu wa kucheza au kusikiliza unapokuwa kwenye klabu; ni wimbo unaobeba ujumbe mzito wa maisha ya kila siku na mahusiano ya binadamu.
Katika wimbo wa ‘Watajua’, Click Master anazungumzia maisha na mabadiliko yake. Anaeleza namna ambavyo alipoteza watu muhimu na vitu vya thamani katika maisha yake, lakini safari haikuishia hapo.
Kwenye moja ya mistari yake inasema "Nilipoteza watu ndo nikapata watu, Mungu na ulimwengu ulimpa watu wengine wapya na vitu vingine bora zaidi. Ni kazi inayigusa jamii moja kwa moja kwa sababu inabeba uhalisia ambao kila binadamu amepitia au anakutana nao katika maisha ya kila siku. Unapopoteza kitu leo, haimaanishi ndio mwisho wa maisha, bali ni fursa ya kupokea kitu kingine kipya.
Muziki unaogusa maisha ya kila siku ya jamii mara zote umekuwa ukidumu kwa muda mrefu kuliko muziki wa kupita tu.
MSIKIE DIAMOND PLATNUMZ
Mkurugenzi wa Wasafi, Diamond Platnumz "Utachagua wewe umzungumzie kwa uzuri au kwa ubaya lakini utamzungumzia amekuja na staili yake na namna yake na ndio maana watu wamempokea ameleta kitu tofauti angetaka aige kitu cha msanii fulani pengine watu wasingempokea," alisema msanii huyo June 24 mwaka huu kwenye uzinduzi wa Masterclass ya Zuchu
"Unafanya kazi nzuri sana Click, nami ni moja ya Shabiki zako, Mwenyez Mungu azidi Kukubariki na kukufungulia zaidi katika kazi na maisha yako."