Christopher Mwahangila: 'Tulimiss' matamasha ya Pasaka
Mkali wa wimbo wa 'Yesu yuko Hapa', Christopher Mwahangila, amesema walimiss tamasha la Pasaka huku akiahidi kuwapa watu burudani ya kutosha siku hiyo.
Mwahangila ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 22, 2023 alipokuwa akithibitisha uwepo wake kwenye tamasha hilo mbele ya waandishi wa habari, tamasha linalotarajiwa kufanyika Aprili 9 viwanja vya Leaders.
Mwimbaji huyo alisema tamasha hilo limekuwa pendwa kwa waimbaji wa Injili kwakuwa ni moja ya sehemu ambayo wanakutana na mashabiki zao kumtukuza Mungu na kumshukuru kwa mema aliyowafanyia.
"Ni miaka saba imepita sasa bila kufanyika tamasha hili hivyo waandaaji ambao ni Msama Promotion kulirudisha mwaka huu ni jambo la kushukuru Mungu" alisema Mwahangila
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kuwahakikishia ulinzi wa kutosha.
"Niwahakikishie kila mtu atakayekuja siku hiyo kutakuwa na ulinzi wa kutosha kuanzia yeye na chombo atakachotumia kuja nacho, hakuna atakayeondoka eneo hilo baada ya tamasha akiwa amefanywa lolote baya" amesisitiza Msama
Aidha Msama amesema waimbaji wengine bado wanendelea kuongezeka na kumtaja Mass Masilya wa nchini Congo kuwa tayari amethibitisha ujio wake wiki hii.
Wasanii wengine ambao tayari walithibitisha ni Joshua Ngoma wa nchini Rwanda, Tumaini Akilimali wa Kenya huku wa nyumbani Tanzania yupo Upendo Nkone, Zablon Singers, Ambwene Mwasongwe na Joshua Mlelwa.
Tamasha hilo kwa mwaka huu limekuja kitofauti kwani mbali na kuimba na kuabudu, pia litatumika katika kumuombea na kumpongeza Rais Samia kwa miaka miwili ya uongozi wake.