BONGO MUSIC FACTS: AY hajawahi kulipa fedha kurekodi kwa P-Funk Majani
Muktasari:
- Ametoa albamu zake mbili, Raha Kamili (2003) na Hisia Zangu (2005) pamoja na moja ya kushirikiana, Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na Mwana FA, huku akishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Channel O, Kisima Awards na kadhalika. Huyu ndiye AY.
LICHA ya kulala kwenye kontena Upanga na kuamkia kuoga mabafu ya jiji Mnanzi mmoja, bado AY aliamini ndoto yake ya kuwa mwanamuziki mkubwa itatimia na kweli ikawa hivyo hadi kuvuka mipaka ya Tanzania.
Ametoa albamu zake mbili, Raha Kamili (2003) na Hisia Zangu (2005) pamoja na moja ya kushirikiana, Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na Mwana FA, huku akishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Channel O, Kisima Awards na kadhalika. Huyu ndiye AY.
1. AY alikuja Dar es Salaam mwaka 1999 kwa lengo la kuanza muziki, pia alishawishiwa zaidi na rafiki yake, G Zingalize ambaye alikuwa anasoma naye Ifunda Technical School huko Iringa.
Sasa alipofika Dar alianza kuishi kwenye kontena Upanga kisha akahamia kwa kina G Zingalize na baadaye kwa King Crazy GK ambaye walikuja kufanya wote muziki kwenye kundi la East Coast Team.
2. AY ndiye msanii wa kwanza mkubwa Bongo kumshirikisha Vanessa Mdee ambaye alisikika katika wimbo wake ‘Money’, baada hapo ndipo Vanessa akatoa wimbo ‘Closer’ uliomuwezesha kushinda tuzo ya kwanza ya TMA 2013 kama wimbo Bora wa RnB.
3. Kwa mara ya kwanza AY ana Professor Jay walikuta wakati AY akienda ofisi za Hard Blasters Crew (HBC), Jay aliposikia sauti yake baada ya kutamba na wimbo ‘Ni Raha Tu’, akamwambie aende kwa P-Funk Majani akarekodi wimbo ‘Nawakilisha’ walioshirikiana.
Utakumbuka wimbo ‘Nawakilisha’ ulikutanisha wasanii watano ambao ni Black Rhino, Adili Chapakazi, Complex na AY aliyechana vesi ya mwisho.
4. Wakati AY na Maurice Kirya kutoka Uganda wanarekodi wimbo ‘Binadamu’, Maurice alikuwa hajui kabisa Kiswahili, hivyo AY ikabidi amwandike maneno yote ya Kiswahili aliyoimba katika wimbo huo.
5. Ziara (tour) ya kwanza AY kimuziki alipewa nafasi ya Professor Jay, ni katika ziara ya albamu yake ya kwanza, Machozi Jasho na Damu (2001), hapa ndipo AY alipozunguka sana nchi akiwa msanii wa kwanza kupanda jukwaani.
Na Profesa Jay ndiye alimpeleka AY Mombasa, Kenya kufanya shoo kwa mara ya kwanza, pia waliambatana na Chidi Benz ambaye alikuwa msaidizi wa Jay kwa wakati huo.
6. Ukaribu wa AY na Prezzo ulianzia kwenye simu ambapo walikuwa wanaongea mara kwa mara, mwisho wa siku Prezzo akamkaribisha AY kwao, Nairobi, Kenya ndipo wakarekodi wimbo ‘Nipe Nikupe’ uliojumuishwa katika abamu ya pili ya AY, Raha Kamili (2005).
7. Baada ya kurekodi wimbo huo (Nipe Nikupe) studio za Homeboyz Entertainment, AY akapewa nafasi ya kurekodi nyimbo zake mbili ambazo ni ‘Kimya Chako’ na ‘Inategemea na Mtu’ ambao aliuandika papo hapo studio.
8. AY ndiye msanii wa kwanza ambaye Ommy Dimpoz alitaka kumshirikisha ila hakufanikiwa, ndipo akampata Alikiba aliyesikika kwenye wimbo wake ‘Nai Nai’ uliomtoa kimuziki na kushinda tuzo ya TMA 2012 kama Msanii Bora Chipukizi.
9. Solo Thang ambaye yeye na Juma Nature ndio wa kwanza kusainiwa Bongo Records, ndiye msanii wa kwanza Bongo kumpa shoo AY nje ya Dar es Salaam wakati anaanza kuwika kimuziki, wawili hao walienda kutuimba Mwanza.
10. Nyimbo za AY ambazo amerekodi Bongo Records kwa P-Funk Majani hakuwahi kulipa fedha kutokana na ukaribu wake na Majani ambaye aliamua kufanya hivyo kutokana na kusapoti kipaji chake.
Na Majani aliyeanza ‘game’ akitumia jina la ‘DJ Skills of Pain’, ndiye aliyempa AY jina la ‘Mzee wa Commercial’ baada ya rapa huyo kubadili aina ya muziki wake. Pia Majani ndiye aliyemzoesha AY kuvaa kofia, hapo awali alikuwa sio mpenzi sana wa kuvaa kofia.