Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bambo, Kingwendu 'wagoma kuzeeka'

Muktasari:

WAKATI kizazi kipya cha wasanii kikizidi kutikisa tasnia ya burudani kwa mitindo mipya ya muziki, vichekesho na maudhui ya mitandaoni, wakongwe wa uchekeshaji Bongo, Bambo, Kingwendu na Mtanga wameamua kutokaa pembeni, wakijichanganya na vijana katika mazingira mapya ya sanaa.

WAKATI kizazi kipya cha wasanii kikizidi kutikisa tasnia ya burudani kwa mitindo mipya ya muziki, vichekesho na maudhui ya mitandaoni, wakongwe wa uchekeshaji Bongo, Bambo, Kingwendu na Mtanga wameamua kutokaa pembeni, wakijichanganya na vijana katika mazingira mapya ya sanaa.

Wakongwe hao, ambao wamejenga majina yao kwa miaka mingi kupitia uchekeshaji, sasa wanaonekana kuendelea kutafuta nafasi katika ulimwengu wa burudani unaobadilika kila siku.

Kinachowafanya wazungumzwe zaidi ni namna wanavyojaribu kuendana na kizazi cha sasa, ambacho kimejaa ubunifu wa mitandaoni, muziki na ushirikiano wa wasanii kutoka fani tofauti.


BAMBO: MIMI SIO MZEE

Bambo anaamini kuwa ili kazi ya sanaa iendelee kukua, wasanii wanahitaji kubuni njia mpya za kufanya kazi zao na kutafuta wadau wa kuwaunga mkono.

Akizungumzia mipango ya kukuza uchekeshaji, anasema suala la udhamini ni muhimu ili waweze kuandaa maonyesho yao ya stand-up comedy kwa ubora zaidi.

“Kikubwa ni kupata masponsor tu. Tunaweza tukatengeneza stand-up comedy zetu wenyewe ikawa nzuri, tukapata mwalimu wa kututengenezea stand-up comedy kukuza zaidi,” anasema Bambo.

Kauli hiyo inaonyesha kuwa pamoja na uzoefu alionao, bado anauona umuhimu wa kujifunza, kuboresha kazi na kutafuta fursa mpya zitakazowasaidia kufikia mashabiki wengi zaidi.

Bambo pia anaeleza namna alivyoanza kufikiria kuingia katika muziki baada ya kuona waimbaji wakipata nafasi na malipo katika shughuli mbalimbali za burudani.

“Sisi tulikuwa tunajiongeza baadhi ya wakati. Tukawa tunajiuliza kwa nini wenzetu hawa kina Dudu Baya, kina Mwana FA kipindi kile wanakutana kwenye 'ma-concert' mengi, lakini wenzetu wale wanawekwa kipao mbele sana kwamba ni waimbaji. Bambo akauliza, kwa nini mimi na Kingwendu hatuwezi kuimba? Tukasema kweli, kwa nini tusiimbe bwana? Tukajitahidi tukaimba,” anasema.

Kwa maelezo yake, hatua hiyo ilikuwa sehemu ya kujitafutia nafasi nyingine katika tasnia ambayo fursa zake hazikuishia kwenye uchekeshaji pekee.


KINGWENDU: VIJANA HAWA NI HATARI

Kwa upande wake, Kingwendu anaonekana kuvutiwa na uwezo wa vijana wa sasa kutumia maarifa na teknolojia kuboresha kazi zao.

Akizungumzia Chino Kidd, msanii anayejulikana kwa kuendana na mitindo ya muziki wa kizazi kipya, Kingwendu anasema kijana huyo ana namna yake ya kuendesha maisha na kazi zake.

“Chino anatumia maarifa sana, na sijawahi kuona Chino akiishi kwa shida. Chino anaenda na usasa, kila kitu kiko vizuri,” anasema Kingwendu.

Kauli hiyo inaonyesha namna anavyoutazama ubunifu wa vijana kama sehemu muhimu ya mafanikio katika mazingira ya sasa ya burudani.

Kingwendu anaongeza kuwa kizazi kipya kina uwezo mkubwa wa kujifunza mambo mengi kwa haraka, hivyo wasanii wakongwe wanapaswa kuwa tayari kujifunza na kwenda na mabadiliko ya wakati.

“Hawa vijana bwana kama AI. Hawa watoto wepesi, wanaweza kila kitu. Ukitaka uende na maisha, deal na vijana hawa, hawa wanakutoa,” anasema. Hata hivyo, Kingwendu hakuficha kutoridhishwa kwake na kile anachokiona kama kushuka kwa ubora wa baadhi ya kazi za uchekeshaji, akiwataka wasanii kutumia akili na uwezo wao badala ya kutegemea bwebwe pekee.


CHINO KIDD AINGIA KWENYE MCHAKATO

Katika kuunganisha vizazi hivyo, Chino Kidd ni miongoni mwa wasanii wanaotoa nafasi ya kuangalia namna ushirikiano unavyoweza kuwakutanisha watu wenye uzoefu tofauti katika burudani.

Akielezea wazo la mradi unaohusisha Father, anayejulikana pia kama Enock Plat, na Tony, Chino anasema alilikuta wazo hilo likiwa limeandaliwa na akaona lina nafasi ya kufanya vizuri.

“Idea ilikuwa ya Father (Enock Plat) na mwanaye Tony. Tony ni mtoto wa Bambo ambaye tuko wote pale tunafanya kazi pamoja. Nilikuja nikakuta hiyo idea ishatengenezwa, na mimi nikaona ni kitu kizuri sana na kitapokelewa kwa ukubwa kwa sababu unajua baraka zinatoka kwa wazazi,” anasema Chino Kidd.

Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuhusisha watu wenye uzoefu katika kutengeneza kazi zinazoweza kuwafikia mashabiki wa rika tofauti.

Kwa Bambo, Mtanga na Kingwendu, kuendelea kuwepo kwenye mazingira haya kunamaanisha kutafuta namna ya kutumia uzoefu wao bila kupuuza mabadiliko yanayoletwa na vijana.

Pia, kwa wakongwe hao, wanatamani kurudi katika kazi yao ya uchekeshaji kwa kushikwa mkono na kupewa sapoti na wadau ili kukuza tasnia ya uchekeshaji, na si kwenye muziki tu.