Aunty na Kusah: Miaka sita ya safari
Muktasari:
- Leo, miaka sita tangu kuanza kwa safari hiyo, Aunty na Kusah bado wanaonekana pamoja.
MIAKA SITA si michache kwenye penzi la mastaa, hasa pale linapokuwa limepitia maneno ya watu, mahusiano yaliyopita, ujauzito, watoto na maswali ya umri. Hiyo ndiyo safari ya Aunty Ezekiel na Kusah, penzi ambalo limeendelea kuzungumzwa tangu walipoanza hadi leo.
Kabla ya Kusah, Aunty alikuwa kwenye uhusiano na dansa Mose Iyobo, ambao uliwazalia mtoto Cookie. Kusah naye alikuwa ametoka kwenye uhusiano na msanii Ruby, ambaye walipata mtoto mmoja. Baada ya kila mmoja kuvuka ukurasa wake, njia zao zikakutana na penzi likaanza.
Lakini mwanzo huo haukuwa mwepesi. Aunty alikumbana na maneno amemchukulia Ruby mpenzi wake, huku uhusiano wake na Kusah ukizua mjadala.
Wakati huo pia kulikuwa na kipindi ambacho wawili hao walihusishwa na ujauzito wa Aunty, lakini hawakuwa tayari kuweka wazi kila kitu hadharani.
Novemba 2020, Aunty akajifungua mtoto wa kiume, Noman ‘Nono’, na hapo ukurasa mpya wa safari yao ukafunguka. Kutoka kuwa wapenzi, wakawa pia wazazi, huku uhusiano wao ukiendelea kufuatiliwa na mashabiki.
Kisha likaja suala lingine lililowahi kuwasha moto kwenye penzi lao, tofauti ya umri. Watu walizungumzia Aunty kuwa mkubwa kwa Kusah, lakini Kusah hakukubali hilo liwe sababu ya kuyumba kwao.
Aliwahi kusema familia yake inampenda Aunty na kumkubali kama sehemu ya maisha yake.
Hata Ruby hakubaki mbali kabisa na simulizi yao. Mwaka 2024, Kusah na Ruby walipotoa pamoja wimbo Leo, maswali yakarudi tena kuhusu uhusiano huo wa zamani.
Aunty hakutengeneza vita, bali aliupotezea mzigo huo na kuendelea na maisha yake pamoja na Kusah.
Mwaka 2025, safari yao ikapata sura nyingine baada ya Aunty kupata ujauzito wa pili akiwa na Kusah.
Machi 3 akajifungua mtoto wa kike, Zara, ambaye akawa mtoto wake wa tatu baada ya Cookie na Nono, na wa pili kati yake na Kusah.
Leo, miaka sita tangu kuanza kwa safari hiyo, Aunty na Kusah bado wanaonekana pamoja.
Septemba 2026, Aunty alimwandikia Kusah ujumbe wa kimahaba katika siku yake ya kuzaliwa, huku Kusah akimjibu kwa kumuita “mama wa wanangu.”