Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Agnes Masogange amekufa, lakini Jebby amekufa zaidi

Muktasari:

  • Staa wa sinema na vipindi vya televisheni Marekani, Bobby Driscoll, alifariki dunia Machi 30, 1968 lakini aligundulika takriban wiki nne baada ya kifo. Driscoll akiwa kwenye kilele cha mafanikio yake, alitopea kwenye ubwiaji wa dawa za kulevya. Alifikwa na mauti akiwa kwenye jengo lililotelekezwa.

Januari 24, mwaka huu, mwandishi Anna Fifield wa gazeti na mtandao wa The Washington Post, Marekani, aliandika ripoti jinsi Wajapan wengi kwenye Jiji la Kawasaki, Japan wanavyofariki dunia wakiwa wapweke na kusababisha miili yao kuoza ndani bila kugunduliwa na ndugu au majirani.

Staa wa sinema na vipindi vya televisheni Marekani, Bobby Driscoll, alifariki dunia Machi 30, 1968 lakini aligundulika takriban wiki nne baada ya kifo. Driscoll akiwa kwenye kilele cha mafanikio yake, alitopea kwenye ubwiaji wa dawa za kulevya. Alifikwa na mauti akiwa kwenye jengo lililotelekezwa.

Mwili wa Driscoll ulizikwa bila utaratibu maalumu na mamlaka za serikali. Baadaye mama yake, Isabelle Kratz, aligundua mwili wa Driscoll kwa kutambua alama za vidole, hivyo kulijengea kaburi la mtoto wake. Driscoll alikuwa staa mkubwa, lakini alikutwa na mauti kama chokoraa!

Anzia ripoti ya Anna Fifield wa The Washington Post kisha kifo cha Driscoll, unapata tafsiri kuwa kuna watu hufa ila wengine hufa zaidi. Inawezekana nyakati za mwisho wa uhai wake alitamani msaada ambao, ungeokoa maisha yake lakini hakupata. Nyakati za kumsaidia kumsitiri kwenye nyumba yake nazo zinapita.

Kila binadamu angependa akifikwa na mauti basi awe na ndugu au jamaa ambao watamsitiri kwa kufuata taratibu zote kwa mujibu wa imani yake. Hakuna mwenye kuombea afe peke yake, atoe harufu kisha aoze ndani au porini pasipo kufanyiwa mazishi.

Zaidi kila mtu hutamani mazishi ya heshima kulingana na tabaka lake. Mwanamichezo angependa akifa azikwe kama wanamichezo wengine mashuhuri waliopata kuzikwa kwa hadhi kubwa, msanii atawaza naye safari yake ihitimishwe mithili ya wasanii wenzake. Akifa na kukosa ‘kampani’ ya wenzake, huyo hufa zaidi.

MASOGANGE NA JEBBY

Aprili 20, mwaka huu, mwanamitindo wa video za muziki (video vixen), Agnes Gerald ‘Masogange’ alifariki dunia akiwa Hospitali ya Mama Ngoma, Dar es Salaam. Aprili 22, mwaka huu, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Janabi Mbaraka ‘Jebby’ alifikwa na mauti alipokuwa Hospitali ya Mkoa Dodoma.

Agnes aliagwa na idadi kubwa ya wasanii kwenye Viwanja vya Leaders Club, Aprili 22. Aprili 23, alizikwa nyumbani kwao Mbalizi, Mbeya. Siku Agnes aliyozikwa Mbalizi ndiyo ambayo Jebby alihifadhiwa kwenye makaburi wa Mailimbili, Dodoma.

Utaratibu wa kumuaga Agnes ulikuwa mzuri. Wasanii wenzake walijitoa kumwandalia mwenzao safari ya mwisho yenye heshima. Wengine walisafiri mpaka Mbalizi na wakahusika kikamilifu katika shughuli mbalimbali. Hakika familia ya Agnes imeona upendo wa wasanii kwa mtoto na ndugu yao.

Mambo mengi kwa Agnes yaliwezekana kutokana na imani yake. Kwa Wakristo, ibada ya kumuaga anayefikwa na mauti imerefushwa na watu hupata nafasi ya kumuona na kumtolea salamu za mwisho. Ni tofauti na mazishi ya Muislam. Imeagizwa mtu anapokufa basi azikwe haraka iwezekanavyo.

Kwa msingi huo hakukuwa na uwezekano kwa Jebby shughuli yake ya kumuaga kurefushwa kama Agnes. Pamoja na hivyo, namna Jebby na Agnes walivyozikwa na jinsi jamii ilivyopokea taarifa za vifo na taratibu za mazishi, utaona kwamba kuna mtu hakupewa heshima yake.

Kuna mtu alivutia jamii mbalimbali za watu maarufu, mwingine alihifadhiwa kana kwamba hakuwa na utambulisho mkubwa kwenye umma wa watu mashuhuri. Mmoja amezikwa kwa thamani iliyokuzwa, mwingine kwa hadhi iliyoshushwa.

NANI NI NANI?

Mwaka 2009 Agnes alionekana kwenye video ya wimbo mkubwa sana Tanzania wakati huo, unaoitwa Masogange, mali ya staa wa Morogoro, Abednego Damian ‘Belle 9’. Kuanzia hapo Agnes akapenya kwenye uso wa vyombo vya vyombo vya habari hasa magazeti, jina likawa Agnes Masogange.

Kuanzia hapo Agnes akawa anatambulika kama ‘modo’ wa video za muziki. Hata hivyo, maisha yake nje ya kazi zake hizo ndiyo yalimfanya aendelee kuwa gumzo. Mapenzi yake na skendo ya kutumika kusafirisha dawa za kulevya.

Julia 5, 2013, Agnes akiwa na mwenzake, Melisa Edward, walikamatwa Uwanja wa Ndege wa OR Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini ikidaiwa walikutwa na dawa za kulevya aina ya crystal methamphetamine zilizokuwa na thamani ya Sh6.8 bilioni.

Baadaye mashitaka yaligeuzwa na kuelezwa kwamba walichokutwa nacho kilikuwa ni kemikali hatari zisizoruhusiwa kuingia Afrika Kusini. Mahakama ya Kempton, Afrika Kusini ilimhukumu Agnes kifungo cha miezi 30 au kulipa faini ya Randi 30,000 (Sh4.8 milioni). Agnes alilipa faini na kuachiwa huru, Melisa yeye hakukutwa na hatia. Maisha ya Agnes yaliendelea kuwa ya visanga nje ya sanaa na mapema mwaka jana alikuwa mmoja wa waliokamatwa katika msako wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwahusu wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Hayo ndiyo maisha ya Agnes yaliyosababisha abebe umaarufu mkubwa kwenye jamii. Akawa hakatiki kwenye magazeti. Kwa mfuatiliaji na msomi wa vitabu vya video vixen, Karrine Steffans ambaye ametokea kwenye video nyingi za wasanii wakubwa wa muziki wa Rap Marekani hawezi kushangaa.

Karrine ameandika vitabu; Confessions of a Video Vixen (2005), The Vixen Diaries (2007) na The Vixen Manual: How to Find, Seduce & Keep the Man You Want (2009). Ndani yake ameeleza namna maisha ya video vixen yalivyo, anavyoweza kutoka na wanaume wengi maarufu, vilevile anavyoweza kumtongoza, kumpata na kumtunza mwanaume anatemtaka.

Upande wa Jebby ni mwanamuziki wa kitambo. Achana na nyimbo zake kama Kastory, Wanapagawa na nyinginezo, Jebby alitisha mno alipoachia Swahiba ambao alimshirikisha Mfalme wa Morogoro, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’. Swahiba ni wimbo ambao bila shaka hautakufa. Hivyo Jebby ataendelea kuishi redioni na mitandaoni.

Kwa kutafsiri kazi, Jebby ni mkubwa na alistahili mazishi ya heshima kuliko ya Agnes. Tatizo sanaa ya Bongo, vitimbi (drama) nje ya sanaa hupata malipo makubwa, ndiyo maana Agnes msiba wake umevuta wengi kuliko Jebby. Ni sawa kusema Jebby alistahili heshima aliyopewa Agnes.

TATIZO LILIPO

Ni kweli drama zinateka soko la muziki. Hutokea wasanii wanatoa kazi nzuri, lakini wenye vioja vingi wanang’ara kuliko. Hata hivyo, katika suala la mazishi ya Agnes na Jebby, shida kubwa ipo kwa wanamuziki wa Bongo Fleva ambao, walipaswa kujitoa kwa mwenzao.

Mara nyingi wasanii wa Bongo Movie huzodolewa kuwa wanapenda maonesho na kudandia matukio ya kukuza majina yao. Hata la Agnes walilibeba wao, wakawavuta wanamuziki wa Bongo Fleva, wanamichezo na viongozi wa serikali kushiriki na kumzungumzia Agnes. Maneno ya maombolezo ya Agnes unaweza kusema si yule wa vitimbi na ambaye Aprili 3, mwaka huu alikutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya, hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini Sh1.5 milioni kisha akamudu kulipa faini. Salamu za rambirambi zilimtakasa kweli. Tatizo walijikausha kama haliwahusu. Wana’Bongo Fleva hawajamtendea haki mwenzao.