Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

911, Nandy alikosa kitu?

NANDY Pict

Muktasari:

  • Albamu hiyo iliyotoka usiku wa kuamkia Novemba 27, 2026, imekuja baada ya miaka minane tangu Nandy alipotoa albamu yake ya The African Princess mwaka 2018.

MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, amezindua albamu yake mpya ya 911, yenye nyimbo 16, akiwashirikisha wasanii 10 kutoka mataifa mbalimbali, akiwemo Tiwa Savage, Sheebah, Rayvanny, Nyashinski, Ferré Gola, Jux na Marioo. Uzinduzi huo ulifanyika Dovenest Garden, Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Albamu hiyo iliyotoka usiku wa kuamkia Novemba 27, 2026, imekuja baada ya miaka minane tangu Nandy alipotoa albamu yake ya The African Princess mwaka 2018.

Pamoja na majina makubwa ya wasanii waliomo ndani ya albamu hiyo na maandalizi ya uzinduzi, tukio hilo lilikuwa na mambo yaliyovutia, lakini pia likaacha swali: Kwa nini ukubwa wa kampeni ya kuitangaza albamu hiyo haukuendana na tukio lenyewe?


NAND 01

RANGI NYEKUNDU YATAWALA

Rangi nyekundu ndiyo iliyotawala katika uzinduzi huo, kuanzia kwenye mapambo hadi muonekano wa jukwaa, ikionekana kuwa sehemu ya utambulisho wa albamu ya 911.

Hata katika kampeni ya kuitangaza albamu hiyo, Nandy alitumia gari la zimamoto, ubunifu uliosaidia kuongeza utofauti na kuipa kazi hiyo taswira ya kipekee kabla ya uzinduzi.


NAND 03

ACHEZA NA MASHABIKI

Moja ya mambo mazuri yaliyoonekana ni namna Nandy alivyowashirikisha mashabiki wake katika burudani badala ya kubaki jukwaani na kutumbuiza pekee.

Alionekana kucheza nao na kufurahia uwepo wao, huku akitumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa mapenzi na sapoti wanayoendelea kumpa katika safari yake ya muziki.

Mwingiliano huo ulikuwa miongoni mwa sehemu zilizoongeza ladha ya tukio, ukionyesha kuwa pamoja na uzinduzi wa albamu, Nandy hakuwasahau watu wanaounga mkono kazi zake.


NAND 02

WASHIRIKISHWA HAWAKUWEPO

Licha ya albamu ya 911 kuwa na majina makubwa ya wasanii 10 akiwemo Tiwa Savage, Sheebah, Rayvanny na Nyashinski, idadi ya washirikishwa waliojitokeza katika uzinduzi huo haikuendana na matarajio yaliyokuwepo.

Katika tukio hilo, Sheebah ndiye aliyeonekana miongoni mwa wasanii walioshirikishwa kwenye albamu hiyo, huku Tiwa Savage, ambaye mashabiki walikuwa wakimsubiri, pamoja na wengine, akikosekana.

Uwepo wa wasanii hao ungeweza kuongeza ladha ya uzinduzi, hasa kwa mashabiki waliotamani kuona baadhi ya nyimbo zilizofanyika studio zikipata nafasi ya kuimbwa kwa pamoja jukwaani. Hata hivyo, kushirikishwa kwa msanii kwenye albamu hakumaanishi kwamba ni lazima awepo siku ya uzinduzi.


NAND 04

GARDEN ILIPOA

Tofauti na baadhi ya wasanii wanaogeuza uzinduzi wa albamu zao kuwa matamasha makubwa yenye burudani na maonesho ya aina mbalimbali, uzinduzi wa Nandy uliofanyika Garden haukuonekana kuwa na msisimko mkubwa uliotarajiwa.

Mfano ni Diamond Platnumz alipozindua albamu yake ya A Boy From Tandale Machi 2018 nchini Kenya. Tukio hilo lilikuwa na burudani za aina mbalimbali, huku akitumbuiza nyimbo zake kabla ya kumkaribisha Omarion jukwaani na kutumbuiza naye kwa pamoja wimbo wao African Beauty.

Harmonize naye, alipozindua albamu yake ya Afro East mwaka 2020 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, aliandaa shoo iliyohudhuriwa na viongozi na mastaa wengi, akiwemo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Matukio hayo yanaonyesha namna uzinduzi unavyoweza kuwa zaidi ya kutambulisha nyimbo, bali pia kutoa burudani inayobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki.

Hata Nandy Festival zake zimekuwa zikichangamka zaidi, zikiwa na mwingiliano mkubwa na mashabiki. Hivyo, albamu ya 911 ilihitaji nguvu zaidi katika upande wa burudani ili kufikia matarajio yaliyowekwa na jina la Nandy.


AMWAGIWA SIFA

Pamoja na hali hiyo, uzinduzi haukukosa sura za mastaa. Miongoni mwa waliojitokeza kumuunga mkono Nandy ni Jokate Mwegelo na mtayarishaji wa muziki S2kizzy.

Wawili hao walimwagia sifa Nandy kutokana na safari yake ya muziki na hatua aliyofikia, huku wakitambua juhudi zake katika kuendelea kukuza muziki wake.

Kwa upande wa S2kizzy, uwepo wake ulikuwa na uzito zaidi kutokana na nafasi yake katika utengenezaji wa muziki, kwani pia alishiriki katika uzalishaji wa albamu hiyo.

Ujio wa mastaa hao uliongeza uzito wa wageni waliohudhuria, huku ukionyesha kuwa Nandy anaungwa mkono na watu mbalimbali ndani ya tasnia ya burudani.


NAND 05

HAKUBADILISHA NGUO

Katika upande wa mavazi, Nandy aliendelea na muonekano uleule bila kubadilisha nguo, tofauti na baadhi ya matukio makubwa ya muziki ambako wasanii hutumia mavazi mbalimbali kuongeza mvuto wa jukwaa.

Mabadiliko ya mavazi yanaweza kuwa sehemu ya burudani, hasa kwa msanii anayekuwa na ratiba ya kutumbuiza nyimbo nyingi mbele ya mashabiki.

Ingawa mavazi si kipimo pekee cha ubora wa uzinduzi, mabadiliko ya muonekano yangeweza kuongeza ladha nyingine katika jukwaa la 911.


BILLNASS ALIKUWEPO, LAKINI KAMA HAYUPO

Mumewe Nandy, mwanamuziki Billnass, pia alikuwepo katika uzinduzi huo kuonyesha sapoti kwa mkewe katika hatua hiyo muhimu ya safari yake ya muziki.

Hata hivyo, uwepo wake haukuonekana kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza shamrashamra za tukio hilo, kwani muda mwingi alionekana akiutumia kwenye simu yake.

Pamoja na hali hiyo, Billnass alionekana kucheza na mkewe wakati wa kutumbuiza mojawapo ya nyimbo zake, jambo lililoonyesha kuwa hakuwa amekaa pembeni wakati wote wa burudani.