Ndoto ya Stara Thomas ilivyogeuka kuwa kweli
Muktasari:
- Stara Thomas ambaye ametoa albamu na kushinda tuzo, ametengeneza muziki ambao hadi sasa unaishi huku ukibeba kumbukumbu nzuri kwa mashabiki. Fahamu zaidi.
KATI ya waimbaji wa kike waliochangia kuipa nguvu Bongo Fleva, basi jina la Stara Thomas nalo lipo katika orodha hiyo baada ya nyota yake kuanzia kung'aa mwanzoni kabisa mwa miaka ya 2000.
Stara Thomas ambaye ametoa albamu na kushinda tuzo, ametengeneza muziki ambao hadi sasa unaishi huku ukibeba kumbukumbu nzuri kwa mashabiki. Fahamu zaidi.
1. Wanamuziki waliomvutia hadi kujiona na yeye anaweza kuja kufanya muziki ni pamoja Lionel Richie, Whitney Houston, Papa Wemba, Tabu Ley, Mbilia Bel, Tshala Muana na Yvonne Chaka Chaka wa Afrika Kusini.
2. Kipindi Stara Thomas akiwa shule alipenda sana kuimba nyimbo za Mariah Carey, mkali wa kibao cha All I Want for Christmas Is You (1994) ambacho hurejea kwenye chati kila mwisho wa mwaka.
3. Kutokana na aina ya sauti yake, Stara Thomas alipendelea pia kuimba na nyimbo za rapa wa kike kutokea Marekani, T-Boz (Tionne Watkins) aliyetamba na kundi la TLC, kitu kilichokuza uimbaji wake kwa wakati huo.
4. Kabla ya kuvuma katika miondoko ya Zouk, Stara Thomas aliandika kurekodi nyimbo kadhaa za Kiingereza, baadhi ya hizo ni Children's Right na My Body.
5. Akiwa bado hajatoka kimuziki, tayari Stara Thomas alishaanza kuimba pamoja na bendi maarufu Tanzania, zikiwemo The Kilimanjaro Band na In Africa Band.
In Africa Band wanakumbukwa na wengi kupitia wimbo wao 'Indege' ambao mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nandy alichukua vionjo vyake na kuvitumia katika wimbo wake wa Amapiano, Mchumba.
6. Wanamuziki wa kimataifa aliotamani kufanya nao kazi ni Akon na Mary J. Blige, rapa aliyetoka na albamu, What's the 411? (1992) inayotajwa kuwa ya kwanza duniani kwa kuchanganya R&B na Hip Hop katika utamaduni wa Pop.
7. Akiwa na In Africa Band, Stara Thomas alikutana na DJ Boniluv na kupata nafasi ya kurekodi Mawingu Studio, sehemu ambayo imewatoa wasanii kadhaa akiwemo Mwana FA ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
8. Hatimaye Stara Thomas alitoka kimuziki kupitia wimbo wake, Mimi na Wewe (2000) uliotayarishwa na Master J katika studio za MJ Records, zamani MJ Production.
9. Wimbo 'Mimi na Wewe' ndio ulioibeba albamu yake ya kwanza, Nyuma Sitorudi (2000), kisha albamu yake ya pili, Hadithi (2002) akaja na wimbo wake mwingine maarufu, Nipo kwa Ajili Yako.
10. Hadi sasa Stara Thomas amefanikiwa kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) akishinda kipengele cha Msanii Bora wa Kike 2003, na Wimbo Bora wa Kushirikiana (Nipigie) 2010 akiwa na AT, msanii wa zamani wa kundi la Offside Trick kutokea Zanzibar.