Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zuchu, Nandy ni kiki, bifu? Iko hivi!

Muktasari:

  • Kinachoongeza uzito wa mjadala huo ni, wakati majibizano hayo yakizidi, Nandy yupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuachia albamu yake mpya 911, Novemba 27, 2026, huku tarehe hiyo hiyo ikihusishwa na mipango ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Zuchu.

MITANDAO ya kijamii imewaka moto baada ya wasanii wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Faustina Mfinanga ‘Nandy’ kutupiana maneno na kinachoonekana kuna tofauti baina yao.

Kinachoongeza uzito wa mjadala huo ni, wakati majibizano hayo yakizidi, Nandy yupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuachia albamu yake mpya 911, Novemba 27, 2026, huku tarehe hiyo hiyo ikihusishwa na mipango ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Zuchu.

Hali hiyo imeibua maswali. Lakini, je ni bifu lililofika hatua ya kuanikwa hadharani au ni mbinu ya kutengeneza gumzo kwa sababu ya kazi mpya za muziki?


MOTO UMEANZA WAPI?

Katika siku za hivi karibuni, Zuchu amekuwa akieleza madai mbalimbali yanayohusisha Nandy, akigusia mambo ambayo anadai yamekuwa yakitokea kwa muda, ikiwemo suala la mitindo ya urembo, watu waliowahi kufanya kazi naye na matukio ambayo ameyatafsiri kama ishara za kutokuelewana.

Zuchu pia amegusia ushindani wa matukio, akidai baada ya yeye kutangaza shughuli yake ya Imbeju, Nandy naye alitangaza tamasha, jambo ambalo amelihusishwa na tofauti zao.

Nandy hakubaki kimya, akihusisha kauli za Zuchu na maandalizi ya albamu yake mpya, akionyesha kushangazwa na majibizano hayo wakati ametangaza orodha ya nyimbo za 911.

NOVEMBA 27 KUNA NINI?

Hapa ndipo kwenye utata. Kuhusu albamu na siku ya kuzaliwa.

Ni hivi. Nandy alitangaza ujio wa albamu yake ya 911 itatoka Novemba 27, yenye nyimbo 16, huku wimbo ‘Oya’ ukiwa miongoni mwa kazi zilizotangulia kutolewa.

Albamu hiyo inakuja ikiwa ni miaka minane tangu atoe ya kwanza ya The African Princess iliyotoka mwaka 2018.

Wakati huo huo kumekuwa na taarifa za uwepo wa sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Zuchu.

Ilielezwa upangaji wa sherehe hiyo ilikuwa ni ili kuingilia uzinduzi wa albamu hiyo jambo ambalo Zuchu amelipinga na kuna taarifa ya kuahirishwa.

Sherehe hiyo inaelezwa ilikuwa iwakutanishe mastaa wakubwa akiwamo Diamond Platnumz ambaye ni mume wa Zuchu.


WASANII WAPITA NA 27

Wakati Novemba 27 ikitajwa kwa wasanii hao wawili kuhusu albam ya 911 na sherehe ya kuzaliwa, huku nyuma baadhi ya wasanii wameitumia tarehe hiyo kuachia ngoma zao mpya.

Tarehe hiyo imekuwa ikitajwa kwenye burudani na hivyo kutumiwa kama fursa katika kazi na ushindani wa wasanii hao.


WALIKUWA MARAFIKI

Historia ya wawili hao inafanya mjadala huu kuwa na uzito zaidi. Mwaka 2015 na 2016, walikuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano ya muziki ya Tecno Own The Stage, yaliyowakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Nandy aliwahi kueleza walikuwa karibu na walikuwa wakitafuta maisha ya muziki pamoja, lakini baadaye walipotezana kutokana na majukumu na mabadiliko ya safari zao za kisanii.

Mwaka 2021 na 2022, Nandy aliwahi kuzungumzia madai ya bifu kati yao, akisisitiza walikuwa na urafiki, huku Zuchu naye akiwahi kueleza hakuwa na bifu na Nandy.

Mwaka 2023, Zuchu alionekana kumpongeza Nandy baada ya kutangaza kuanzisha lebo yake ya The African Princess, akimuita ‘Da Fau’ na kumtakia mafanikio.


AROBAINI WALIKUWA PAMOJA

Ushahidi mwingine wa ukaribu wao ni Septemba 10, 2026, kwenye Henna Night ya Zuchu kuelekea Arobaini ya mtoto wake Sandrah Naseeb. Nandy alihudhuria akiwa na mumewe Billnass, wakacheza na kufurahia pamoja na wageni wengine.

Septemba 12, wawili hao walikutana tena kwenye Arobaini ya Sandrah iliyofanyika Saint Laurent Garden, Kawe, Dar es Salaam. Uwepo wa Nandy katika matukio hayo, akiwa na mumewe, ulionyesha wakati huo walikuwa na ukaribu wa kijamii.

Septemba 17, Nandy alizungumza tena kuhusu urafiki wao na hawana bifu na wamekuwa wakikutana hata nje ya macho ya mashabiki, ikiwemo studio. Alisema pia waume zao, Billnass na Diamond ni marafiki na wamekuwa wakisaidia kuendeleza maelewano yao.

Hali hiyo inafanya majibizano ya sasa kuwa na maswali zaidi: Je, kuna jambo lilitokea baada ya Septemba hadi sasa likabadilisha uhusiano wao, au ushindani wa muziki na kulinganishwa kwao ndio umechangia mvutano huu?


BIFU HALISI AU KIKI?

Kwa kuangalia historia yao, kuna sababu za kujiuliza kama tofauti hizi ni za kweli au zimechochewa na mazingira ya sasa ya muziki.

Majibizano yamekuja wakati Nandy anajiandaa kuachia albamu, huku Novemba 27 ikiwa na matukio na kazi mbalimbali zinazohusishwa na mastaa.

Hata hivyo, si sahihi kuhitimisha kuwa kila kinachotokea ni kiki. Zuchu ameeleza madai yanayoonyesha kuna mambo yanayomkera na Nandy amejibu kwa namna inayoonyesha haoni majibizano hayo kuwa ya kawaida.

Huenda kukawa na tofauti za kweli ambazo zimeibuka hadharani katika kipindi ambacho kila mmoja ana kazi zinazohitaji 'attention', na matokeo yake majibizano hayo yakawa na faida ya ziada katika kutengeneza gumzo.

Kwa sasa, macho ya mashabiki yameelekezwa Novemba 27, siku ambayo 911 inatarajiwa kutoka. Je, majibizano haya yataendelea, yatapoa au yatazua sura nyingine ya ushindani kati ya mastaa hao?

Swali kubwa linalobaki: Zuchu na Nandy kweli wamefikia hatua ya kuwa maadui au ni ushindani wa wasanii wawili wakubwa ambao sasa umeingia kwenye hatua ya kuzungumzwa hadharani?

Hata hivyo, ikumbukwe hii siyo mara ya kwanza kwa wasanii kuonyesha wana utofauti kumbe ni kwa ajili ya kusukuma kazi zao zifanye vizuri.

Dunia ya muziki imekuwa na ushindani kwa miaka mingi na bifu hizo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuunyanyua.

Walipita kina 2Pac Shakur na Notorious BIG, Juma Nature na Inspector Haroun, 50 Cent na Ja Rule, Cardi B na Nick Minaj, Hadija Kopa ambaye ni mama wa Zuchu na Nasma Hamis (marehemu) na nyingine zote na hizo ziliwasaidi kunyanyua kazi zao na kupata mafanikio.