2Baba kuwarudisha Wabongo ya mwaka 2005
Muktasari:
- 2Baba ambaye majina yake kamili ni Innocent Ujah Idibia hii itakuwa mara ya pili kufanya shoo nchini na ya kwanza ni Agosti, mwaka 2005 katika tamasha la Fiesta, akitamba na wimbo wake wa African Queen, uliotoka mwaka 2004.
MSANII mkongwe wa Afro Pop kutoka Nigeria, 2Baba anatarajiwa kupanda katika jukwaa la Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, litakalofanyika jijini Mbeya, Novemba 7, 2026.
2Baba ambaye majina yake kamili ni Innocent Ujah Idibia hii itakuwa mara ya pili kufanya shoo nchini na ya kwanza ni Agosti, mwaka 2005 katika tamasha la Fiesta, akitamba na wimbo wake wa African Queen, uliotoka mwaka 2004.
Wimbo huo ndiyo uliomfungulia milango katika muziki ndani na nje ya Nigeria na kupata shoo nyingi. Pia alikuwa na nyingine kali kama, ‘Nfana Ibaga (No Problem)’,’Ole (Thief)’, ‘Right Here’, U No Holy Pass na nyingine nyingi katika Albamu ya Face 2 Face.
Katika kazi hizo, amejenga jina kwa kuimba kuhusu mapenzi, maisha na changamoto zinazogusa watu wa rika tofauti.
Huyu ni msanii wa pili mkubwa wa kimataifa kupanda katika tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, baada ya Mr Cheecks kutoka Marekani kunogesha lile la Arusha.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha wasanii wakongwe wa Bongo Fleva na Mbeya unakuwa mkoa wa sita, likiendelea kuwakutanisha na mashabiki wao walioanza nao miaka ya nyuma na ili kurudisha heshima ya muziki wa kitambo.
Ujio wa 2Baba unatarajiwa pia kumkutanisha na mashabiki wa nyimbo zake tangu 2004 alipotoa African Queen ulioshika chati na kumpa jina, pia litamkutanisha na kizazi kipya cha muziki kwa vijana (GenZ).
Katika safari yake ya muziki, 2Baba ameachia albamu kadhaa, zikiwemo Face 2 Face (2004), Grass 2 Grace (2006), The Unstoppable (2009), Away & Beyond (2012), The Ascension (2014) na Warriors (2020).
Kazi hizo zinaonyesha safari yake ya zaidi ya miongo miwili katika tasnia ya muziki, akiendelea kutoa kazi katika vipindi tofauti vya mabadiliko ya muziki wa Afrika.