Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunda Man anavyopita na upepo wa Simba

TUNDA MAN Pict

Muktasari:

  • Baada ya Simba kushinda mabao 6-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea, msanii huyo alionekana katika gari akiwa na washikaji zake akiimba wimbo unaohusu timu hiyo.

MSANII wa Bongo Fleva, Tunda Man anajua kupita na upepo wa Simba. Klabu hiyo inapofanya vizuri, mara nyingi amekuwa akiachia nyimbo za kuisifia, jambo linalorahisisha mashabiki wa timu hiyo kuzisikiliza.

Baada ya Simba kushinda mabao 6-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea, msanii huyo alionekana katika gari akiwa na washikaji zake akiimba wimbo unaohusu timu hiyo.

Baadhi ya maneno yaliyosikika katika wimbo huo yalihusu mechi ya marudiano iliyopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita, wapinzani wa Simba watakimbia kwa kuogopa kuingiza timu uwanjani wakihofia kufungwa mabao mengi zaidi.

Pia, alimtaja mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Doumbia, akifurahia kuanza safari yake ya kucheka na nyavu.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya nyimbo ambazo kwa kiasi kikubwa amezitoa baada ya Simba kufanya vizuri na ambazo zimekuwa zikitamba katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mfano Instagram na TikTok, ambako mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakizitamba nazo.

Ingawa huisifia Simba, lakini nyuma ya jambo hilo ananufaika kwa kupata sapoti ya mashabiki pamoja na shoo, mfano zile za Simba Day ambako amekuwa akitumbuiza kwa nyakati tofauti.


TUNDA 01

SIMBA TUNAJIDAI

Wimbo huo aliuachia Julai 26, 2021, wakati Simba ilipokuwa ikichukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya mwisho msimu wa 2020/21. Baadhi ya maneno yaliyokuwa yakisikika katika wimbo huo yalihusu kujidai na Simba yao na wapinzani hawawawezi.


TAMBENI

Wimbo huo aliuachia Julai 15, 2020, wakati Simba bado ilikuwa ikifanya vizuri katika Ligi. Video yake ilihusisha kwa kiasi kikubwa mashabiki wa timu hiyo waliovalia jezi nyekundu.

Pia, walionekana baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo, kama Meddie Kagere, ambaye alionyesha staili yake ya kushangilia kwa kufumba jicho moja, pamoja na Pascal Wawa na John Bocco.

Akizungumzia jambo hilo, Kagere anasema: “Unapofanya vizuri, nilichokiona kwa Simba ni rahisi mashabiki au wanamuziki kukuunga mkono. Ndicho kilichofanyika, ingawa kwa nyakati hizo, kama mchezaji, inakuwa vigumu kujua kila kitu, kwani akili inakuwa inawaza kazi zaidi.”


TUNDA 02

KWA MKAPA HATOKI MTU

Wakati Simba ilipokuwa ikifanya vizuri katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, Tunda Man alitoa wimbo wa Kwa Mkapa Hatoki Mtu, Machi 30, 2022. Hiyo ilikuwa kaulimbiu ya mashabiki wa Simba.

Timu hiyo ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa katika msimu wa 2021/22, ilipotolewa na Wydad Casablanca ya Morocco. Wimbo huo ulikuwa ukitumika kuhamasisha mashabiki uwanjani.


TUNAITAKA NUSU

Wimbo huo aliutoa Machi 2024, Simba ilipokuwa hatua ya robo fainali, lakini ikafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ilikotolewa na RS Berkane ya Morocco, kipindi hicho ilikuwa inanolewa na Fadlu Davids, ulikuwa ukipigwa uwanjani ulikuwa na mwitikio wa mashabiki.


TUNDA 03

HATA HATURINGI

Wimbo huo aliuachia Oktoba 21, 2022. Nyimbo nyingine ni Simba Africa, Simba na Simba Sihami, ambao ndani yake anasikika akisema watampiga hadi wamuue, lakini hafikirii kuacha kuishabikia klabu hiyo.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, anasema: “Raha ya Simba msimu huu wa 2026/27 ni imezifunga Azam, Yanga na kimataifa inafanya vizuri. Kubwa zaidi ni kitendo cha Ibrahim Doumbia kufunga mabao mawili. Sasa hivi ni mwendo wa ngapi ngapi, mwendo wa sita sita.”

Upekee wa Tunda Man ni kuwa na nyimbo nyingi za Simba, tofauti na wasanii wengine waliowahi kuimba zile zinazohusiana na klabu hiyo.