Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Damian Soul: Mapopo ilianzia ‘Club’

MAPOPO ni moja ya vibao vinavyotesa kwa sasa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni hapa nchini.

Wimbo huo ambao una mahadhi ya nyimbo za Afrika Kusini - mtindo unaojulikana kama Amapiano uliachiwa Desemba, mwaka jana.

Licha ya kuachiwa mwezi huo, hivi sasa ndio kama unazidi kushika kasi kwa namna ambavyo umekuwa ukipendwa.

Mwandishi wa makala haya alifanya mahojiano na mwimbaji wa wimbo huo, Damian Mihayo maarufu kama Damian Soul kujua wazo la wimbo huo lilipotokea na historia yake kwa ujumla katika muziki.

Damian anasema wazo la wimbo wa Mapopo lilikuja akiwa anasoma nchini Uganda, ambapo rafiki yake waliyekuwa wanasoma naye huko alimuunganisha na rafiki mwingine wa Afrika Kusini anayemtaja kwa jina la Nhlonipho ambaye alimueleza kuwa anapenda jinsi anavyoimba na alifanya kazi ya kuwaunganisha hadi kufika hatua ya kutoa kibao hicho.


SAFARI KIMUZIKI

Mwishoni mwa 2010, Damian anasema ndio alianza kazi ya sanaa na alianzia kanisani, na mwaka 2011 alitoa kibao cha kwanza kinachokwenda kwa jina la ‘Hakuna Matata’.

“Wakati natoa kibao cha Hakuna Matata, watu walipata tabu kunijua mimi ni msanii wa nchi gani na wengine kunifananisha na wasanii wa Kenya kwani licha ya wimbo huo kutoka mapema lakini ulijulikana zaidi baada ya miezi sita,” anasema msanii huyo.

Ukiachilia hapo alishiriki katika mashindano kadhaa ikiwemo Tusker Project Fame msimu wa tano na kuingia katika 10 bora.

Baada ya hapo alifanya wimbo na Jo Makini ulioitwa ‘Nipenzi’ ambapo anaeleza ulikuwa wimbo mzuri kwani ulitajwa pia kwenye tuzo za Kili Music Awards kama wimbo bora wa RnB.

Wimbo mwingine ni ‘Tudumishe’ alioufanya na G Nako miaka mitano iliyopita na ule wa Kaumba alioufanya na Vanessa Mdee mwaka 2016, ambapo licha ya kuwa wimbo uliofanya vizuri ndani na nje ya nchi, lakini hakuwahi kuufanyia video.

“Baada ya hapo nilikuwa kimya kutokana na kuwa bize na shoo mbalimbali za ndani na nje ya nchi, hivyo kunifanya kuachia nyimbo mbili au tatu kwa mwaka,” anasema.

Nyimbo nyingine ni Dat aliowashirikisha Nikki wa Pili na Quick Racka. EP aliyomshirikisha Barnaba ya nyimbo za injili inayoitwa ‘Asante’ iliyotoka mwaka juzi.

Baadhi ya matamasha aliyokuwa anaonekana sana, Damiana anayataja kuwa ni pamoja na Zanzibar International Film Festival (Ziff), Sauti za Busara na Jahazi Festival, hivyo akawa amebanwa kwenye maandalizi.

Hata hivyo mwaka jana alikuwa na mpango mkubwa, lakini kutokana na janga la virusi vya corona ndio akaachia wimbo wa Nothing But Love mwezi Septemba, PS I love U (Mwantumu) uliotoka Novemba na mwishoni mwa Desemba ndio akaachia wimbo wa Mapopo.

Anasema waliamua kuuachia mwezi huo kwa kuwa waliona ni kipindi cha likizo ambacho watu wanatakiwa kujiachia na mwishoni mwa Januari ndio ulianza kusikika zaidi.


'KU-HIT' KWA MAPOPO

Sababu ya ku-hit kwa wimbo huo, Damian anasema ni kipindi tu kwa kuwa muziki ni kama kamari, kwani kuna ambao walimjua kutokona na nyimbo alizowahi kutoka nazo huko nyuma wakiwemo waliomjua kupitia Mapopo.

Anasema muziki wa Amapiano ni kati ya ile inayopendwa kwa sasa, hivyo nayo ni moja ya sababu ya kuifanya ifanye vizuri.

Hata hivyo, anasema katika kuitambulisha alianzia kwenye kumbi za muziki tofauti na wasanii wengi kwa sasa hupenda kuachia kupitia mitandaoni kama You tube au redio na televisheni.

“Niliupeleka wimbo wangu moja kwa moja kwa madj, lengo likiwa kuwafuata watu wengine, kwani madj nao wana mchango mkubwa katika kutangaza kazi zetu,” anasema.


KUPAA KIMATAIFA

Damiana anasema licha ya Tanzania kuwa na wasanii wenye vipaji, bado kazi hiyo haijawekewa msisitizo katika uwekezaji na ndio maana haiifikii vyema katika soko la kimataifa kama ilivyo wenzao kutoka nchi za Nigeria, Afrika Kusini na mataifa mengine ya Afrika Magharibi.

Uwekezaji huo anasema ungetakiwa uanzie kwenye ngazi ya familia badala ya kuacha mtu kusota mwenyewe na kumthamini anapoanza kuonyesha matunda.

“Tunavyokazania kuwapeleka watoto shule, pia kunapoonekana kipaji katika familia zetu, basi tuwaunge mkono watu wa aina hii kwani kipaji ni kama biashara ya madini, inapoamua kukutoa inakutoa kweli,” anasema Damian.

Anasema serikali inapaswa kutia mkono ikiwemo kulinda kazi za wasanii kwa hali yoyote ile ili waweze kunufaika na kazi zao.

“Kama haitoshi kuwekeza katika elimu ya sanaa, kwani wengi walioingia kwenye kazi hiyo utasikia mimi nilikuwa muuza matunda, nilikuwa muuza nguo na kadhalika, hivyo kunakuwa na vipaji visivyokuwa na elimu ya biashara hiyo ya muziki.”