Sauti za Busara kumenoga, wasanii kila kona

Muktasari:

Tamasha la  17 la Sauti za Busara limezinduliwa rasmi leo Februari 13 visiwani  Zanzibar huku wakiwaenzi  wa moja wa waasisi  wa tamasha hilo ambao ni Ruge Mutahaba na  Makame Faki Makame ambao ni marehemu kwa sasa

SAUTI za Busara moja  ya Tamasha kubwa barani Afrika limezinduliwa jana Ijumaa eneo la kihistoria  la Ngome Kongwe likiwa na orodha kubwa ya wasanii kutoka kila kona.

Akizungumza na Waandishi wa Habari  visiwani Zanzibar  hapa, Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud aliwasihi Watanzania na wageni ambao wamefika kutoka kila kona ya ulimwengu kujumuika kwa pamoja na kushuhudia kwa kushiriki tukio hilo la aina yake.

“Tunaanza tamasha hili la aina yake katika mwaka, wakati Zanzibar itakuwa inaandaa siku nne mchana na usiku bila kusimama kwa muziki wa kiafrika chini ya anga la Afrika, tamasha lina majukwaa matatu ambayo yote kwa asilimia 100 wanamuziki watapiga muziki ‘live’ ikiwamo muziki utakaokuwa unapigwa bure kwenye bustani za Forodhani” alisema  Mahmoud

Mwenyekiti wa bodi  ya Busara promotion  Mohamed Simai , ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar amesema ni furaha kuona wazo la watu saba leo limekuwa wazo la watu wengi ambao wanapata faida nalo.

"Tulianzisha tamasha hili watu saba leo hii limekua na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi, jamii inafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na tamasha hilo" alisema Sumai.

Aliongeza kuwa katika timu ya watu saba waasisi wa tamasha hilo alikuwepo Marehemu Ruge Mutahaba pamoja na Mzee Makame Faki Makame ambapo hili ni tamasha la 17 la Sauti za Busara.